Magavana benki kuu SADC kujadili namna ya kulinda uchumi
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Mkutano wa 62 wa Magavana wa benki kuu za nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) unafanyika wakati ambapo nchi nyingi duniani zinaendelea kukabiliwa na shinikizo la mfumuko wa bei, misukosuko ya masoko ya fedha na athari za migogoro ya hasa mashariki ya kati.
Dar es Salaam. Magavana wa benki kuu kutoka nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana jijini Dar es Salaam kujadili mikakati ya kulinda uchumi dhidi ya changamoto za kiuchumi duniani zinazoongezeka.
Majadiliano hayo yanahusisha mivutano ya kisiasa ya kimataifa, mabadiliko ya bei za nishati na misukosuko katika biashara ya kimataifa.
Mkutano wa 62 wa magavana wa benki kuu za SADC unafanyika wakati ambapo nchi nyingi duniani zinaendelea kukabiliwa na shinikizo la mfumuko wa bei, misukosuko ya masoko ya fedha na athari za migogoro ya hasa mashariki ya kati.
Akizungumza kabla ya mkutano huo leo Alhamisi Juni 11, 2026 jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa watunga sera wa kikanda kutathimini hali ya uchumi na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wa SADC dhidi ya mishtuko ya nje.
“Tupo hapa kujadili maendeleo ya kiuchumi katika nchi 16 za SADC na kuweka mikakati ya kujilinda dhidi ya changamoto za kimataifa. Tumeona jinsi uchumi wa dunia unavyotikiswa na ni wajibu wetu kuhakikisha mifumo ya kifedha na kiuchumi ya ukanda wetu inakuwa imara,” amesema Tutuba.
Amesema magavana wanatarajiwa kujadili hatua za kuimarisha mifumo ya malipo ya kikanda, kuongeza ukwasi katika sekta ya fedha na kusaidia ukuaji endelevu wa uchumi huku wakidhibiti mfumuko wa bei.
“Mifumo ya malipo ni mhimili wa uchumi wa kisasa. Tunajadili namna ya kuisimamia kwa ufanisi ili kuhakikisha uhamishaji wa fedha ndani ya SADC unakuwa salama wa haraka na wa gharama nafuu,” amesema.
Tutuba amesema kupitia kile kinachoendelea duniani, mfumuko wa bei unaoongezeka ni changamoto kubwa kwa watunga sera duniani, hali inayowalazimu benki kuu kuweka sawa sera za fedha na haja ya kuunga mkono shughuli za kiuchumi.
Katika muktadha huo amesema Tanzania imeendelea kudumisha kiwango cha mfumuko wa bei kilicho thabiti zaidi katika ukanda wa SADC, ambapo ongezeko lake limebaki ndani ya lengo la BoT la asilimia tatu hadi tano.
“Katika baadhi ya nchi, mfumuko wa bei umefikia zaidi ya asilimia 12 lakini Tanzania umebaki ndani ya viwango vilivyokubalika. Tunaendelea kutumia zana za sera ya fedha kuhakikisha mfumuko unabaki katika kiwango kinachokubalika,” amesema.
Mkutano huo pia unafanyika sambamba na maandalizi ya maadhimisho ya miaka 60 ya BoT yatakayofanyika kesho Ijumaa Juni 12 hatua ambayo Tutuba amesema ni fursa ya kutafakari mchango wa taasisi hiyo katika mageuzi ya kiuchumi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966 chini ya Rais wa kwanza wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Katika kipindi hicho amesema benki imebadilika kutoka kusimamia mfumo wa uchumi uliotegemea zaidi fedha taslimu hadi kusimamia mfumo wa kisasa wa malipo ya kidijitali unaowezesha miamala kufanyika kwa sekunde chache.
“Leo mtu anaweza kufanya malipo kupitia simu ya mkononi, QR code au Mfumo wa Malipo wa Papo kwa Papo wa Tanzania (TIPS) au kuhamisha fedha kwa haraka kutoka benki moja kwenda nyingine. Haya ni mafanikio makubwa yaliyotokana na mageuzi ya mfumo wa kifedha nchini,” amesema.
Kwa mujibu wa Tutuba, matokeo ya mageuzi hayo yanaonekana katika mwenendo wa uchumi wa Tanzania ambao ulikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025 kiwango kilicho juu ya wastani wa ukuaji wa dunia wa asilimia 3.2.
Pia sekta ya benki pia imeimarika ambapo kiwango cha mikopo chechefu kimeshuka hadi asilimia 2.9 Machi mwaka huu chini ya kiwango cha kimataifa cha asilimia 5.
Kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 60, BoT itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kitaifa kujadili namna Tanzania inaweza kukabiliana na changamoto mpya za uchumi wa dunia na kutumia fursa zinazotokana na teknolojia ya fedha na akili mnemba.
“Tunaamini miaka 60 ni mwanzo wa safari nyingine ya ubunifu. Tunataka kuona mifumo ya kifedha inayowafikia Watanzania wengi zaidi, kurahisisha miamala ya biashara na kusaidia ukuaji wa uchumi unaowanufaisha wananchi,” amesema Tutuba.