Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sheria ya fedha inavyong'ata



Dodoma. Wakati Serikali ikikubali kuondoa baadhi ya tozo na ushuru uliokuwa umependekezwa kwenye bajeti ya mwaka 2026/27, Kamati ya Bajeti imekataa pendekezo la kuruhusu Serikali kukopa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa dharura, ikisema ipo njia mbadala ya kupata fedha bila kuathiri majukumu ya benki hiyo.

Hatua hizo zinakuja baada ya Kamati ya Bajeti pamoja na wabunge mbalimbali kupendekeza kufanyiwa marekebisho kwenye bajeti, wakieleza kuwa baadhi ya tozo na ushuru uliopendekezwa ungeongeza gharama za maisha na uzalishaji.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyokubaliwa ni kuondolewa kwa ongezeko la tozo kwa pikipiki, ushuru wa kilo ya sukari inayozalishwa ndani ya nchi na marekebisho ya kodi zilizokuwa zikihusu magari yaliyotumika, hatua zinazotarajiwa kutoa nafuu kwa wananchi na sekta husika."

Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti bungeni jijini Dodoma leo Jumatano, Juni 24, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alipowasilisha muswada wa sheria ya fedha 2026 na Kamati ya Bajeti ilipowasilisha maoni yake kuhusu muswada huo.

Balozi Omar amesema sheria hiyo itaanza kutumika Julai mosi 2026, ambapo pendekezo la tozo ya Sh20 kwa kila sigara 1,000 na Sh20 kwa kilo ya sukari kutoka nje ya nchi limepita na kuelekezwa kwenye Mfuko wa Bima ya Afya Wote.

Awali, Kamati ya Bajeti ilipinga ongezeko la tozo kwa bodaboda kutoka Sh95, 000 hadi Sh150,000 ikisema ingewaumiza na kuwagombanisha vijana na Serikali, hivyo ikashauri jambo hilo liondolewe.

Suala jingine ambalo Serikali imekubali ni kuondoa kifungu cha 69 kilichopendekezwa kuiruhusu BoT kuikopesha Serikali kwa ajili ya dharura.

Kwa sasa Serikali imesema itaendelea na utaratibu wa kutumia mfuko wa dharura kama ilivyokuwa awali.

Kuhusu hilo, Kamati ya Bajeti kupitia mwenyekiti wake, Mashimba Ndaki imesema imebaini Serikali imekusudia kufuta kifungu cha 69 ili kubainisha vigezo ambavyo BoT inaweza kutoa mikopo ya muda mfupi kwa Serikali, endapo kutatokea matukio yasiyotabirika au yasiyozuilika.

Hata hivyo, imesema haikukubaliana na mapendekezo ya Serikali kwa sababu mabadiliko hayo yanaondoa sharti la Benki Kuu kutokopesha Serikali au taasisi nyingine ya umma moja kwa moja au kwa njia nyingine.

Pia, imesema mabadiliko hayo yanaondoa sharti la Serikali kulipa riba kwa kiwango cha soko kwa mkopo utakaochukuliwa, hivi sasa riba inayolipwa ni asilimia tatu.

“Masuala yote yaliyobainishwa katika tafsiri ya matukio yasiyotabirika au yasiyozuilika, kwenye muswada, hayana tofauti na tafsiri ya maneno maafa yaliyopo kwenye Sheria ya Usimamizi wa Maafa,” imesema.

Kamati hiyo imeeleza matumizi hayo yanatakiwa kugharamiwa na mfuko wa dharura na si mkopo.

Marekebisho hayo, pia yamegusia Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Miamala ya Kielektroniki, ushuru wa bidhaa, usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi, ushindani, Sheria ya Michezo ya Kubahatisha na Sheria ya udhibiti wa uingizaji wa bidhaa nchini.

Nyingine ni Sheria ya Kodi ya Mapato, uwekezaji na maeneo maalumu ya kiuchumi, Sheria ya Ardhi, ukadiriaji majengo katika serikali za mitaa, sheria ya fedha ya serikali za mitaa, Sheria ya madini, ada ya usajili na uhamishaji wa magari na Sheria ya Tume ya Taifa ya Mipango.

“Napenda kulitaarifu Bunge lako, wakati wa majadiliano baina ya Serikali na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Muswada huu, tumefanya maboresho katika maeneo ya kadhaa ikiwemo kupunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa wa asilimia 20 kwenye magari yenye umri wa miaka minane, lakini hayazidi miaka 10 iliyopendekezwa iwe hadi asilimia 18,” amesema.


Magari mitumba

Muswada pia umepunguza ushuru kwenye magari yenye miaka inayozidi 20 na kuendelea uliopendekezwa kutoka asilimia 50 na kuwa asilimia 40 huku ikiondoa pendekezo la ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia tano kwenye pikipiki kama ilivyopendekezwa.

“Serikali imepunguza kodi kwa walipa kodi wa chini ya utaratibu wa makadirio kutoka kiwango cha asilimia 4.5 kinachopendekezwa hadi asilimia 4 kwa mapato yanayoanzia Sh11 milioni hadi Sh200 milioni,” amesema Waziri.

Ametaja lengo la marekebisho hayo ni kuendana na misingi ya usawa ya utozaji kodi na kuhakikisha ushindani wa haki baina ya watoa huduma wa kawaida na wa mtandao, ili kuongeza wigo wa kodi na mapato ya Serikali.

Kwa upande wa halmashauri, wamegusa kodi ya majengo ambayo imekuwa ikihamishwa mara nyingi kupelekwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini sasa imerudishwa halmashauri ambazo zitakusanya kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).


Bima ya Afya

Katika mapendekezo hayo imetajwa kodi mpya zitakazogharamia ambapo mbali na tozo ya sigara na sukari kutoka nje ya nchi kwa ajili ya bima kwa wote, kwenye zawadi ya ushindi katika michezo ya kubahatisha ongezo la asilimia 15 litagawiwa maeneo mawili, asilimia 70 itakwenda mfuko wa kudhibiti Ukimwi na asilimia 30 nayo itapelekwa bima kwa wote.


Kibano bidhaa za kucha

Kwa upande mwingine, Serikali imewanyima ahueni wenye mashine za kukaushia kucha ambapo ushuru wa kiwango cha asilimia 10 kwenye mashine za rangi za kucha zinazoingizwa nchini imebaki kama ilivyopendekezwa.

Pia kuna ongezeko la ushuru wa bidhaa kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 kwenye bidhaa za urembo zinazoingizwa nchini, ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye viatu vya plastiki vinavyoingizwa na kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye magari yanayotambulika kwa HS Code 8703.21.90 yenye ukubwa wa injini (CC) usiozidi 1,000.

Maumivu mengine yako kwa wavuvi ambako nyavu zitokazo nje zimeongezewa ushuru kwa asilimia 10 ingawa eneo hilo limetajwa na wabunge kuwa linapeleka kilio na kusababisha wavuvi waendelee kutumia nyavu chakavu zisizo na ubora.


Kamati ya Bajeti

Hata hivyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya bajeti, imesema haikukubaliana na mapendekezo ya Serikali yanayoondoa sharti la Benki Kuu kutokopesha Serikali na Taasisi nyingine ya umma moja kwa moja au kwa njia nyingine.

Wamesema mabadiliko hayo yanaondoa sharti la Serikali kulipa riba kwa kiwango cha soko kwa mkopo utakaochukuliwa wakisema kwenye muswada hakuna tofauti na Tafsiri ya maneno Disaster yaliyopo kwenye sheria ya Usimamizi wa Maafa.

“Kamati iliona kuwa Serikali ina mawanda mapana ya kupata mikopo kwa ajili ya kugharamia matumizi ya dharura,hivyo basi, haikukubaliana na mapendekezo na imewasilisha jedwali la marekebisho ya Kamati,”amesema Mashimba.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ndaki amesema ni lazima kudhibiti biashara za magendo ambazo licha ya kuwa zinalipa kodi, bali baadhi ya bidhaa zinazopitia njia hii si salama.

“Kamati inaishauri serikali kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato (TRA) kuhakikisha watu wanaofanya biashara ya magendo wanachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufilisiwa,”amesema Ndaki.

Mashimba, ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na uvuvi kutokufanya mabadiliko kwenye baadhi ya maeneo ili kutoongeza ada ya kila mwaka ya leseni ya vyombo vya uvuvi.

Mwenyekiti, ametaja eneo lingine ni kutoongeza ada ya kusafirisha samaki nje ambayo inapendekezwa kuwa Sh75 kwa kilo na kutoongeza ushuru wa kusafirisha samaki au mazao ya uvuvi.

Ametahadharisha endapo Serikali itaendelea na viwango pendekezwa, samaki wanaovuliwa katika Ziwa Victoria watauzwa katika masoko ya nchi jirani kwa sababu ziwani bado kuna ugumu wa udhibiti wa mipaka.


Michango ya wabunge

Mbunge wa Gando (ACT-Wazalendo), Said Ali Mbarouk amesema kuondoa tozo ya Sh10 kwenye sukari ya ndani halafu ikaongezwa Sh20 kwa sukari ya nje, bado ni maumivu kwa Watanzania kwa kuwa sukari ya ndani siku zote haijitoshelezi.

“Makali ni yaleyale maana tunaondoa mfuko wa nyuma tunaweka kodi mfuko wa mbele, kama tunataka kuwasaidia Watanzania tuondoe tozo ya sukari kwa ujumla wake,” amesema Mbarouk.

Mbunge wa Kinondoni (CCM), Abbas Tarimba amesema uchumi wa nchi hauwezi kusimama kwa kutegemea kodi zisizotabirika badala yake Serikali iweke msimamo kwa wafanyabiashara ili wapate utulivu.

Kwa upande wake, Mbunge Nanyumbu (CCM) Yahaya Mhata ameitaka Serikali kuwaelekeza Polisi waache kuwasumbua bodaboda kwani inawezekana wamepunguziwa kodi lakini kila siku ikiwa ni usumbufu wa kukimbizana na polisi.

Mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo ameipongeza Serikali kwa kuwa sikivu kuyafanyia kazi maoni mengi ya kamati ya bajeti kuhusu maboresho ya muswada huo. 

Amesema Serikali ilileta muswada wa kufanya marekebisho kwa wanaotumia vyombo vya moto, hasa bodaboda.

“Niliona kiu ya wabunge hili, wakitueleza wajumbe wa kamati ya bajeti kuhusu kutokukubaliana na hoja hiyo. Hakuna jimbo hapa ambalo halina mchango wa bodaboda au kuthamini mchango wao,” amesema.