Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa avutiwa juhudi Exim, atoa maagizo

Muktasari:

  • Majaliwa avutiwa na huduma za Exim katika jitahada za kuwafikia wananchi hasa wa pembezoni, azitaka taasisi za huduma za kifedha kuendelea kutoa elimu kuhusu sekta hiyo.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameonyesha kuvutiwa na jitihada zinazofanywa na Benki ya Exim Tanzania ikiwemo kuongeza wigo na kusogeza huduma karibu na wananchi.

Majaliwa amesema hatua hiyo inasaidia kukuza uchumi wa maeneo husika na kuimarisha utangamano wa kijamii.

Waziri Mkuu huyo, ameeleza hayo jana Jumatano Novemba 22, 2023 jijini Arusha alipotembelea banda la maonyesho la benki hiyo muda mfupi kabla ya kufungua maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha yanayoendelea kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini humo.

“Niwapongeze jitihada mnazoendelea kuzifanya katika kutoa huduma, jitihada zaidi zinahitajika ili huduma nzuri mnazoendelea kuzitoa ziwafikie wananchi wengi hasa waliopo pembezoni wasiofikiwa na huduma,” amesema Majaliwa.

Pia, ametumia fursa hiyo kuwataka watoa huduma za kifedha kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa umma sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji wa huduma hizo zikiwemo riba na ada. ili wananchi wengi kunufaika.

Akiwa kwenye banda la Exim, Majaliwa alipewa maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na benki hiyo kutoka kwa meneja masoko na mawasiliano wa benki hiyo, Kauthar D’Souza aliyemwelezea kuhusu mkakati wa kuongeza wigo wa utoaji wa huduma zao.

D’ Souza amesema licha ya jitihada za benki hiyo katika kuongeza wigo nchini, hivi sasa ina mtandao wa matawi 33 na mawakala 1500 nchi nzima.

Hata hivyo, D’Souza amesema mkakati wa Exim ni kuwekeza zaidi katika utoaji wa huduma kupitia ubunifu wa kidijitali ili kutoa suluhisho la kibenki linalofaa na salama kwa wateja wake.

“Tunatambua wajibu tulionao katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi hapa nchini, ndio sababu moja ya kipaumbele chetu ni kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara wakiwemo wanawake na wajasiriamali,” amesema D’Souza.

Katika ufunguzi wa maonyesho hayo, Majaliwa ameitaka Wizara ya Fedha iimarishe mifumo ya kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha, ili baadhi ya watoa huduma wasio waadilifu wasitumie changamoto ya uelewa mdogo wa masuala ya fedha kwa baadhi ya wananchi na kuwadhulumu.

Majaliwa amesema Wizara ya Fedha iendelee kushirikiana na watoa huduma za fedha kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo muhimu yakiwemo ya usimamizi wa fedha binafsi, kuweka akiba, mikopo, uwekezaji kupitia hatifungani na hisa, bima, mpango wa kujiandaa na maisha ya uzeeni pamoja na kodi.

“Wizara ya Fedha iandae mpango maalumu wa kutoa hamasa kwa Watanzania, ili wajenge utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha, pia elimu iendelee kutolewa kuhusu wajibu wa kila mmoja kudai na kutoa risiti kwa malipo yanayofanyika," amesema Majaliwa.