Kanuni mpya kulinda wachimbaji wadogo, kibano wageni ‘janja janja’

Dodoma. Baada ya malalamiko ya muda mrefu, Serikali kupitia Wizara ya Madini imetunga kanuni za msaada wa kiufundi katika leseni ndogo za uchimbaji wa madini, ambapo zitaratibu ushiriki wa wageni katika leseni ndogo za uchimbaji wa madini (PML).
Kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha Sheria ya Madini sura ya 123, kimezitamka PML kuwa ni maalumu kwa ajili ya Watanzania, lakini kutokana na kutokuwa na udhibiti wa kikanuni wageni wamekuwa wakitumia mwanya huyo kufanya shughuli zinazotakiwa kufanywa na wazawa.

Hata hivyo kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini kinatoa ruhusa kwa mmiliki wa leseni ndogo ya uchimbaji madini kuingia ubia na mgeni kwa makubaliano ya msaada wa kiufundi, lakini usimamizi wake ulikuwa mgumu hivyo wazawa kutonufaika ipasavyo.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2024/25 Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema Serikali inatarajia kutunga kanuni za kuratibu ushiriki wa wageni katika leseni ndogo, kwa kuwa kumejitokea wimbi kubwa la wageni kuingia katika maeneo ya wachimbaji wadogo kwa mgongo wa msaada wa kiufundi.
Alisema wingi huo wa wageni haukuwa na utaratibu mzuri na hivyo kusababisha wachimbaji wengi wadogo kutopata manufaa yaliyokusudiwa ya kujiimarisha na wakati mwingine katika vikundi vya wachimbaji, viongozi wachache kuingia makubaliano ya msaada wa kiufundi bila kushirikisha wahusika wote na hivyo kuzua migogoro isiyo na sababu.
Kanuni hizo zimetolewa katika gazeti la Serikali la Aprili 25, 2025, tangazo la Serikali kuitambulisha kanuni hiyo mpya ili kuanza utekelezaji wake ikiwa ni ahadi iliyotolewa na Waziri Mavunde akitekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa mambo muhimu yaliyotajwa katika kanuni hizo ni usajili wa mikataba ya kiufundi kwenye Tume ya Madini baina ya mchimbaji mdogo na mtoa msaada wa kiufundi, huku zikifafanua maana ya maneno msaada wa kiufundi ili kutimiza lengo mahsusi la kuongeza tija ya uzalishaji na kukuza ujuzi.

Pia kanuni hizo zimeeleza mgawanyo wa mapato kati ya mwenye leseni ndogo na mtoa msaada wa kiufundi kwa madini yatakayozalishwa, huku lugha ya mikataba hiyo itakuwa ya Kiswahili au Kiingereza.