Ndege iliyokuwa ikishikiliwa Uholanzi yarejea nchini

Arusha. Serikali imesema ndege aina ya Airbus A220 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) iliyokuwa ikishikiliwa nchini Uholanzi kwa takribani mwaka mmoja na nusu, imeachiwa na kurejea nchini juzi.
“Leo niko hapa kuwapa habari njema, siku chache zilizopita niliwajulisha kuna ndege yetu tulikuwa na kesi nchini Uholanzi ikakamatwa, ilikuwa chini ya mikono ya sheria. Bahati nzuri tumefanya mazungumzo na jambo limekwenda vizuri, ndege yetu imerudi jana (juzi) jioni iko Tanzania,” alisema Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa.
Alisema ndege hiyo kwa sasa imo kwenye mchakato ili ianze shughuli zake.
“Chuma kimerejea kiko Tanzania, tunaendelea kuimarisha shirika letu, mambo yetu yatakuwa yanaendelea kuwa mazuri,” aliongeza kusema Msigwa, aliyezungumzia masuala mbalimbali, ikiwamo miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo tofauti nchini.
“Tunataka kuboresha shirika letu la ndege. Tunafahamu tumepokea ndege ya mizigo na habari njema jana (juzi) imeanza safari zake za kusafirisha mizigo Dubai na itakwenda Marekani. Tuna ndege zetu nyingine tatu ambazo zitakuja mwishoni mwa mwaka huu na mapema mwakani,” alisema.
Gazeti hili Desemba Mosi, 2022 liliripoti taarifa ya Serikali ikiwatoa hofu Watanzania kuhusu kushikiliwa kwa ndege hiyo, ikisema haiwezi kutaifishwa kutokana na rufaa ya kesi iliyokuwa ikiendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa wakati huo, viliripoti kuhusu mwekezaji wa Sweden aliyeshinda tuzo ya Dola 165 milioni (Sh380 bilioni) dhidi ya Tanzania na kuishawishi Mahakama ya Uholanzi kushikilia ndege hiyo kama kigezo cha kushinikiza malipo yake, licha ya kutopata uhalali wa ICSID.
Akizungumzia suala hilo kwa wakati huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi alikiri mwekezaji huyo kushinda tuzo hiyo na ndege kushikiliwa.
Kituo hicho cha ICSID chini ya majaji watatu, Christopher Greenwood, Stanimir Alexandrov na Funke Adekoya, kilitoa tuzo kwa niaba ya kampuni ya Eco Energy na kuamuru Tanzania kulipa kiasi hicho cha fedha Aprili mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa zilizonukuliwa katika mashirika ya kimataifa, ndege hiyo ilikuwa uwanja wa ndege wa Maastricht, nchini humo tangu Januari mwaka jana kwa madai ya hitilafu za kiufundi katika injini yake.
“Ni kweli kwamba walienda katika mahakama ya nchini Uholanzi baada ya sisi kufanikiwa kubishana na ICSID ili kusitisha utekelezaji, lakini kila kitu kiko chini ya udhibiti,” alisema Dk Feleshi.
Alisema Serikali ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya Uholanzi na kwamba hawezi kueleza mengi juu ya suala hilo.
Kiini cha mgogoro
Septemba 20, 2017 gazeti hili liliripoti kuhusu uamuzi wa Eco Energy Group kuwasilisha madai ya usuluhishi ya dola milioni 500 dhidi ya Serikali juu ya uamuzi wake wa kufuta umiliki wa ardhi ya mradi wa sukari mjini Bagamoyo. Kamishna wa Ardhi aliieleza Kampuni ya Eco Energy Group Novemba 2017, kuwa Serikali iliazimia kufuta hati miliki ya hekta 20,400 na kuweka jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uamuzi huo ulichagizwa na madai ya Eco Energy, inayomilikiwa na raia 18 wa Sweden na viongozi wa biashara kuwasilisha madai yake ICSID mwaka 2017 chini ya mkataba wa uwekezaji baina ya Sweden na Tanzania, ikilalamika uamuzi wa Serikali kuvunja mkataba wa kuendeleza mradi wa miwa Bagamoyo.
Mradi huo ulikusudiwa kuzalisha sukari kwa ajili ya kuuza nje ya nchi pamoja na kemikali ya ‘ethanol’ kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme. Mwekezaji aliilalamikia pia Serikali kutoanzisha udhibiti mpya wa sekta ya sukari na kutoa ardhi bila kazi.
Takukuru kupigwa jeki
Katika hatua nyingine, Msigwa alisema Serikali imepanga kuongeza ajira mpya za maofisa 800 katika Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru).
Alisema watasambazwa kwenye maeneo mbalimbali ili kukabiliana na vitendo vya rushwa katika miradi, ikiwamo ya kimkakati.
Alisema bado kumekuwa na ubadhirifu katika miradi nchini na ili kudhibiti wamejipanga kuongeza watumishi wapya.
“Nataka niwaambie wale wote ambao wamebeba dhamana ya kusimamia rasilimali za umma, huwezi ukafanya ubadhirifu kwenye miradi ya umma ukabaki salama. Utafikiwa tu,” alisema Msigwa.