Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukuaji deni la Serikali unavyowachanganya walipakodi

Mengi yanazungumzwa kuhusu mwenendo wa deni la Taifa, kimsingi ni miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wana shauku ya kusikia habari zake kila mara.

Kila taarifa inayotolewa juu ya mwenendo wa deni la Taifa inafuatiliwa na wengi na aghalabu huibua mjadala, haijalishi imetolewa na Serikali au chombo cha habari.

Hii inaonyesha kuwa wananchi wanajua wajibu wao, kwani wao ndio walipaji wa deni hilo kwa njia tofauti, ikiwamo kupitia kodi wanazotozwa.

Hivi karibuni mjadala mkubwa uliibika baada ya taarifa kusambaa kuwa deni la Serikali limefikia Sh98 trilioni, taarifa hiyo ilitoka katika ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) juu ya mwenendo wa uchumi wa kila mwezi.

Katika pitapita zangu mtandaoni, mjadala ulikuwa ni mkubwa zaidi, watu wakilinganisha ukopaji wa kila awamu ya uongozi. Kazi yangi ilikuwa ni kusoma michango ya wasomaji ili nione kama naweza kupata kinachonifaa, nikaambulia mkanganyiko.

Wapo wanaosema kiongozi fulani kakopa zaidi ndani ya muda mfupi, wengine wanasema huyu kakopa kidogo, huyu ametumia hivi na yule uchumi ulikuwa hivi au uko vile na wengine wana hofu juu ya athari za huo mwenendo.

Mlipakodi mie nikasema ngoja nikajionee hilo deni lenyewe kwenye tovuti ya BoT. Nikakuta hadi Julai 2024 deni la nje la Serikali Kuu limefikia Dola za Marekani 24.69 bilioni (Sh67.29 trilioni) na riba ya Dola 252 milioni (Sh686.7 bilioni), huku deni la ndani likifikia Sh32.4 trilioni

Kwa jumla hadi Julai, 2024 Serikali ilikuwa inadaiwa zaidi ya Sh100 trilioni, ikijumlishwa na Sh13 bilioni zinazodaiwa kwa mashirika ya umma (kwa kiwango cha kubadilishia fedha cha Sh2,725 kwa Dola moja).

Ukijumlisha deni la Serikali na lile la sekta binafsi, takwimu za BoT zinaonyesha deni la Taifa hadi mwezi huo lilikuwa Dola za Marekani 41.8 bilioni (Sh114 trilioni). Mie sitagawanya kwa idadi ya Watanzania kujua mgawo wa hilo deni kwa kila mtu kwa kuwa haina maana, japo ni karibu Sh2 milioni kwa kila mtu.

Ukiachilia mbali deni la ndani ambalo linalipwa kwa Shilingi, deni la Taifa nje ya nchi linaundwa na Dola ya Marekani kwa asilimia 66.8, Euro ya Ulaya kwa asilimia 17, Yuan ya China kwa asilimia 6.4 na sarafu nyinginezo kwa asilimia 9.9.

Baada ya kuelewa mwenendo na muundo wa deni hilo, jioni nikaenda kijiweni kwangu ambapo huwa napata kahawa muda mwingi, huku mada mbalimbali za kitaifa na kimataifa na kitaifa zikijadiliwa.

Hapo huwa nakutana na wananchi wa kawaida kabisa, lakini wakati mwingine na wasomi wanakuwepo.

Nilijua lazima deni litajadiliwa hapo na hata lisipojadiliwa baadaye nitachokoza mada hiyo ili nipate mtazamo wa wananchi juu ya mwenendo huo. Nimefika tu nikakuta mambo ya Yanga na ushindi mwembamba ambao mashabiki wake hawakuuzoea.

Ulipotokea tu ukimya, nikauliza ndugu zangu mnazungumziaje mwenendo wa deni la Taifa na la Serikali? Mmoja akadakia, ipo siku nchi yetu itachukuliwa, wengine wakawa wanacheka huku naye akisisitiza: “Kabisa nawaambia, hayo matrilioni ya kulipa tutayapata wapi na wengi wetu hali zetu ni kama hizi!

Mwingine akadakia kuwa yeye anaona kwa deni ilipofikia nchi ingepunguza kukopa au kuacha kukopa ili kuiepusha nchi na mzigo wa madeni na hatari inayoweza kujitokeza.

Akaongeza kuwa kadiri miaka inavyozidi kwenda, ndivyo ukopaji wa nchi unavyozidi kuongezeka, naye akawa analinganisha hali ya deni la Serikali na la Taifa miaka ya nyuma na lililopo sasa.

Muda wote tulikuwa tunamsikiliza mtoa hoja ambaye ni mlipakodi mwenzangu kupitia kodi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Katika mijadala kama hii kila mtu huwa anajivika uzalendo katika hoja zake, hisia nazo zinakuwa mbele. Kila anayezungumza huzungumza kwa uchungu.

Lakini jamaa mmoja pale kijiweni akasema “Jamani mimi ni mchumi, nchi haiwezi kuuzwa, hamna kitu kama hicho na kiuchumi mwenendo wa deni la Tanzania ni mzuri kuliko mataifa mengi.”

Akasema jambo ambalo wengi hawalitizami ni kuwa uchumi wa nchi nao unakua kila mara na kwa sasa pato la Taifa (GDP) limefikia zaidi ya Sh220 trilioni, huku pato la mtu mmoja mmoja likiwa ni karibu Sh3 milioni kwa mwaka.

Mchumi huyo akasema kadiri uchumi wa nchi unavyokua ndivyo nchi inavyozidi kupata wigo wa kukopesheka zaidi kwa kuwa inakuwa na uwezo wa kurejesha mkopo husika.

Zaidi, mwenendo wa deni la Tanzania si wa kupanda tu bali ni kupanda na kushuka kama ilivyoshuhudiwa ndani ya miezi mitatu iliyopita.

Nikakumbuka Juni 16, mwaka huu ripoti ya Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na ufanyaji tathmini kwa nchi kujua uwezo wake wa kukopesheka, Fitch Rating, ilieleza Tanzania bado ina uwezo wa kukopa zaidi na kulipa madeni hayo vizuri.

Ripoti ya Fitch ilitoka ikiwa ni miezi mitatu tangu kampuni ya Moody’s Analytics inayofanya kazi kama yake kutoa ripoti iliyoeleza kwa mwenendo wa uchumi inaona Tanzania inakopesheka na ina uwezo wa kulipa madeni.

Moody’s baada ya kufanya mapitio, ilipandisha daraja la uwezo wa kukopesheka kwa Tanzania kutoka B2 ikiwa na mtazamo chanya (Positive Outlook) hadi B1 ikiwa na mtazamo thabiti (Stable Outlook). Daraja hilo ni la juu kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.

Ukuaji deni la Serikali unavyowachanganya walipakodi

Katika tathmini yake, Fitch inaeleza daraja la ukopaji la Tanzania sasa ni B+ ambalo linaashiria uhimilivu mzuri, ikisema hayo ni matokeo ya kuwa na ukuaji mzuri wa pato la Taifa (GDP), kiwango kidogo cha mfumuko wa bei na deni la Serikali lililopo katika kiwango cha kati.

Fitch inaamini ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa mwaka kufikia asilimia 5.4 kama ambavyo Serikali inatarajia, ukibebwa na ukuaji mzuri wa sekta ya kilimo, madini, utalii, miundombinu na kukamilika kwa miradi mikubwa ya uchukuzi na nishati.

“Tunatarajia uchumi utakua kwa kasi ya asilimia 5.9 katika mwaka unaofuata (2025) kutokana na utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kati ya Uganda hadi Tanzania (EACOP). Na kwa siku zijazo pato linaweza kukua zaidi iwapo mradi wa gesi asilia ya kimiminika (LNG) utatekelezwa,” inaeleza ripoti hiyo.

Kadhalika, ripoti hiyo ya Fitch inaelezea kuwa na mwenendo mzuri wa akiba ya fedha za kigeni hadi kufikia Dola 5.7 bilioni mwaka 2025 kutokana na sera zilizopo, ambazo zinavutia uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji kutoka nje (FDI).

Pamoja na maelezo hayo, huku mtaani walipakodi (wananchi) bado wana wasiwasi na mwenendo wa deni hilo, ingawa kila mara Serikali imekuwa ikisisitiza juu ya uhimilivu wake.

Mjadala ulipokuwa mkali juu ya deni la Serikali msimu wa bajeti hii, nilimsikia Kamishina wa Usimamizi wa Deni la Serikali wa Wizara ya Fedha, Japhet Justin akisema ukubwa wa deni unakua kwa kuongozwa na shabaha za uchumi.

“Kunakuwa na malengo yanayopelekwa bungeni, mfano mwaka ujao tunasema tunataka kukopa kiasi fulani, hivyo bajeti iliyosomwa hivi karibuni inaenda kutengeneza matumizi na mapato tarajiwa kwa mwaka husika wa fedha,” alifafanua.

Alisema ukopaji unasimamiwa na sheria ya mikopo na madeni na taratibu za kukopa zinazofanyika kutokana na msingi ya sheria.

Nikiwa bado niko kijiweni pale, nilipoona mjadala umekuwa wa moto niliwakumbusha walipakodi wenzangu kuwa kukopa hakuepukiki, ikizingatiwa kuwa kuna miradi mingi ya maendeleo inatekelezwa miaka hii, tena yenye thamani kubwa.

Nikakumbusha tena juu ya ruzuku na huduma za kijamii ambazo Serikali inazigharimia, ikiwemo elimu bila malipo, huduma nafuu za afya, maji na ruzuku katika baadhi ya bembejeo za kilimo.

Nikawakumbusha wenzangu kuwa kwa mujibu wa bajeti ya sasa, asilimia 30 itategemea mikopo, misaada ili kutekelezwa.

Nikawaeleza kuwa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025 sehemu kubwa ya Sh49.3 trilioni zilizopangwa kukusanywa na kutumika zitatokana, pamoja na mambo mengine, ni mikopo na misaada.

Katika bajeti hiyo, mapato ya ndani ya Serikali kuu ni Sh33.25 trilioni (mapato ya kodi na yasiyo ya kikodi), mikopo ya kibiashara ndani na nje ya nchi (Sh9.6 trilioni) huku misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ikichangia Sh5.1 trilioni.

Kwa maana hiyo ni kuwa pamoja na kutegemea mifuko ya walipa kodi kwa zaidi ya theluthi mbili (Sh33.25 trilioni), karibu theluthi moja itakayobakia Serikali itategemea kukopa na misaada ili kutekeleza bajeti yake ambayo kwa jumla itakuwa (Sh14.7 trilioni).

Wote wakatikisa vichwa, nikawaambia wacha nimpigie mchumi ninayemwamini, huyu jamaa anafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni profesa kabisa, nikamuuliza, vipi tathimini yako juu ya deni la Taifa, naye akasema kukopa hakuepukiki kwa kuwa vyanzo vya ndani havitoshi.

Simu ilikuwa laudispika (sauti ya juu) muda huo, nikamuuliza tena, sasa tunatokaje hapo? Akajibu kuwa: “Muhimu siyo nani kakopa ngapi kwa muda gani, bali anatumiaje alichokopa. Kama mikopo itatumika kwenye shughuli za kukuza uchumi ni jambo jema, kwani mkopo utajilipa.”

Akasema kisichofaa ni kuwa na matumizi mabaya wa mkopo, kwani yanasababisha ulipaji wake kuwa mgumu, hata hivyo alishauri namna nyingine, kuwa nchi inapaswa ijaribu kutumia kilichoko ndani ya uwezo wake.

Hapa alimaanisha kubana au kupunguza matumizi ile sehemu ya fedha za matumizi ya kawaida zitumike kufadhili miradi ya maendeleo na kupunguza ukopaji.

Mlipakodi mimi nikagundua kuwa matamanio ya walipakodi yanaweza kutimizwa kukiwa na nidhamu na kufuata ushauri wa wachumi.

Matumizi na uwazi unaweza kuwafanya watu wasione deni kama tishio la nchi yao kuuzwa au kuzorota kwa maendeleo.

Alamsiki!