Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijana wa BBT walioajiriwa na bodi ya korosho wapewa zigo

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack akimkabidhi kishikwambi kwa Ofisa ugani, Juma Ally  kutoka Kata ya Kitumbikwera. Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

  • Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imewataka vijana kutoka BBT kuhakikisha kuwa wanatimiza malengo ya Serikali kwa kuzalisha korosho Tani laki 7 kwa mwaka 2025/2026 hadi Tani Milioni 1 kwa mwaka 2030.

Lindi. Vijana walioajiriwa kwa mkataba na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) wamepewa kibarua cha kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo unaongezeka.

Lengo la Serikali ni kuwa ifikapo 2025/2026 kuzalisha tani 700,000 za korosho zizalishwe nchini na tani 1,000,000 hadi mwaka 2030.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki na vishikwambi kwa vijana hao Machi 16,2025, Mkurugenzi wa CBT, Francis Alfred amesema kuwa bodi ya korosho imeajiri vijana 500 nchi nzima ambapo kwa mkoa wa Lindi wameajiriwa vijana 152 ambao watakwenda kushirikiana na maofisa kilimo wa wilaya katika kuzalisha korosho ilikufikia malengo ya Serikali ya kuzalisha korosho bora .

Alfred ameendelea kusema kuwa vijana walioajiriwa ajira yao itadumu kwa mwaka mmoja ili kuwaangalia kama wataleta matokeo chanya kwa wakulima na Serikali kufikia malengo mahususi.

"Hawa tuliowaajiri ni ajira ya mwaka mmoja ili tuwaangalie kama wataenda na matarajio ya Serikali ya kuzalisha kwa tija ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa,”amesema Alfred

"Lengo ni kuleta mabadiliko na kila mkulima afikiwe na huduma za ugani, maofisa ugani watasaidia kwenda kufufua mashamba pori pamoja na zoezi la kugawa pembejeo za kilimo ,lengo ni kusogeza huduma karibu ili kila mkulima afikiwe na ofisa ugani,”ameongeza Alfred.

Awali akikabidhi vifaa hivyo kwa vijana hao  152, Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Telack amewataka kwenda kuvitumia kwa lengo lililokusudiwa na pia amesema kuwa Serikali imewaamini na inawategemea waende wakafufue mashamba pori na kuweza kuzalisha korosho kwa tija .

"Pikipiki hizi ziende zikafanye kazi iliyokusudiwa na pia niwaombe kwenda kufufua mashamba pori ili kuweza kuzalisha kwa tija,"amesema RC Zainab

Kwa upande wa maofisa ugani walionufaika na mradi wa BBT ambao wamepatiwa ajira chini ya CBT wamesema wako tayari kuhakikisha wanafikia lengo.

Winfrida Mashala, ofisa kilimo Kata ya Jamuhuri, Manispaa ya Lindi amesema watahakikisha wanaenda kuwasaidia wakulima kufikia malengo yao.

"Vishikwambi vitatusaidia kuuisha taarifa za wakulima na kuingiza taarifa zao na hizi pikipiki zitatusaidia katika kuwafikia wakulima na kukuza zaidi zao la korosho na kuhakikisha tunafikia malengo"amesema Mashala