Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wa utalii wahimizwa kutoa ushauri wa kuboresha sekta hiyo

Muktasari:

  • Wakati wadau wa utalii wakielezea manufaa ya vikao na Serikali, yenyewe imewataka kufunguka ili kuboresha sekta hiyo.

Dodoma. Serikali imewataka wadau wa utalii nchini kufunguka kwa kutoa ushauri wa jinsi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta ya utalii.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Mei 13, 2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana wakati wa mkutano wa nne wa majadiliano kati ya wadau wa utalii na wizara yake.

Mkutano huo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika mkutano wa 13 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Juni 7, 2022 jijini Dodoma.

“Serikali inataka maoni yenu, uboreshaji wa mazingira ya biashara ya utalii kuna masuala ya fedha, sheria hapa leo tunataka watu wafunguke tubadilishane mawazo,” amesema.

Amesema wizara imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza utalii ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Pindi Chana akizungumza katika mkutano wa wadau wa sekta ya utalii, jijini Dodoma.

Dk Pindi amesema kufuatia utekelezaji wa mikakati hiyo, idadi ya watalii imeongezeka na kufikia 5,360,247 ambapo watalii wa ndani ni 3,218,352 na watalii wa nje ni 2,141,895.

“Nitoe rai kwamba tuendelee kushirikiana katika kusimamia na kuendeleza sekta ya utalii kwa maslahi mapana ya Taifa kwani mikutano ya namna hii inatoa fursa ya kuwasilisha mchango utakaowezesha maendeleo ya sekta ya utalii,” amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava ameshauri mikutano ya aina hiyo iwe mingi ili wadau watoe maoni ya kuboresha sekta hiyo.

“Na sisi kama Bunge tutaendelea kujitahidi kukutana na wadau, pia, ili yale ambayo mtakuwa mmeshindana nayo ama walikosa ujasiri wa kutosha wa kuyasema watakuwa na ujasiri wa kuyasema na sisi tutarudisha kwako,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama wa Waongoza Watalii Tanzania (Tato), Elirehema Maturo amesema mikutano hiyo itawezesha kuleta maendeleo na tija kubwa katika sekta ya utalii nchini.

“Tumekuwa na changamoto mbalimbali katika sekta ya utalii ikiwemo tozo mbalimbali zinazotoka katika sekta ya utalii ambazo zinawaletea wadau wetu changamoto,” amesema.

“Leo hii tuko na Waziri wa Maliasili na Utalii na Katibu Mkuu wa wizara kujadili ni namna gani bora tunaweza kwenda mbele bila kuathiri sekta yetu,” amesema.