Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sarakasi za dabi zinavyotoboa mifuko ya watu

Katika historia ya michezo nchini Tanzania, hakuna tukio linalovuta hisia za watu kama pambano la watani wa jadi Yanga dhidi ya Simba. Hii ni zaidi ya mechi; ni tamasha la kijamii, kiuchumi, na kiutamaduni.

Hivyo basi, mchezo wa Ligi Kuu ya NBC wenye namba 184 ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki na wadau mbalimbali, umegeuka kuwa chanzo cha hasara kubwa ya kiuchumi kutokana na kutochezwa kwake kwa muda mrefu licha ya kuendelea kutangazwa na kutarajiwa mara kwa mara.

Sarakasi hizi sasa si tu zimevuruga ratiba ya ligi, bali zimewatoa jasho wafanyabiashara, mashabiki, wadhamini, wamiliki wa haki za matangazo, na hata kuiweka kwenye hatari taswira ya Tanzania katika kusimamia soka kisasa.

Kwa hali ilivyo sasa kuna wasiwasi wa hasara zaidi kwa wenye haki za matangazo na watazamaji. Mathalani Azam TV, yenye haki za kipekee za kuonyesha Ligi Kuu ya Tanzania, imekuwa ikitumia muda na rasilimali kutangaza mchezo wa namba 184. Kila tangazo lina gharama iwe ni muda wa hewani, nguvu kazi ya uhariri, au usafiri wa vifaa vya kurusha matangazo.

Vilevile TBC Taifa ndiyo yenye haki ya matangazo ya redio ambayo pia imewapatia washirika kadhaa kwa makubaliano waliyonayo, kuahirishwa kwa mechi hii nao watahesabu hasara nyingine.

Mathalani, baada ya kuahirishwa kwa mechi ya kwanza (ya Machi 08, 2025) Azam Media Limited (AML) ilitoa taarifa ikieleza kusikitishwa na tukio hilo wakisema limeleta athari kubwa kwa mashabiki wa soka, wateja wetu na wadau wa mpira wa miguu kwa ujumla.

“Kuahirishwa kwa mchezo huu kumesababisha hasara kubwa kwetu kutokana na gharama za maandalizi, matangazo ya kuhamasisha mechi kwa vyombo mbalimbali vya habari, usumbufu kwa kampuni zinazotangaza bidhaa na huduma kwetu na wateja wanaolipa kuangalia mpira kwenye visimbuzi vyetu,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano kwa Umma ya AML ilieleza kuwa tayari timu yetu ya matangazo yakiwemo magari ya kurushia matangazo, kamera, mitambo mingine ya kurushia matangazo na timu nzima ya uzalishaji ilikuwa ipo Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya mechi hiyo.

Mpaka sasa Azam inaendelea kutangaza juu ya mchezo huo ambao bado haujathibitishwa na mamlaka kuwa umeahirishwa lakini kuna uwezeako mkubwa yaliyotokea Machi 08, 2025 yakajirudia tena.

Mbali na Azam kama ilivyo kuwa kwa mchezo uliopita kwa baadhi ya vituo kutuma waandishi uwanjani, wengine walikodisha magari, vifaa vya kiufundi na hata kulipa posho za wafanyakazi yote haya yakiwa na matumaini ya kupata pato kupitia udhamini wa kipindi cha mechi.

Kwa mchezo kutochezwa kwa mara nyingine huku umma ukiendelea kuamishwa kuwa upo ni gharama kubwa bila mapato jambo linalowavunja moyo kwa wawekezaji katika habari za michezo.


Watazamaji

Kwakuwa mchezo unaendelea kutangazwa na umesisitizwa kuwa utachezwa kama ilivyopangwa maelfu ya Watanzania wamelipia vifurushi vya Azam kwa matarajio ya kushuhudia mechi hii ya kihistoria.

“Nimelipia na ninchojua dabi ipo watazungumza hapa katikati watamalizana tu ndiyo maana hata mchezo unaendelea kutangazwa. Nausubiri kwa hamu maana ndiyo mechi kubwa ya msimu iliyobakia,” alisema Obadia Njoni shabiki wa soko na mtumiaji wa Azam Tv.

Pengine kuna waliojichanga ili kupata pesa ya kulipia king’amuzi hicho kuhakikisha hawakosi mchezo huo. Kutokana na mchezo kutochezwa, pesa hizi zimeishia kuwa "bili za hewa", huku wateja wakihisi kudhulumiwa.

Hilo lilitokea kwa waliolipia kuona mchezo huo Machi 08, 2025 na sasa huweza wakapigwa kichwani tena jambo ambalo linaweza kupoteza imani na huduma ya kulipia kwa vile matarajio yao yamegeuka kuwa shubili.


Nafasi ya Kujitangaza kwa wadhamini yeyuka

Sehemu kubwa ya vyanzo vya mapato ya mchezo wa soko ni udhamini kutoka kwa kampuni na taasisi mbalimbali zenye lengo la kujitangaza, hawa hutoa fedha nyingi kulingana na ukubwa wa ligi ambao ni matokeo ya ukubwa wa timu na ushindani uliopo.

Bila shaka hata kampuni zinazodhamini Ligi Kuu ya NBC zinalenga mechi kubwa kama Yanga dhidi ya Simba kwa ajili ya kuonyesha bidhaa na huduma zao kwa mapana zaidi ili kuwafikia watu wengi.

Kampuni kama SportPesa, Azam, na NBC zinakuwa na fursa ya kuvuta wateja kupitia matangazo ya moja kwa moja na mabango ya uwanjani. Kukosekana kwa mechi hiyo kunapunguza fursa ya kufikia hadhira kubwa ya kimataifa, hasa kutokana na kuongezeka kwa ufuatiliaji wa ligi hii kupitia mitandao ya kijamii.

Hii ni pigo si tu kwa wadhamini bali pia kwa ligi nzima inayotegemea kuvutia wawekezaji zaidi kupitia michezo ya kuvutia kama huu. Wanaweza wasiseme ila bika shaka hawafurahishwi na hili linaloendelea.


Watoa huduma

Uwanja wa Benjamin Mkapa ni kama soko kubwa linalochangamka kila panapokuwa na mechi ya watani wa jadi. Wauzaji wa vinywaji baridi, vyakula na nguo zenye rangi za timu, pamoja na madereva wa boda boda, daladala, na taxi wote hujiandaa kwa wingi wa wateja. Kukosekana kwa mchezo huo ni pigo kubwa kwao.

Kwa kawaida, katika mechi ya Yanga na Simba, biashara hufikia kilele ambapo baadhi ya wauzaji hupata mapato ya siku tano hadi saba kwa siku moja tu. Kila mechi inapoahirishwa kunavuruga mzunguko wa kipato na kuongeza ukosefu wa uhakika wa maisha kwa wajasiriamali.

Mbali na huduma za uwanjani mashabiki kutoka mikoa mbalimbali kama Mwanza, Mbeya, Arusha, Tanga na Iringa hukodisha magari aina ya Coaster, basi na kulipia ndege ili kushuhudia pambano hilo jijini Dar es Salaam.

Kwa baadhi yao, tiketi za basi na malazi jijini huwa tayari zimeshalipiwa siku kadhaa kabla. Kuahirishwa kwa mchezo huo dakika za mwisho kunawaletea hasara si tu kifedha bali kisaikolojia, hasa ikizingatiwa kuwa kwa wengine wanakuwa wamepania kushuhudia pambano hilo.


Athari pana zaidi

Sekta ya michezo ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa. Inatoa ajira kwa maelfu ya vijana, inalipa kodi serikalini, na kuimarisha mzunguko wa fedha kupitia uuzaji wa tiketi, bidhaa, na huduma mbalimbali.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikisifika kwa hatua kubwa katika maendeleo ya soka kutoka uboreshaji wa miundombinu, ushiriki wa klabu kwenye michuano ya kimataifa hadi kupanda kwa viwango vya FIFA.

Hata hivyo, sarakasi za mchezo huu zinatishia mafanikio haya. Wadhamini wa kimataifa, wawekezaji, na hata mashirikisho ya soka huangalia namna nchi inavyosimamia mashindano yake ya ndani. Kukosa uwezo wa kusimamia mechi kubwa kama Yanga dhidi ya Simba kunaipa Tanzania alama ya udhaifu wa kitaasisi katika michezo.