Wafugaji kuku wapewa mbinu

Songwe. Wafugaji wa kuku wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe wameshauriwa kuzingatia ushauri wa wataalamu ili waweze kufuga kwa mafanikio ili kupata tija.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Oktoba 23, 2023 na ofisa mifugo katika Halmashauri ya Wilaya Mbozi, Musa Mstafa wakati akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake kuwa wapo wafugaji ambao wanafanya shughuli hiyo kwa mazoea na kujiamini huku wakifanya vibaya na hivyo kupunguza tija.
Amesema katika ufugaji bora wa kuku ni lazima pia kuzingatia lishe bora kwa kulisha chakula chenye virutubisho vinavyotakiwa ili kumfanya kuku akue vizuri na kwa viwango vinavyotakiwa.
"Chakula cha kuku lazima kizingatie makundi yote matano ya vyakula yanayohitakika mwilini, pia mkulima anapaswa afahamu aina ya kuku alio nao kama ni wa nyama kuna chakula chake na iwapo ni wa mayai hali kadharika chakula chao kinatofautiana na wanyama," amesema Mstafa
Kuhusu magonjwa Mstafa amesema kuku wanaugua magonjwa yanayotibika na yasiyotibika ambayo yanahitaji chanjo ili kuyadhibiti.
"Magonjwa yasiyotibika ni pamoja na ugonjwa wa kideri, magonjwa ya maambukizi ya mafua na ugonjwa wa ndui ambayo ili kuyadhibiti ni lazima mfugaji atoe chanjo kwenye mifugo yake kabla haijaonesha dalili zozote za kuugua," amesema Mstafa.
Ameyataja magonjwa yanayoathiri kuku lakini yanatibika kuwa ni pamoja na homa ya matumbo, na minyoo.
" Nawashauri wafugaji wa kuku kuhakikisha wanawapatia maji safi na salama kuwaepusha na ugonjwa wa homa ya matumbo unaotokana na kunywa maji yasiyo safi na salama na kuwa ugonjwa huu pia unaweza kuhamia kwa binadamu" amesema Mstafa
Akizungumzia ugonjwa wa minyoo amewataka wakulima kutibu mifugo yao ingali michanga na kuendelea hivyo Kila baada ya miezi mitatu.
Akizungumzia hoja ya ukosefu wa chakula amesema wafugaji wanaweza kuandaa chakula wao wenyewe kwa kuzingatia kanuni za uchanganyaji na uwiano sawa, lakini wanapaswa kuwa na mizani lakini pia kuwatumia wataalamu waliopo.
Ofisa huyo wa mifugo alikuwa akijibu hoja zilizotolewa na baadhi ya wafugaji kuku walizozitoa juzi kuwa wanakabiliwa na ukosefu wa chakula Bora, dawa za tiba kwa magonjwa yanayojitokeza.