Mabenki Tanzania kutoa huduma rafiki kwa wanawake

Mwenyekiti wa TBA, Theobald Sabi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Muktasari:
- Miongoni mwa mambo yaliyosisitizwa ni sekta ya benki kushughulikia pengo la utoaji wa huduma maalumu za kifedha kwa wanawake wajasiriamali.
Dar es Salaam. Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) umeahidi kutoa bidhaa rafiki za kifedha kwa wanawake ili kusaidia kuondoa vikwazo kama vile ukosefu wa dhamana kwa mikopo.
Mwenyekiti wa TBA, Theobald Sabi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ametoa ahadi hiyo leo Machi 06, 2025 wakati wa mkutano wa viongozi wa benki na sekta ya fedha, ulioangazia kuhakikisha usawa wa huduma za kifedha na kuwawezesha wanawake.
Hata hivyo, amekiri changamoto zilizopo, akisisitiza dhamira ya sekta ya benki kushughulikia pengo la utoaji wa huduma maalumu za kifedha zikiwemo akaunti mahususi kwa wanawake wajasiriamali.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuboresha lugha katika huduma za kifedha ili taarifa za kifedha zinapatikana na kueleweka kwa wote.
“Biashara zinazoendeshwa na wanawake zinapofanikiwa, huzalisha ajira nyingi, kukuza uchumi wa ndani na kuchochea maendeleo jumuishi,” amesema.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, ameeleza umuhimu wa ujumuishwaji wa kifedha, akisema licha ya maendeleo yaliyopatikana, wanawake hasa wa maeneo ya vijijini bado wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo upatikanaji mdogo wa huduma za benki, mahitaji ya dhamana na vikwazo vya lugha.
Amesema utafiti wa hivi karibuni wa FinScope umeonyesha kuwa licha ya juhudi za kupanua huduma za kifedha, bado kuna tofauti za kijinsia.
Ili kukabiliana na hili, benki zinatekeleza mikakati jumuishi ya kifedha inayolenga kuhakikisha upatikanaji kamili wa huduma za kifedha kwa jinsia zote ifikapo mwaka 2030, huku lengo la muda mrefu likiwa ni kufanikisha usawa wa 50-50 katika ujumuishwaji wa kifedha ifikapo mwaka 2033.
“Zanzibar, ujumuishwaji wa kifedha unachukuliwa kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi. Benki zinafanya kazi kuondoa tofauti za kifedha zinazoegemea jinsia, kwa kuendana na Lengo la Maendeleo Endelevu (SDG) namba 5, linalotaka usawa wa kijinsia na upatikanaji kamili wa rasilimali za kifedha kwa wanawake,” amesema.
Sabi amebainisha kuwa umoja huo umepanga kuzindua mipango mipya inayolenga kuwawezesha wanawake kifedha kupitia bidhaa maalumu na programu za uhamasishaji.
Aidha, amesema benki zinapaswa kusaidia wanawake wajasiriamali kwa kuhakikisha wanapata nyenzo muhimu na rasilimali za kifedha.
“Biashara Ndogo na za Kati (SMEs), hasa zile zinazoendeshwa na wanawake, zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi. Kwa kuzisaidia biashara hizi, benki si tu kuwawezesha wanawake, bali pia kuimarisha familia na kuchangia maendeleo ya Taifa,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa kuwa ujumuishwaji wa kijinsia bado ni kipaumbele, taasisi za kifedha zinatambua kuwa kufunga pengo la kijinsia si tu wajibu wa kimaadili bali pia ni hitaji la kiuchumi.
“Kwa kuwapatia wanawake nyenzo sahihi za kifedha na msaada unaohitajika, sekta ya benki inaweka msingi wa mustakabali jumuishi na wenye mafanikio zaidi,” amesema.