Mavunde afuta leseni za uchimbaji zisizotumika, aonya wanaoshikilia maeneo
Waziri wa Madini, Antony Mavunde, akikabidhi leseni za uchimbaji kwa wachimbaji wadogo wa madini katika Kijiji cha Gulumwa, Kata ya Mhande, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba.
Muktasari:
- Eneo la hekari 5,441 lilikuwa limeshikiliwa na watu wachache, na kuwazuia wachimbaji wa Wilaya ya Kwimba kufanya shughuli za uchimbaji wa madini. Hali kama hiyo pia ipo katika maeneo mengine ya nchi.
Mwanza. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Serikali imeanza operesheni ya kufuta leseni za uchimbaji wa madini ambazo wamiliki wake wamekuwa wakizishikilia bila kuziendeleza, akisisitiza kuwa hatua hiyo haitabaki Mkoa wa Mwanza pekee, bali itatekelezwa nchini kote ili kufungua fursa kwa wachimbaji wenye nia ya kufanya kazi.
Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikiendelea kutekeleza mageuzi katika sekta ya madini yenye lengo la kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia zaidi ukuaji wa uchumi, ajira na mapato ya Serikali badala ya kubaki mikononi mwa watu wanaozuia maendeleo kwa kushikilia maeneo bila shughuli za uchimbaji.
Akizungumza jana, Julai 17, 2026, wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo katika Kata ya Mhande, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Mavunde amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kupata leseni na kuzihifadhi kwa muda mrefu bila kuendeleza shughuli za uchimbaji.
Amesema hali hiyo imekuwa ikiinyima Serikali mapato na kuwanyima maelfu ya wananchi, hususan vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, fursa za kujipatia kipato kupitia sekta ya madini.
"Nimefuta leseni katika maeneo mengi ya Mkoa wa Mwanza na nitaendelea kufuta nchi nzima. Nataka watu waache kushikilia maeneo. Maeneo yafanyiwe kazi. Kila eneo ukiligusa watu wanasema ni lao, lakini hawafanyii kazi. Tunawaacha vijana, akinamama na watu wenye ulemavu wakikosa shughuli za kiuchumi kwa sababu ya watu wachache," amesema Mavunde.
Amesema katika Wilaya ya Kwimba pekee, eneo lenye ukubwa wa hekari 5,441 lilikuwa limehodhiwa na watu wachache kwa muda mrefu bila kuendelezwa, hali iliyowazuia wachimbaji wadogo kupata maeneo ya kufanya shughuli za uchimbaji.
Waziri huyo amesema tabia hiyo haipo Kwimba pekee, bali imejitokeza pia katika maeneo mengine nchini, jambo linalolazimu Serikali kuchukua hatua za kufuta leseni ambazo hazitumiki kwa mujibu wa masharti yake.
Hata hivyo, amewataka wachimbaji wadogo kuheshimu sheria kwa kuepuka kuvamia maeneo yenye leseni halali, akisema kufanya hivyo kunaleta changamoto wakati wa ukaguzi na kufuatilia iwapo mmiliki ametimiza masharti ya leseni.
"Nasisitiza tena, ni marufuku kuvamia leseni ya mtu mwingine. Mnanipa kazi ngumu ya kufuta leseni kwa sababu baadhi ya maeneo mnayavamia, na tunapokwenda kufanya ukaguzi ushahidi unapotea," amesema.
Katika hatua nyingine, Mavunde ameliagiza Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kupeleka mashine ya kuchoronga madini katika Wilaya ya Kwimba ili kusaidia shughuli za utafiti na uchimbaji.
Pia amemwagiza Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Mwanza kuhakikisha huduma za ugani zinaimarishwa katika eneo hilo ili kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kuhusu mbinu bora za uchimbaji na uzingatiaji wa sheria.
Katika hafla hiyo, jumla ya leseni 30 zilikabidhiwa kwa vikundi 30 vya wachimbaji wadogo, ikiwa ni sehemu ya leseni 282 zinazotarajiwa kunufaisha zaidi ya wachimbaji 300 katika Kijiji cha Gulumwa, Kata ya Mhande.
Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Mwanza, Nyaisara Mgaya, amesema baadhi ya waombaji bado hawajapatiwa leseni kutokana na kutokamilisha masharti mbalimbali, ikiwemo malipo na nyaraka za utambulisho.
"Tunawaomba waliobaki wakamilishe taratibu walizoelekezwa ili nao waweze kupatiwa leseni zao," amesema.
Baadhi ya wachimbaji waliofaidika na mpango huo wamesema utoaji wa leseni utapunguza migogoro iliyokuwa ikitokea kutokana na uchimbaji katika mashamba ya watu bila utaratibu.
Katibu wa Wachimbaji wa Wilaya ya Misungwi, Bahati Boniface, amesema changamoto kubwa inayowakabili ni taasisi za fedha kutokuwa na imani ya kuwapatia mikopo ya kuendeleza shughuli zao.
"Taasisi za kifedha bado hazituamini. Lakini sisi wachimbaji tunaaminiana kiasi kwamba tunaweza kukopeshana hata Sh200 milioni na fedha zikarudishwa," amesema.
Naye mchimbaji mdogo, Peter Charles, amesema kabla ya kupata leseni walilazimika kufanya uchimbaji katika maeneo yasiyo rasmi, jambo lililosababisha migogoro na wamiliki wa mashamba.
"Tulikuwa tunaonekana kama wavamizi, lakini sasa tumepata maeneo halali na tutafanya kazi kwa utaratibu," amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wanawake Mkoa wa Mwanza, Helen Paulin, amesema leseni hizo zitawawezesha wanawake kuongeza kipato na kuchangia zaidi mahitaji ya familia.
"Awali tulikuwa tunadharauliwa, lakini sasa tunachangia uchumi wa familia na kupunguza mzigo kwa waume zetu," amesema.
Mkoa wa Mwanza una zaidi ya vikundi 120 vya wachimbaji wanawake, huku kila kikundi kikiwa na zaidi ya wanachama 50.