Wanawake wajasiriamali wapewa siri ya mafanikio

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) Mwajuma Hamza akizungumza wakati wa kongamano la Wajasiliamali lililofanyika jijini Dar es Salaam
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC) Mwajuma Hamza, ametoa wito kwa wajasiriamali nchini kujiunga na taasisi za kibiashara zinazohusika na aina ya shughuli wanazozifanya.
Hamza ametoa wito huo leo Alhamisi, Aprili 27, 2023 wakati wa kongamano la wajasirimali lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Commmunications Limited (MCL) kwa lengo la kujadili namna ya kuwezesha biashara changa, za chini, ndogo na za kati (MSMEs) kukua haraka.
Kongamano hilo linalofanyika katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki jijini Dar es Salaam limedhaminiwa na Benki ya CRDB, Kampuni ya usafirishaji ya DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media na Ukumbi wa mikutano wa Dome.
Hamza amesema fursa bado ni kubwa kwa Tanzania kwa sababu imezungukwa na nchi nyingi zilizopo kwenye Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hivyo wajasirimali wazitumia vyema
“Ni muhimu kwa mjasiriamali kujiunga na taasisi za kibiashara zinazohusiana na kile wanachokifanya kwa ajili ya kujua jambo gani lipo sokoni na kinachoendelea duniani,” amesema Hamza wakati akichangia mada isemayo uvumbuzi kwa ajili ya ukuaji.
Kuhusu ujasiriamali na wanawake Hamza, amesema zaidi ya asilimia 54 ya MSMEs hapa Tanzania ni wanawake kwa mchango wake katika pato la nchi na soko la ajili kundi hilo ndilo limeshikilia uchumi wa nchi.
Anasema MSMEs wanachangia zaidi ya asilimia 40 katika pato la Taifa huku wakichangia zaidi ya asilimia 90 ya ajira zote.
Hamza amesema changamoto kubwa wanayoiona wanawake wajasiriamali ni miundombinu ambapo licha ya kupitia mafunzo lakini miundombinu ya kuwawezesha kuingia sokoni ni changamoto.