Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yakubali azimio la COP28  kubadili kilimo, mfumo wa chakula

Muktasari:

  • Tanzania miongoni mwa nchi 152 zilizoidhinisha azimio la pamoja kuhusu kilimo endelevu, mifumo stahimilivu ya chakula na inayoendana na mabadiliko ya tabianchi. Wadau wataja mwamko wa kisiasa na mwitikio wa raia kufanisha hayo.

Dar es Salaam. Tanzania imekubaliana na  azimio la pamoja kuhusu kilimo endelevu, mifumo stahimilivu ya chakula na inayoendana na mabadiliko ya tabianchi.

Azimio hilo  linasisitiza uhitaji wa haraka wa kubadili mifumo ili kuwa na uhakika na usalama wa chakula, kutokana na athari zinazoonekana kwenye sekta.

Taarifa iliyowekwa na Wizara  ya Kilimo kwenye mtandao imethibitisha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 152 zilizoidhinisha azimio hilo kwenye mkutano wa pamoja wa viongozi wa sekta uliofanyika Desemba 10, huko Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) siku chache kabla ya kukamilika mkutano huo Desemba 12, 2023.

Katika mkutano huo wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC-COP28), mataifa yalifikia maazimio hayo na kusisitiza mabadiliko ya haraka yenye  lengo la msingi la kuhakikisha ustahimilivu, kuzuia tatizo la upungufu wa chakula, utapiamlo, na changamoto za kiuchumi, huku kukiwa na ustawi wa pamoja unaoendana na mabadiliko ya hali hewa.

Taarifa ya mazimio inaeleza malengo makuu na kuahidi kuweka kipaumbele katika hatua za mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza hatua za kukabiliana na hali hiyo kwa wakulima na wavuvi, kutoa msaada wa kifedha, kiufundi na elimu, na kukuza usalama na uzalishaji endelevu wa chakula.

Mpango huo pia unalenga kuangalia makundi yaliyo katika hatari zaidi hasa wanawake, watoto, vijana, watu wa vijijini, wakulima wadogo, na wenye ulemavu kuhakikisha wanapata msaada wa haraka unaoendana na mahitaji yao kwa kuwalinda na kufanya utafiti.

Usimamizi jumuishi wa maji na miundombinu yake katika kilimo umeangaziwa, ili kuhakikisha uendelevu na kupunguza athari kwa jamii.

Kufikia mwaka 2025, mataifa yamekubaliana kushiriki kikamilifu, kuunganisha kilimo katika mikakati muhimu ya nchi na hivyo kuhakikisha sera zinaendana na uhalisia, jambo litakalosaidia katika kuongeza mapato, kupunguza uzalishaji wa hewa joto na kuimarisha uthabiti, kwa kuzingatia lishe, ufanisi wa matumizi ya maji na mfumo wa ikolojia.

Vyanzo mbalimbali vya fedha, ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi, vitafadhili kukabiliana mnyororo wa thamani wa sekta.

Tamko hilo linahitimishwa kwa nchi kufuata mfumo wa haki wa biashara, wenye uwazi na ushirikishwaji..

Mtazamo wa wadau

Mdau wa kilimo, Audax Rukonge, amesema mafanikio ya maazimio hayo yanategemea mambo mawili,  ambayo ni mwitikio wa kisiasa na msukumo wa wananchi.

Amesema kwa sababu utekelezaji, usimamizi na maamuzi yanategemea kwa kiwango kikubwa mwamko wa kisiasa na linapokosekana hili,  ndio raia wanaweza kuisukuma Serikali kutekeleza malengo haya.

“Nchi ina mikakati mizuri ya kilimo na mifumo ya chakula na tumeona mwitikio wa kisiasa kama ongezeko la bajeti kwenye miaka ya karibuni, tafiti za mazao na mbegu, ruzuku kwenye kilimo, na hata   Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imeshusha riba na benki za biashara zikifuata hilo,” amesema.

Audux ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa huru la Kilimo (Ansaf) amehoji: “Sasa sijui ni kwa kiwango gani kuna utekelezaji? lakini je inafika kwa wakati? kwa sababu suala la mabadiliko ya tabianchi ni suala la muda”.

Akizungumzia muunganiko wa wizara amesema suala la kilimo na mifumo ya chakula sio la wizara ya kilimo pekee.

“Kukiwa na muunganiko mzuri kunasaidia kuvutia uwekezaji na sekta binafsi … ndio maana nasisitiza suala la utaratibu ni muhimu sana.. lakini pia ushirikishwaji wa wadau kama vyombo vya habari unahitajika kwenye suala zima la kutoa elimu” ameongeza kusema.

Rukonge alishauri ushirikishwaji hasa makundi yanayoathrika zaidi kama wakulima wa kawaida, watoto na wanawake na maeneo yanayoathrika zaidi yasiachwe nyuma ila yatafutiwe suluhisho.

Mkurugenzi wa kampuni ya kilimo ya Altitude X, Rose Funja amependekeza nchi itumie utaratibu wa  kuunganisha dhana ya miundombinu ya umma ya kidijitali (DPI) katika mipango ya kufikia kilimo himilivu na mifumo ya chakula, ambayo anaamini inaweza kuongeza ufanisi zaidi.

"DPI inahusisha kutumia teknolojia ya kidijitali kutoa huduma za kimsingi na data zinazoweza kufikiwa na umma, wafanyabiashara na taasisi za Serikali. Mfumo huu unatoa taarifa za hali ya hewa na teknolojia hitajika za kilimo na huduma za ugani” amesema Rose.

Amependekeza pia Serikali kuendelea kujumuisha wadau kwa kutoa ruzuku, kupitia mifumo ya kodi na kipaumbele cha kufikia rasilimali za nchi kwa wanaofuata sheria na washiriki na kuboresha mifumo ya utoaji elimu kwa wadau na wakulima.

Naye, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao wa Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu, ameeleza mambo matano, akisema kuwa wizara inajua umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kilimo na chakula na kutaja mambo hayo ni utafiti, umwagiliaji, uhifadhi wa maji, kukabiliana na wadudu na magonjwa, na mifumo ya utoaji taarifa.

“Wizara imejikita katika tafiti za mbegu zinazostahimili hali ya hewa, mifano ni alizeti, mbegu za ‘Record’ na mahindi ‘T105’ ambazo zimethibitika kufanya kazi,’’ amesema na kubainisha kuwa katika bajeti ya sasa Serikali imetenga Sh80 bilioni kwa ajili ya tafiti za kilimo.

Vilevile Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa kutokana na uchache wa mvua katika miaka ya hivi karibuni, Serikali inatoa elimu kwa wakulima jinsi wanavyoweza kuhifadhi maji katika msimu wa mvua, kukarabati na kujenga miundombinu ya umwagiliaji.

Kukabiliana na wadudu na magonjwa, ameitaja Mamlaka ya Afya na Viuatilifu vya Mimea Tanzania (TPHPA), kuwa ina uwezo wa kutoa taarifa na utabiri unaohusu wadudu na magonjwa ya kuudhi.


Habari hii imewezeshwa na MESHA pamoja Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini