Ndege ya mizigo ya ATCL kufanya safari ya pili leo

Muktasari:
- Ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) itakuwa inafanya safari zake kila Jumatatu na Ijumaa kwenda Dubai.
Dar es Salaam. Ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) leo Jumatatu, Julai 10, 2023 inatarajia kufanya safari yake ya pili ya kupeleka mzigo Dubai huku ikiendelea kuvutia kasi masoko mengine muhimu.
Julai 7, 2023 ndege hiyo aina ya Boeing 767-300F ilifanya safari yake ya kwanza kwenda Dubai ikitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julias Nyerere (JNIA).
Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni hiyo, Patrick Ndekena alisema ratiba ya safari za Dubai itakuwa mara mbili kwa wiki (Ijumaa na Jumatatu).
Alisema adhma ya ATCL ni kuhakikisha bidhaa za wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi zinafika kwa wakati na zikiwa na ubora wake kwenye nchi mbalimbali kwa kadri ya inavyotakiwa.
“Leo tunafuraha kubwa kwa kuanza rasmi safari zetu za ratiba kwa ndege yetu hii mpya ya mizigo Boeing 767-300F yenye uwezo wa kusafiri masafa marefu na uzito mkubwa yaani tani 54 kwa mara moja,” alisema Ndekena wakati ndege hiyo ikipakia mzigo kwa mara ya kwanza.
Akifafanua kuhusu uwezo wa ndege hiyo alisema nitoleo la kisasa, ina uwezo wa kwenda mwendo wa kilometa 850 kwa saa na kukaa angani kwa zaidi ya masaa 10 bila kutua.
Kwa upande wake, wakala wa usafirishaji mizigo, George Magoti alisema uwepo wa ndege hiyo ni mkombozi kwa wafanyabiashara nchini kwani itawasaidia kupunguza gharama za usafirishaji.
Magoti alisema kutokana na ukubwa wa mizigo hii, isingewezekana kusafirishwa kwa ndege ya abiria hivyo wangelazimika kukodi ndege ya mizigo kutoka nje ya Tanzania ili kuweza kupakia mizigo mikubwa ya aina hiyo.
“Tunashukuru ATCL kukubali kufanyabiashara nasi ya mizigo la sivyo tungelazimika kutafuta ndege kutoka nchi zingine ambapo ingeongeza gharama, kuchelewesha muda kusubiri ndege ifike na usumbufu wa vibali vya hiyo ndege ya nje,” alisema Magoti.
Alisema mzigo uliosafirishwa na ndege hiyo Ijumaa utapelekwa hadi Dubai na kutoka hapo utasafirishwa kwenda Marekani kwa urahisi na uharaka kuliko wangetumia usafiri mwingine.
Aidha wakiwa katika maonyesho ya sabasaba yanayoendelea Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema wanakamilisha hatua za mwisho ili kuanza safari za kupeleka mizigo Mumbai nchini India.
“Tutaanza na Mumbai na maendeo mengine Afrika ikiwemo Lubumbashi (DRC), Lusaka (Zambia) Harare (Zimbabwe), Nairobi (Kenya), na Entebe (Uganda)”
“Vilevile tunakamilisha mchakato wa kuelekea Kinshasa na kuanza safari za Lagos nchini Nigeria,” alisema Matindi na kuongeza kuwa safari nyingine zaidi ikiwemo ya China zitazingatia mahitaji.