Prime
Macho na masikio yako hapa bajeti ikisomwa leo

Wabunge wameeleza matarajio yao katika bajeti ya Serikali ya lala salama kabla ya kuvunjwa kwa Bunge la 12 huku wengine wakionesha hofu ya kusuasua kwa upelekwaji wa fedha za maendeleo.
Machi 11,2025, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwasilisha Mwelekeo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26 huku ikionyesha ongezeko la asilimia 13, ikikua kutoka Sh50.29 trilioni katika mwaka wa 2024|25 hadi Sh57.04 trilioni.
Akizungumza na Mwananchi, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Asha Abdallah Juma (Mshua) anasema anatarajia bajeti hiyo itaangalia katika kodi kwa kuhakikisha bidhaa zenye mahitaji makubwa zinapunguziwa kodi.
“Kwa mfano huduma za mawasiliano mitandao wananchi bado wanailalamikia kuwa ni kubwa. Kwa hiyo kodi ishuke kwenye bidhaa na kwenye miamala ya kutuma fedha ili watu wengi waweze kuitumia na kuyapatia pesa makampuni ya mitandao ya simu na Serikali kupitia miamala itakayotumika katika manunuzi,” alisema.
Mshua alisema watu wengi wanapenda kuitumia miamala ya kielektroniki lakini wamekuwa wakikwazika na kodi kubwa wanayotozwa kwenye mitandao ya simu.
Aidha, alisema gharama za usafiri zinaonekana kuwa kubwa na kutolea mfano kwenye treni ya mwendo kasi ambayo wengi wanapenda kusafiri nayo lakini wanashindwa kumudu gharama.
“Nauli inaonekana iko juu ya uwezo wa wananchi, kuna bidhaa zinazotumiwa sana na wananchi zisiwekewe kodi kubwa. Wafanye watakavyofanya basi waongeze kwenye vileo. Maana mtu akishashiba ndio anakwenda kutafuta kileo,” alisema.
Alisema kwenye mazao pia waangalie kuhakikisha kuwa wakulima wanapata bei nzuri ya mazao na ushuru uangaliwe upya ili kutoa unafuu kwa kundi hilo ambalo linabeba Watanzania wengi.
Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM) Pius Chaya amesema mategemeo yake ni kuwa kasi kubwa aliyokuja nayo Rais Samia itaendelea na itakuwa ya kasi kuzidi aliyoyafanya kwenye miaka minne iliyopita.
“Tumeanzisha kilimo cha umwagiliaji sio kwa Manyoni tu, bali nchi nzima ningependa kuona bajeti hii sasa inaendeleza ile miradi mikubwa ambayo Rais ameanzisha lengo kuhakikisha wakulima hawategemei mvua katika uzalishaji na wategemee kilimo cha umwagiliaji ili waweze kulima mara mbili kwa mwaka,” anasema.
Dk Chaya anasema jambo hilo litahakikisha kuwa Tanzania inakuwa na uhakika wa chakula katika kipindi chote.
Anasema wameona mafanikio makubwa katika ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora mkoani Dodoma, hivyo anatamani kuona nguvu kubwa sasa inaelekezwa katika kukamilisha vipande vilivyobakia vya SGR.
“Ukumbuke wakati Rais Magufuli (Hayati John Magufuli) aliacha ujenzi wa SGR ukiwa asilimia 30, lakini kupitia awamu ya Sita, Rais Samia ameenda kuongeza asilimia 70 ndani ya miaka minne hii. Kwa hiyo tuna imani kubwa atakamilisha vipande vilivyobakia,” anasema.
Naye Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM) Charles Mwijage anasema bajeti ijayo itakuwa nzuri kutokana na bajeti za kisekta zilizokwisha wasilishwa.
“Kwa nzuri sana kwa mfano ukichukulia bajeti ya Wizara ya Kilimo, Serikali bado imeendelea kuwekeza zaidi kwenye. Sekta ya kilimo, kwa umwagiliaji, pembejeo kwa wakulima na ukichukulia kazi iliyofanyika mwaka uliopita na sasa ambako sasa pesa zimeongezeka tuna matumaini kwamba tutazalisha chakula cha kutosha,” anasema.
Anasema katika mauzo ya nje Tanzania imeweza kuuza mazao yenye thamani ya Sh35.4 bilioni kwa mwaka uliopita na kuwa kwa uwiano wa fedha zilizotengwa zinaashiria bajeti nzuri.
“Kwa hiyo kwa kupeleka pesa nyingi kule ina maana inakwenda kukamilisha miradi ina maana tutakuja kupata matokeo ya ule uwekezaji wa miaka iliyotangulia na mwaka huu unaokuja,” anasema.
Kwa upande wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mwijage anasema kumekuwa na uwekezaji kwa kuongeza fedha za kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo shule na vyuo vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo Stadi (VETA).
Amesema elimu ya VETA itasaidia watu kupata na kuongezewa ujuzi wa kuweza kujituma kujiajiri wao wenyewe.
“Bajeti inayokuja itakuwa nzuri lakini jambo ambalo tunapaswa tu tuzungumze ukweli kwamba hii bajeti ya inayokuja ni bajeti ya uchaguzi,” alisema.
Mwijage alisema ni jambo la kujivunia kwa Tanzania kujipanga kwa kutumia bajeti yake katika uchaguzi.
Upelekaji wa bajeti ni changamoto
Hata hivyo pamoja na matarajio hayo ya wengi Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee yeye anasema hakuna matarajio mapya kwa sababu bajeti huwa inaleta matarajio makubwa lakini utekelezaji ni changamoto.
Anasema wabunge wamekuwa wakiaminishwa kuwepo kwa nyongeza ya fedha kwenye wizara mbalimbali lakini mwaka unaofuatwa hazionekani kutoka Hazina kwenda zilipopangiwa.
“Hata katika Key Ministry (wizara muhimu) kama Mifugo, Kilimo, Maji, Ujenzi kiwango cha pesa kinatoka hakiendani na kile kilichopitishwa na Bunge. Unakuta ina - range (inacheza) kati ya asilimia 19 hadi asilimia 30 kwa fedha za maendeleo,” anasema.
Anasema bajeti inakuwa na maana kama mambo ambayo mlijipangia katika mwaka husika wa fedha mnatekeleza na hata mkishindwa basi mwaka unaofuta zipelekwe ili isitikise miradi iliyopangwa kufanywa.
Mdee anasema Bunge lilipitisha sheria ya kuanzisha mifuko maalumu mbalimbali ambayo fedha zake zinatokana na ushuru katika mafuta kwa lengo la kusaidia maeneo husika kama maji, barabara, umeme na reli.
“Kwa mfano mwaka jana Bunge limesema kwenye mfuko wa Barabara tukusanye Sh859 bilioni hadi Februari mwaka huu, mmekusanya hizo fedha zinatakiwa zipelekwe Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) ili zijenge, zitengeneze na kulipa madeni ya wakandarasi, sasa zimepelekwa Sh123 bilioni,” anasema.
Mdee anasema watu hawezi kulalamika kama Serikali haikukusanya fedha kwa kadri ya malengo yaliyotarajiwa ila wanalalamika kwa sababu fedha zinakusanywa lakini hazipelekwi kunakotakiwa.
Anasema iwapo ukisoma Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa Machi mwaka huu ambayo inazungumzia ukaguzi wa 2023/24, Serikali katika mwaka huo ilitarajia kukusanya Sh44 trilioni lakini hadi CAG anakwenda kufunga hesa Juni mwaka jana anakuta Sh46 trilioni zilikusanywa.
“Sh2 trilioni juu kwa nini hizo fedha haziwi reflected (haziakisi) katika miradi ya maendeleo? Tungekuwa na upungufu tungesema sawa mambo ndivyo yalivyo. Tuna chajuu, madeni ya wakandarasi hayapungui, Bunge limepitisha mambo hayaendi vizuri. Hela zinapelekwa wapi,” Anahoji.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu Conchesta Rwamlaza anasema anatarajia bajeti hiyo, itajibu matatizo ya wananchi yakiwemo masuala ya miundombinu ya barabara elimu, afya na kutazama makundi mengine ya kijamii hasa wazee.
“Tuseme kwamba bajeti iunganishe makundi yote, isiache mtu nyuma ndio mambo mazuri yanapaswa kuwa bajeti. Bajeti imepanda sasa hivi kwa hiyo nina mategemeo kwamba itaweza kukusaidia kujibu,” alisema.
Anasema matarajio ya Watanzania kutoka kwenye bajeti yao kuhakikisha makundi yote ya kijamii yanashirikishwa katika bajeti na hakuna mtu ambaye anaachwa nyuma.
“Lakini pia kuhakikisha hakuna hii kitu inaitwa drop out (mdondoko wa watoto) kuhakikisha anayetakiwa kumaliza darasa la saba, darasa la 12 (kidato cha nne) wanamaliza,” anasema.
Rwamlaza anasema nchi haiwezi kuwekeza katika elimu halafu kuna watoto hawamalizi masomo yao.