Mambo ya kufanywa kuepusha upotevu wa mapato ya halmashauri

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere. Picha na Maktaba.
Muktasari:
- Wadau waanika sababu, njia za kufanywa ili kuepusha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Dar es Salaam. Wakati ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ikionesha upotevu wa mapato ya baadhi ya halmashauri nchini, wadau katika sekta ya fedha na uchumi wameshauri njia za kufanya ili kidhibiti upotevu huo unaoitia hasara Serikali.
Wadau hao wametoa mapendekezo katika mjadala Mwananchi X Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) uliofanyika usiku wa jana Jumatano Aprili 23, 2025 ukiwa na mada inayohoji: Nini kifanyike kudhibiti upotevu wa mapato halmashauri?
Hata hivyo, kukosekana kwa kanzidata za wafanyabiashara, mifumo ya ukusanyaji, baadhi ya watumishi wasiowaaminifu ni miongoni mwa sababu zilizotajwa za kupotea kwa mapato.
Msingi wa mjadala huo ni ripoti za CAG kwa mwaka 2023/24 zilizowasilishwa bungeni wiki iliyopita zikionesha uvujaji wa mapato kwa baadhi ya halmashauri nchini.
Akizungumza katika mjadala huo, Mhadhiri wa Fedha, Uhasibu na Kodi, Chuo cha Serikali za Mitaa Dodoma, Charles Matekele amesema kukosekana kwa kanzidata za wafanyabiashara ni moja ya chanzo cha kupotea kwa mapato ya mamlaka za serikali za mitaa.
Kukosekana kwa kanzidata amesema kunawafanya wafanyabiashara na watu wengine wasio na leseni wafanye shughuli zao bila kulipa ushuru au tozo mbalimbali za Serikali.
“Sababu nyingine ni uwezo hafifu wa kuthibitisha taarifa za mauzo hivyo halmashauri zinashindwa kujua je, kampuni fulani kwa mwaka husika imeuza kiasi gani na imelipa ushuru kiasi gani.
“Jambo lingine ni udhibiti hafifu wa mifumo ya ndani kwa maana mifumo yetu bado ina changamoto. Mambo yote haya yanaleta maswali kuwa kwamba halmashauri zina kila kitu lakini zinashindwa kudhibiti mapato, maana kuna mahali hapajakaa sawa kuna udhaifu,” amesema.
Amesema unaweza kushangaa na kujiuza je, mwekahazina wa halmashauri, jiji, manispaa au kamati ya fedha, baraza la madiwani, mkaguzi wa ndani, hawa wote wameshindwa kufanya kazi zao vizuri?
Akishauri cha kufanya amesema lazima jukumu la kukusanya mapato au ushuru lihamishiwe Serikali Kuu upande wa TRA, wakusanya mapato ya halmashauri wapewe adhabu stahiki, mfumo wa udhibiti wa ndani ufanyiwe marejeo, pamoja na kuwa na viongozi wenye utaalamu wakiwemo madiwani.
Ushauri huo unashabihiana na aliyosema, Mkaguzi wa mahesabu, mshauri wa fedha na uwekezaji, Ahobokile Mwaitenda kwamba halmashauri zinatakiwa kuimarisha mifumo ya Tehama kwa sababu siku hizi makusanyo yanategemea teknolojia.
"Wanatakiwa kuimarisha mifumo ya Tehama maana siku hizi hakuna haja ya kwenda ofisini kwa mtu, mfano anayeuza TV na anatumia Tehama ni lazima kulink (kuunganisha) na mfumo wako ili kuweza kuyaona mauzo yake," amesema.
Jambo lingine ni mafunzo kwa wafanyakazi ambao bado wanatumia malipo ya mkononi badala ya kulipa kielektroniki.
Pia, kupunguza urasimu kwa sababu lengo la kuweka halmashauri ili maendeleo yafike haraka kwa wananchi, lakini kuna uamuzi wa matumizi lazima yarudi kwa waziri makao makuu na matokeo yake pesa nyingi zinakwama.
Meneja Huduma na Uendeshaji Benki ya NBC Nyanda za Juu Kusini, Stanslaus Sana yeye amesema lazima kuwe na muunganiko wa taarifa kuanzia ukusanyaji hadi zinapokwenda katika taasisi za kibenki.
Amesema lazima tujiulize tatizo la pesa kutofika mahali husika lipo kwenye mfumo wa ukusanyaji mapato au wakusanyaji wa mapato ndipo tutafahamu kwanini pesa hazifiki.
“Suluhisho la hili lazima kuwe na namna nzuri ya ku-Link (Kuunganisha) kati ya pesa zinazokusanywa hadi pale zinapoenda kama ni Benki Kuu au taasisi za kifedha,” amesema Sana.
Amesema lazima Serikali ije na mfumo dhabiti wa ukusanyaji wa mapato pamoja na mnyororo wa mawasiliano.
Brighton Lunana, mdau kutoka Tarime Vijijini amesema kupotea kwa mapato kumechangiwa na watumishi wa halmashauri ambao wanatakiwa kuhamia kwenye maeneo yao ya kazi lakini hawafanyi hivyo na matokeo yake wanaendelea kuishi mjini na kuchukulia kila siku kupelekwa vijijini.
Amesema kitendo cha kuwachukua kutoka mjini na kuwapeleka kijijini ingesaidia kupunguza gharama na matumizi ya fedha ambayo hayana ulazima kwenye halmashauri kwa wao kuishi katika maeneo yao ya kazi.
"Sifikirii kama tunaweza kutunza fedha zetu kwa watumishi wa Serikali tulionao tunahitaji kupata mtu ambaye atawasimamia hawa ili wajue kwamba hizi rasilimali ni za Taifa na siyo za watu wachache," amesema.
Munana amesema ni jambo la kuwa na viongozi waadilifu ambao wanatunza mali za umma kwa kuamini kuwa walipa kodi wafanyabiashara ndogondogo.
Hivyo, amesema ili kudhibiti pesa za umma lazima kudhibiti watumishi wa Serikali kuwe na mabadiliko kwenye halmashauri kwa kuwa na watu waadilifu na anapokosea anatolea na kupelekwa mwingine.
Mdau wa masuala ya uchumi, Eugene Kabendera ameshauri kuwapa fursa wananchi kuchagua wawakilishi inavyopaswa kwa upana wake, kwani watu hao watakuwa na uchungu na mapato pamoja na kusimamia kwenda mahala husika.