Prime
Maana ya sheria ya fedha katika lugha rahisi
Bajeti ya mwaka 2026/27 ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar Juni 11, mwaka huu, inakuja katika kipindi ambacho Tanzania inajitahidi kuimarisha uchumi wake kupitia mabadiliko ya kidijitali na uwekezaji wa kimkakati.
Sheria ya Fedha 2026 (The Finance Act, 2026) ndiyo chombo cha kisheria kinachotekeleza sera hizo kwa kurekebisha sheria 27 tofauti za kodi na mapato ambapo imepitishwa na Bunge na itasainiwa kuwa sheria itakayoanza kutumika Julai 1, mwaka huu.
Hii bajeti ni ya kwanza kwenye utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2050 (Vision 2050) pia ni utekelezaji wa mpango wa nne wa miaka mitano wa Serikali. Serikali imepanga kukusanya na kutumia kiasi cha Sh62.33 trilioni na mada ya bajeti ikiwa ni “Kujenga Ustahimilivu wa Kiuchumi kupitia Mabadiliko ya Kidijitali, Uwekezaji wa Kimkakati na Uendelevu wa Kifedha kwa ukuaji jumuishi.”
Bajeti ya 2026/27 inaonyesha mkakati wa kupanua wigo wa kodi badala ya kuongeza viwango vya juu kwa walipakodi waliopo. Sheria ya Fedha 2026 imeongeza kima cha juu cha mauzo yanayotozwa kodi kwa utaratibu wa makadirio kutoka Sh100 milioni hadi Sh200 milioni, na hivyo kuingiza biashara zaidi katika mfumo rasmi wa kodi.
Kwa upande mwingine, kiwango cha kodi kimeongezeka kutoka 3.5% hadi 4.5% kwa biashara zenye mauzo yanayozidi Sh11 milioni hadi Sh200 milioni. Hata hivyo, biashara mpya zinazosajiliwa zinapewa likizo ya kodi ya miezi 12 motisha muhimu ya kuvutia wafanyabiashara wadogo kuingia katika mfumo rasmi. Hii ni fursa ya kuanzisha na kuendeleza biashara bila kufikiria kodi, kitu ambacho wafanyabiashara wengi wanakiona ni kikwazo.
Sheria pia inataja kodi ya kidijitali kwa watoa huduma za kidijitali wa nje ambao wanatoa huduma hizo kwa watumiaji wa Tanzania. Hii ni njia nyingine ya kuongeza wigo wa kodi.
Sheria pia inasisitiza umuhimu wa usimamizi wa kodi kwa kulazimisha malipo ya kielektroniki, ikiwamo malipo yanayohusiana na uhamisho wa mali kama ardhi, majengo, na magari. Hatua hii itapunguza miamala ya fedha taslimu na kuongeza uwazi katika uchumi. Ni vizuri kujua sasa unapouza ardhi au nyumba au pengine gari hutakiwi kulipia fedha taslimu ila kwa kutumia malipo ya kielektroniki.
Unafuu pia umetolewa kwa wafanyabiashara wenye kulipa kodi ya ongezeko la dhamani yaani (VAT) ambapo serikali sasa inalazimika kurejesha VAT ndani ya siku 30 baada ya maombi kukamilika, na riba itatozwa pale malipo yakichelewa. Hii ni hatua muhimu ya kulinda mtiririko wa fedha wa wafanyabiashara na wawekezaji.
Pia kuna hatua za makusudi kwa wafanyabiashara wanaozalisha bidhaa zao Tanzania ambapo bidhaa nyingi zinazozalishwa ndani ya nchi zinaendelea kupata msamaha wa baadhi ya kodi, wakati bidhaa sawa zinazoagizwa kutoka nje zinatozwa kodi kubwa. Pia serikali inaendelea kulinda sekta ya mafuta ya kula na utengenezaji wa nguo kwa kutumia pamba inayolimwa nchini.
Sera za bajeti hii zina athari mchanganyiko kwa raia wa kawaida kwa mfano likizo ya kodi kwa biashara mpya, ongezeko la mgao wa mikopo ya serikali za mitaa kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu kutoka asilimia 10 ya mapato hadi asilimia 15 na pia dirisha la mikopo ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana ambapo Sh200 bilioni zimetengwa.
Pia kuna mwelekeo wa kukuza usafiri na usafirishaji kupitia magari au vifaa vinavyotumia umeme kwa kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwa vifaa vya kuchajia.
Kuna fursa pia ya ubunifu kutokana na pendekezo la kuanzishwa kwa Kituo cha Fedha cha Kimataifa cha Dar es Salaam (DIFC) na sera za kulazimisha malipo ya kielektroniki ambapo vinafungua fursa katika huduma za kifedha za kidijitali, teknolojia ya malipo, na wabunifu wa sekta ya kifedha (FINTECH).
Kwa ujumla, Sheria ya Fedha 2026 inaweka msingi imara wa kisera kwa ajili ya ukuaji wa kiuchumi endelevu, ingawa mafanikio yake yatategemea ubora wa utekelezaji na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, na wananchi katika kusimamia na kuwajibika kufuata hii sheria ili iweze kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.
Ni matarajio yetu kuwa wataalamu mbalimbali na taasisi za kiserikali zitatekeleza kikamilifu yale yaliyotajwa na ambayo hayakubadilika kwenye sheria nyingine katika kutekeleza mipango tarajiwa.