Prime
Wakulima wa mahindi wasikilizia tamko la bei Jumatatu
Muktasari:
- Bei mahindi inatajwa kuwa kati ya Sh5, 000 hadi Sh7,000 kwa debe moja (ndoo ya kilo 20), tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita wa kilimo ambapo ilifika hadi zaidi ya Sh8,000 kwa maeneo ya mjini.
Mikoani. Wakati wakulima wakilalamika kuporomoka kwa bei ya mahindi, Serikali imewataka kuwa wavumilivu hadi Jumatatu Julai 20, 2026 ambapo itatoa mwongozo rasmi wa kuanza ununuzi wa zao hilo, utakaofanywa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Bei ya mahindi inadaiwa kuporomoka kutokana na mazao mengi kuingia sokoni kwa wakati mmoja, jambo linalosababisha kusababisha adha kwa wakulima.
Nyanda za Juu Kusini yenye mikoa saba, mbali na kuwa kinara katika kilimo cha mazao ya chakula, mahindi ndilo zao linaloendesha maisha yao kwa sehemu kubwa na hata Taifa kwa ujumla.
Kwa sasa, bei mahindi inatajwa kuwa kati ya Sh5, 000 hadi Sh7,000 kwa debe moja (ndoo ya kilo 20), tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita wa kilimo, ambapo ilifika hadi zaidi ya Sh8,000 kwa maeneo ya mjini.
Kutokana na kilio hicho, hivi karibuni, akiwa ziarani mkoani Songwe, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo alisema Serikali inatambua changamoto ya kushuka kwa bei ya mahindi kutokana na mazao mengi kuingia sokoni kwa wakati mmoja, hali inayowapa baadhi ya wanunuzi nafasi ya kushusha bei na kuwaumiza wakulima.
Alisema Serikali kupitia NFRA, ipo katika hatua za mwisho za kuanza kununua mahindi kutoka kwa wakulima, hatua itakayosaidia kuimarisha bei ya soko na kulinda na masilahi ya wazalishaji.
“Niwashauri wakulima kutokimbilia kuuza mazao yote mara baada ya mavuno, bali wauze kiasi kinachokidhi mahitaji ya haraka na kuhifadhi yaliyobaki ili kuuza wakati bei itakapokuwa nzuri zaidi.
“Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara, kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo bora na kushirikiana na wadau wote wa sekta ya kilimo ili kuongeza tija ya uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa Taifa,” amesema Chongolo.
Masikio keshokutwa
Matumaini aliyoyabainisha Chongolo yanawekewa uzito na kauli ya Meneja wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) Kanda ya Makambako, yenye mikoa ya Njombe na Iringa, Revocatus Bisama anayewataja wakulima wa mikoa ya Njombe na Iringa wawe na uvumilivu hadi keshokutwa Julai 20, 2026 litakapotolewa tamko rasmi kuhusu ununuzi na bei ya zao hilo.
Amesema kama alivyoelekeza Waziri Chongolo, NFRA haiwezi kuwa na maelezo mengine, badala yake itakuwa tayari kwa utekelezaji wa maelekezo ya Serikali.
“Waziri alielekeza kwamba Julai 20 atatoa kauli rasmi, tunaendelea na maandalizi ya hapa na pale, sisi NFRA hatutoi bei elekezi, badala yake Serikali ndio yenye mamlaka, kwa hiyo tunasubiri maelekezo ya waziri mwenye dhamana,” amesema Bisama.
Kilio cha wakulima
Kauli za Serikali na NFRA zinatokana na kilio cha wananchi kuhusu nyakati wanazozipitia baada ya bei ya mahindi kushuka wakati zile pembejeo zikiwa juu, hivyo wakaiomba Serikali iingilie kati kuwakwamua katika hali ngumu wanayopitia.
Agnes Mwashiuya, mkulima katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe amesema gharama za uzalishaji wa mahindi ziko juu ukilinganisha na bei iliyopo sokoni na kwamba hakuna bei elekezi inayowabana wanunuzi.
“Gunia tunauza kati ya Sh36,000 hadi Sh38,000, bei ambayo inamkata sana mkulima, ukizingatia gharama tunazotumia kuanzia maandalizi ya shamba hadi mavuno ni kubwa.
“Pia, gharama za pemebejeo ziko juu sana kwani mpaka sasa mfuko wa mbolea ya kupandia tunanunua Sh95,000, mbolea ya kukuzia Sh80,000 na kwa upande wa mbegu kwa sasa tunazipata kwa bei za rejareja mpaka Sh100,000 kwa mfuko,” amesema mkulima huyo.
“Tunachoomba Serikali itutafutie soko la uhakika kwa zao la mahindi angalau debe moja tuuze kuanzia Sh10, 000 kama ilivyokuwa mwaka jana tuweze kunufaika na kilimo chetu,” amesema Agnes.
Kwa upande wake, Joseph Mwampashi, mkulima wilayani Ileje, amesema kutokana na changamoto ya bei ya mahindi, ni muhimu Serikali ikaimarisha upatikanaji wa masoko yenye uhakika, kuongeza ununuzi kupitia taasisi husika ikiwepo NRFA.
“Tunaomba Serikali na NFRA ije na mpango wa kununua zao hili kama ilivyo kwa mazao mengine, ukiwepo ufuta, kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo tutakuwa na bei elekezi,” amesema Mwampashi.
Mwangwi wa vilio cha Songwe ni sawa na vile vya mkoani Rukwa ambako Rafael Mwembezi, mkazi wa Sumbawanga pia amesema wanatumia gharama kubwa kwenye uzalishaji wa mahindi lakini wanayauzwa kwa bei ndogo, jambo linalowaingizia hasara.
“Bei ya chini ya mahindi kwa kilo moja ni Sh635, bei ya juu Sh800, wastani Sh710 kwa kilo, kwa sasa bei ya mahindi kwa gunia mkoani Rukwa ni kati ya Sh40,000 hadi Sh55,000,” amesema Mwembezi.
Mkoani Njombe mambo ni yaleyale, Wema Ngwale kutoka Kijiji cha Chalowe wilayani Wanging'ombe, amesema mwanzoni mwa msimu wa kilimo, alikuwa na matarajio makubwa katika uzalishaji wa zao hilo lakini sasa yameyeyuka.
“Tunauza debe moja la mahindi Sh6,000 sasa, bei hii ni tofauti na gharama za kilimo tulizoinmgia. Hii inaweza kusababisha msimu ujao tusirudi shambani kama bei itaendelea kuwa hivi,” amesema.
Kilio cha Ngwale kinaungwa mkono na Tula Msala kutoka wilayani humo, akiongeza kuwa gharama za kuhifadhi mahindi yasiharibike nayo ni changamoto ambapo ukitumia mifuko ya kinga njaa, kila mmoja ni Sh4, 500 lakini ukitumia dawa gharama ni kati ya Sh4,500 hadi Sh7,000.
“Pamoja na kulazimika kutumia dawa hizo ili mahindi yasiharibike, pia kiafya dawa hizo si nzuri na zaidi ni kwamba kutunza mzigo wa mahindi ndani ni gharama kubwa,” amesema Msala.
Huko Mbeya mambo ni yaleyale, Witness Kamwela amesema msimu uliopita, debe moja liliuzwa kati ya Sh8,000 hadi Sh9,000 shambani, lakini msimu huu bei imeshuka hadi kati ya Sh6,000 na Sh7,000 katika baaadhi ya maeneo.
“Msimu huu kilimo kimetukata sana, tumewekeza fedha na nguvu nyingi kuanzia kulima hadi kuvuna, lakini tuna changamoto ya kukosekana kwa soko la uhakika,” amesema Witnes.
Ni bei ya soko
Wakati wakulima wakieleza mapio yao, Joseph Mwashilindi ambaye ni mnunuzi wa zao hilo, amesema wananunua zao hilo kwa bei ya soko na kuwa licha bei wanayotoa kwao haina athari, zaidi ya kumbana mkulima.
Mwashindi amesema miaka ya nyuma Serikali ilikuwa ikinunua mahindi kupitia NFRA, lakini kwa mwaka huu bado shughuli hiyo haijaanza, hali ambayo inamfanya mkulima aendelee kulalamika.
“Wote tunatafuta riziki, kwa maana hiyo wapo matajiri wananunua kwa ajili ya baadaye, tunaamini bei huenda ikabadilika kwa kuwa uhitaji ni mkubwa, lakini kwa sasa mkulima ndiye anaumia,” amesema Mwashilindi.
Mnunuzi mwingine ni Numenye Mbughi ambaye amesema bei ya zao hilo hairidhishi kwani awali walikuwa wananunua Sh5,000 lakini sasa wananunua Sh6,500 kwa debe moja.
“Kwa sisi wanunuzi bei tunazonunulia kwa wakulima ni rafiki, kwani wakija wafanyabiashara wakubwa tunauza Sh7,000 mpaka Sh7,500 kwa debe moja. Tunaomba Serikali iboreshe na kutafuta masoko ya uhakika,” amesema Mbughi.
Bei hiyo licha ya kuwa kilio kwa wakulima, kwa sehemu ni kicheko kwa wanunuzi kama anavyoeleza Julius Mwanalinze.
“Japokuwa ni hasara kwa mkulima aliyetumia gharama katika uzalishaji, kwa wanunuzi wa mahindi, bei kuwa chini ni furaha kwao. Lakini kwa mkulima aliyenunua pembejeo za kilimo kwa gharama kubwa na kuja kuuza mahindi kwa bei ya chini ni hasara kubwa,” amesema Mwanalinze.