Mpango wa Sh17.92 bilioni kuinua wanawake kibiashara

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima (wa tatu kulia) akiongoza uzinduzi wa Mpango wa 'ANAWEZA' ambao utamsaidia mwanamke kujikwamua kiuchumi.
Muktasari:
- Mpango huo wa miaka mitano wenye thamani ya dola za Marekani 7.5 milioni sawa na Sh17.92 bilioni unalenga kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa wanawake na ushiriki wao katika uongozi, kuongeza idadi ya wanawake wafanyabiashara na upatikanaji wa huduma za kifedha na zisizo za kifedha katika biashara zao.
Dodoma. Serikali imezindua mpango miaka mitano wenye thamani ya dola za Marekani 7.5 milioni sawa na Sh17.92 bilioni, ukiwa na lengo la kumkomboa na kumwinua mwanamke kichumi.
Taarifa zinasema mpango unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), ambapo nyanja zingine zitaangaliwa ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wanawake katika kuhakisha nyadhifa za uongozi lakini pia kuanzisha na kukuza biashara zao.
Hayo yameelezwa leo Mei 31 jijini hapa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima alipozungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango katika uzinduzi wa mpango wa ‘Anaweza.’
Waziri Gwajima amesema mpango huo unalenga kumkomboa mwanamke kiuchumi, na kwamba umekuja kwa wakati muafaka ambapo Tanzania ipo katika jitihada za kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi.
“Rai yangu kwenu hakikisheni ushiriki mkubwa wa walengwa ili kufikia malengo mazuri ya programu,” amesema na kuongeza;
“Ninafuraha kuona kuwa mradi huu utafungua fursa za kiuchumi kwa wanawake na utasaidia sekta binafsi kukuza ushiriki wa wanawake kwenye uchumi wa Tanzania.”
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma amesema Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hussein Mwinyi ameendelea kuwaamini wanawake kwani ameteua mawaziri sita katika serikali yake.
“Rais alisema hatujamuangusha na sasa hivi anaendelea kuwachagua mpaka katika sekta binafsi na ameanzisha program maalumu ya kupinga ukatili ambayo wanaume wanazungumza na wanaume wenzao kuhusu haki za wanawake,” amesema Waziri huyo.
Naye, Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), Jumoke Jagun amesema mpango huo wenye thamani ya dola za Marekani 7.5 milioni sawa na Sh17.92 bilioni una malengo matatu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, malengo hayo ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa wanawake na ushiriki wao katika uongozi, kuongeza idadi ya wanawake wafanyabiashara na upatikanaji wa huduma za kifedha na zisizo za kifedha kwa ajili ya biashara zinazomilikiwa na wanawake.
Pia, kuimarisha biashara za wanawake ziweze kuongeza uzalishaji wa mtaji na kupata masoko katika sekta muhimu kama vile biashara ya kilimo, viwanda, huduma za kidijitali na utalii.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IODT), Said Kambi amesema mpango huo utawasaidia wanawake kuweza kujikwamua kiuchumi na kuwapeleka katika fursa mbalimbali.