Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu za uchache wa walipakodi na namna ya kuongeza makusanyo

Miongoni mwa takwimu ambazo siyo mpya lakini zimeshitua wengi hivi karibuni ni idadi ya walipakodi nchini Tanzania ambayo inatajwa kuwa ni watu milioni mbili.

Ni taarifa iliyowashitua wananchi, walipakodi wenyewe lakini hata Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alisema inashangaza na inapaswa kubadilika kwa kuwa uchumi wa nchi unakua na hata idadi ya watu inaongezeka.

Oktoba 4, 2024 wakati wa uzinduzi wa Tume ya Rais ya maboresho ya kodi ambayo itafanya kazi ya kutathimini mfumo wa kodi nchini, Rais Samia alisema kila anayestahili kulipa kodi nchini anapaswa kufanya hivyo, kwani sasa walipa kodi ni wachache na makusanyo hayaendani na viashiria vingine vya ukuaji wa nchi.

“Ni watu kama milioni mbili kati ya 65 milioni wanaolipa kodi, ukitoa watoto na wengine ambao hawapaswi kukatwa kodi hatupungui milioni 37... ina maana watu kidogo wanalipa kuwajenga watu wengi, hatuwezi kufika. Lazima wote tuchangie kwa kila mtu na kiasi chake,” alisema Rais Samia katika hafla hiyo.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kiuchumi barani Afrika na mahitaji ya huduma za kijamii na miundombinu nayo yanaongezeka na Serikali ili iweze kutimiza hayo lazima ukusanyaji wa mapato uongezeke.

Alitolea mfano wigo wa vyanzo vya ndani ya kodi na visivyo vya kodi, akisema upo chini ya lengo lililowekwa la kufikia asilimia 14.4 ya pato la taifa ifikapo mwaka 2026 na hapo ndipo nchi itaweza kufadhili yenyewe miradi yake ya maendeleo.

Kwa mujibu wa takwimu za TRA, kwa mwaka 2022/2023 mapato ya kodi yalifikia asilimia 12, hivyo kuna upungufu wa asilimia 2.4 na wakati huohuo licha ya ongezeko la makusanyo ya kodi, pato la Taifa nalo linaongezeka.

“Kodi za ndani ni chanzo cha mapato ya Serikali cha kuaminika, hivyo tumeunda Tume hii ili kutathimini, kuchambua na kutoa mapendekezo ya kuimarisha mfumo wetu wa kodi ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii,” alisema Rais Samia.

Wigo finyu wa walipakodi unatajwa kuchangiwa na watu wengi kufanya kazi katika sekta ambazo haziwawezeshi kulipa kodi ya moja kwa moja na kuweka ugumu kwa mamlaka husika katika kuwafikia

Profesa Aurelia Kamuzora wa Chuo Kikuu Mzumbe alitolea mfano wa kilimo kilichoajiri asilimia 68 ya Watanzania, lakini mchango wake katika uchumi bado ni finyu kutokana na wakulima wengi kuendeleza kilimo cha kizamani ambacho kinafanya shughuli nyingi za mnyororo wa thamani kutochangia kodi.

“Wengi wanatumia teknolojia za zamani, ili kuwapata hawa ni lazima kuwahamasisha wawe na kampuni au viwanda vidogovidogo vinavyoongeza thamani ya bidhaa ili watumie wanachozalisha kama malighafi, huko ndiyo tunaweza kupata kodi kutoka kwao,” anasema Kamuzora.

Pia Profesa Kamuzora anasema kukosekana kwa ajira nayo ni sababu nyingine ambayo inafanya kutokuwapo kwa walipa kodi wa moja kwa moja.

“Kitu kingine kinachofanya wigo kuwa mdogo ni kodi zinazotozwa, kama zinawaumiza watu wataendelea kuona ni bora wakae nje ya mfumo rasmi wa kikodi. Kinachoweza kufanyika ni kuwahamasisha kwa kuwalipisha kodi kidogo ili walipe kwa wingi na hii itatusaidia kupata kodi nyingi.”


Kupanua wigo wa walipa kodi

Februari mwaka huu, Mkurugenzi wa TPSF, Raphael Maganga aliishauri Serikali kupanua wigo wa walipakodi, akisema licha ya watu wengi kuwa na uwezo wa kulipa kodi, bado asilimia 80 ya mapato ya ndani ya kodi hukusanywa kutoka kwa walipa kodi wakubwa 400, huku sehemu kubwa iliyobaki ya walipa kodi wakichangia asilimia 20 pekee.

Alitoa kauli hiyo katika uzinduzi wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 lililokuwa limelenga kujadili Maboresho ya Sera katika Uwekezaji, Ukusanyaji wa Mapato ya ndani na Ukuaji wa Uchumi Jumuishi.

Maganga alisema moja ya changamoto inayoukumba mfumo wa kodi ni sehemu za makusanyo kuwa chache na mara nyingi ndio hizohizo zinatolewa macho kuongeza kodi.

“Mfano asilimia 80 ya mapato ya ndani ya kodi hukusanywa kutoka kwa walipa kodi 400 wakubwa. Sehemu kubwa iliyobaki ya walipa kodi huchangia asilimia 20 tu,” alisema.

Alisema watu wengi walio katika nafasi ya kuchangia kodi kwa kiasi kikubwa ni kundi lisilo rasmi, hivyo ni vyema kuhakikisha kwenye sekta rasmi kunavutia kuliko kubaki kwenye sekta isiyo rasmi.

“Tuangalie jinsi ya kuwapunguzia mahitaji ya wao kuwa rasmi, tuwapunguzie na kodi ili waingie kwenye mfumo rasmi," alisema Maganga.

Alisema mwaka 2023/2024 Serikali imelenga kukusanya Sh44.39 trilioni kama bajeti ya mwaka, hivyo ni muhimu kuweka mifumo thabiti ya ukusanyaji kodi ili kukidhi mahitaji hayo.

“Maana, hatuwezi kuwakamua ng’ombe walewale kila mwaka,” alisema Maganga.


TRA nako vipi

Katika kutanua wigo wa kodi, Kamishna wa TRA, Yusuph Mwenda amesema wamejipanga kuimarisha vitengo vya ukaguzi na uchunguzi ili wachache wanaokwepa kodi hatua za kisheria juu yao zichukuliwe.

Alisema wanafahamu uwepo wa watu wanaofanya biashara kwa njia ya mtandao na wengine nyumbani ambao baadhi wamekuwa wakiagiza mzigo na kuuzia ndani.

“Niwaombe wawe wazalendo na tutawafuatilia, waje wajisajili, wawe walipakodi, wapo ambao hawana hata namba ya mlipakodi (TIN) na wanafanya hizo biashara. TIN hatuuzi, tunatoa bure, waombe na waanze kulipa kodi watakadiriwa kiasi kidogo,” alisema Mwenda.

Akitolea mfano kwa watu ambao mauzo yao ya mwaka hayazidi Sh11 milioni, alisema makadirio yao ya kodi ni Sh250,000 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kidogo, huku akisema kufanya hivi kunaweza kufanya nchi kuwa na uwezo wa kukusanya Sh4 trilioni kwa mwezi.


Kuongeza walipakodi

Profesa wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo alisema ili kuongeza idadi ya walipakodi na makusanyo, Serikali inapaswa kurasimisha sekta isiyo rasmi ambayo hailipi kodi, licha ya kuwa na uwezo wa kuzalisha.

Hilo litawezekana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ili waone kuwa kulipa kodi ni wito na una faida ndani yake.

“Lakini watozwe kidogo, ukianza na asilimia 10 hadi 20 watakimbia sekta rasmi, wanatakiwa kukaribishwa kwa kulipishwa kidogo kwanza ujue wako wapi na ukitaka kujua walipo usitake walipe mamilioni,” alisema Profesa Kinyondo.

Alisema hatua ya kwanza katika hilo ni kumuingiza kwenye wigo kwa sababu kadiri wanavyokuwa wengi hata wakitozwa asilimia 5 kuna uwezekano wa kupata fedha nyingi kuliko kuwa na watu wachache wanaotozwa asilimia kubwa.

“Hivyo katika hili Serikali inatakiwa kuwa makini, kama lengo ni kupanua wigo, tufikirie ikiwa na watu wengi tunawezaje kutoza kidogo na kupata hela nyingi kuliko kikubwa na kubaki na watu wachache na TRA ijue kuwa lengo iwe kuwa na walipakodi wengi ili kukusanya zaidi,” alisema.

Maneno yake yanaungwa mkono na Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude ambaye anaeleza kuwa kuna sekta ambazo zinapaswa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria lakini hazifikiwi kikamilifu, hivyo kutochangia mapato ya nchi.

Alisema zipo sehemu ambazo kama nchi kodi inaweza kukusanywa ikiwa kuna maboresho yatafanyika katika baadhi ya sheria, jambo ambalo litasisimua ulipaji kodi kwa kufanya shughuli nyingi za uchumi zifanikiwe na kuchochea ulipaji kodi kwa wingi.

Shughuli hizo huweza kufanya watu kupata ajira, jambo ambalo litawafanya kuwa walipa kodi wa moja kwa moja kupitia makato kupitia mishahara yao.

Hadi sasa takwimu zinaonyesha kuwa walipakodi nchini hawafiki milioni 3, idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na watu walio katika umri wa kufanya kazi. Jambi hili limekuwa likisababisha wafanyabiashara kupaza sauti kila siku ili kuweka mazingira sawa ya biashara.


Matumizi sahihi ya kodi

Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanashauri serikali kuangalia matumizi inayoyafanya kupitia kodi inazokusanya, kuziba matundu ya upotevu wa fedha kupitia utekelezaji miradi isiyokuwa na tija kabla ya kuanza kufikiri kupanua wigo wa walipa kodi.

Wanasema bila kufanya hayo, matokeo tarajiwa pindi wigo wa kodi utakapotanuliwa hayataweza kuonekana kwa sababu kiasi cha fedha kitakachokuwa kimeongezeka kitaendelea kupotea kupitia maeneo hayo.

Profesa Kinyondo alisema kabla ya kutanua wigo wa kodi ni vyema kuhakikisha makusanyo kiduchu yanayopatikana yanaingia katika mfuko ambao haujatoboka.

“Tutoke katika kuangalia mapato na kuangalia namna ya matumizi yanayofanyika, kupanua wigo wakati kuna matundu kwenye mkoba haitaongeza chochote, lazima kuhakikisha kinachokusanywa kinafanya kile kinachokusudiwa, tukifunga nati kuwa hatuibiwi ndiyo tunaweza kutanua wigo,” alisema Profesa Kinyondo.

Kwa upande wake Mkude yeye anasema ni vyema kuwepo na uwazi juu ya namna mapato ya kodi yanavyotumika ili waone faida yake na kuhisi fahari wanapolipa kodi.

“Serikali iwe na uwazi na matumizi wanayofanya yasiende kinyume na matarajio ya watu, huwezi kuwa unataka kuendesha V8 wakati watu wako hawana maji, barabara, umeme shida, mtu anaona hana haja ya kulipa kodi kwa sababu haimnufaishi,” alisema Mkude.

Jambo hilo lingefanya waone ulipaji wa kodi ni wajibu ili kuboresha huduma zilizopo na kuona kuwa hawalipi fedha ili mtu akafanye matumizi ya anasa, akanunue shangingi na badala yake wapate shule nzuri na huduma za muhimu.

“Uwazi juu ya namna fedha zinavyotumika ni kitu muhimu sana, usiri katika matumizi ya kodi haufai, matumizi ya kodi katika anasa, miradi isiyokuwa na maana, CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) aseme fedha zimepotea inafanya watu waone kulipa kodi hakuna maana,” alisema.


Matumaini ya tume

Katika hafla ya kuzindua Tume ya Rais ya Kodi, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka alisema uundaji wa tume hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wakati wa mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la biashara lililofanyika.

Alisema majukumu yake yatakuwa ni kufanya tathimini ya kina ya muundo wa kodi nchini ili kuondoa kero za walipakodi, kuongeza wigo wa walipakodi na kuongeza uwiano wa kodi na pato la Taifa (GDP).

Wajumbe tisa wanaounda tume hiyo ni Balozi Ombeni Sefue (Mwenyekiti), Profesa Florens Luoga, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Mussa Juma Assad ambaye alikuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Leonard Mususa aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa PricewaterhouseCoopers (PwC) Tanzania na Aboubakar Mohamed Aboubakar Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU).

Wengine ni Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, Mshauri wa Masuala ya Sheria. Kijamii Wengine ni David Tarimo, Mtaalamu na Mshauri wa Masuala ya Kodi na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ushauri wa Kodi, PwC, Balozi Maimuna Kibenga Tarishi, Katibu Mkuu Mstaafu na Rished Bade, Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).