Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh800 milioni kuwezesha vijana kiuchumi

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa (kushoto) na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Mark Bryan Schreiner (kushoto) wakisaini mkataba wa ushirikiano ili kuwawezesha vijana katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Kigoma. Picha na Mpi

Muktasari:

  • Vijana wa kuanzia umri wa miaka 18 hadi 24 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Kigoma, waliopo shuleni na walioacha masomo kwa sababu mbalimbali watawezeshwa kiuchumi.

Dar es Salaam. Vijana wa kuanzia umri wa miaka 18 hadi 24 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Kigoma, waliopo shuleni na walioacha masomo kwa sababu mbalimbali watawezeshwa kiuchumi.

Mpango huo unaolenga kuongeza ujumuishi wa wananchi kiuchumi hasa makundi maalumu, umeanzishwa na Taasisi ya CRDB Bank Foundation baada ya kusaini mkataba wenye thamani ya Sh800 milioni kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA).

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa amesema kufanana malengo kwa taasisi hizo katika kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi ni sababu ya kufikia uamuzi huo.

“Tumeelekeza nguvu kubwa katika kuanzisha programu za kuwezesha vijana na wanawake kujumuishwa kwenye mfumo rasmi wa huduma za fedha, kuwapa mafunzo na mitaji wezeshi kupitia programu yetu ya Imbeju. Ushirikiano huu unakwenda kuimarisha jitihada hizi na kufikia vijana wengi,” amesema Tully.

Amefafanua kuwa  ushirikiano huo unawalenga vijana walio masomoni na wale walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali, walemavu pamoja na mabinti waliopata ujauzito wakiwa shuleni.

Katika utekelezaji wake, amesema wanakusudia kupunguza changamoto za upatikanaji wa ajira, kuwapa elimu ya fedha, ya afya ili kupunguza mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU). 

“Ushirikiano wetu upo maeneo mawili, kwanza kutoa elimu na maarifa ya kujitambua kwa vijana walio shule na walioa nje ya shule itakayojumuisha mafunzo juu ya huduma rafiki za afya, unyanyasaji wa kijinsia, jinsi ya kuepuka na namna ya kuishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.”

“Eneo la pili ni kutoa elimu ya fedha, ujasiriamali kwa vijana na mabinti ili kuwajengea mazingira ya kutekeleza majukumu yao kikamilifu,” amefafanua Tully.

Kwa upande wake mwakilishi mkazi wa UNFPA nchini, Mark   Schreiner amesema shirika hilo limekuwa likitekeleza miradi tofauti inayolenga kuwainua wananchi hasa wa makundi yaliyosahaulika katika jamii ili kuwa na uchumi jumuishi.

“Tukiangalia changamoto zinazowakabili vijana nchini ikiwamo upatikanaji wa mitaji, ukosefu wa ajira na elimu ya ujasiriamali. Tuna kila sababu ya kushirikiana na wabia wa kimkakati kusaidia kuwawezesha vijana nchini kushiriki kujenga uchumi wa taifa lao,” amesema Schreiner.

Katika maelezo yake Schreiner amesema taasisi hiyo inatekeleza programu yake ya tisa nchini inayohamasisha uzazi salama kwa kuitambua na kuikubali kila mimba inayopatikana, pamoja na kumwezesha kila kijana kutimiza ndoto za maisha yake. 

“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma hivyo tunashirikiana na wadau wenye mtazamo kama wetu kama ilivyo Taasisi ya CRDB Bank Foundation,” amesema Schreiner.