Malimbikizo ya madeni yanatesa wananchi

Waziri wa Biashara na Viwanda, Dk Abdallah Kigoda
Muktasari:
Hali kama hiyo ya kukopa mazao ya wakulima na kushindwa kulipa, pia imewakumba wakulima wa mazao mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na pamba, korosho na tumbaku.
Tumesikitishwa na taarifa kwamba wakulima wa mahindi mkoani Ruvuma wanaidai Serikali zaidi ya Sh22 bilioni, hali inayowafanya kuishi katika umaskini na ufukara. Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu aliielezea hali hiyo ya kusikitisha hivi karibuni wakati wa kikao kati ya Waziri wa Biashara na Viwanda, Dk Abdallah Kigoda na wafanyabiashara mkoani humo kilichofanyika mjini Songea. Katika kuonyesha ukubwa wa tatizo hilo, mkuu huyo wa mkoa alisema asilimia 50 ya mahindi ya wakulima yaliyouzwa kwa Kitengo cha Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA), hayajalipwa na Serikali.
Katika kikao hicho, Waziri Kigoda alielezwa na wafanyabiashara hao kwamba kitendo cha Serikali kutolipa fedha hizo kimesababisha wakulima washindwe kujiandaa mapema kwa ajili ya msimu ujao, ikiwa ni pamoja na kununua pembejeo, huku wawakilishi wa wakulima wa mahindi wakimweleza waziri huyo kwamba kitendo cha Serikali kutolipa deni hilo, siyo tu kumesababisha washindwe kununua pembejeo, bali pia kulipa ada za shule kwa watoto wao. Walisema hali yao ni ngumu kwa kuwa waliwekeza fedha nyingi katika kilimo cha mahindi na wanajiuliza sababu za Serikali kushindwa kulipa mahindi iliyokopa. Hali kama hiyo ya kukopa mazao ya wakulima na kushindwa kulipa, pia imewakumba wakulima wa mazao mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na pamba, korosho na tumbaku.
Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukiitahadharisha Serikali kuhusu madhara yatakayotokea kwa nchi yetu kutokana na kutolipa madeni. Ni jambo la kusikitisha kwamba Serikali siyo tu inadaiwa kila kona ya nchi, bali pia na mataifa ya kigeni. Siyo siri kwamba dunia sasa inajua kwamba Serikali yetu imelimbikiza madeni na kujikuta ikidaiwa madeni mengi ambayo sasa inaonekana haina uwezo wa kuyalipa. Kwa mfano, Serikali kwa muda mrefu sasa imekuwa ikichukua ardhi ya wakulima katika sehemu mbalimbali nchini bila ridhaa yao wala kuwalipa fidia, pia ikishindwa kuwalipa makandarasi wa miundombinu na wanaotoa huduma mbalimbali katika taasisi za Serikali, kama Magereza na hospitali.
Inashangaza kuona kwamba katika baadhi ya sekta, fedha za kulipa madeni zimekuwa zikitengwa katika bajeti za kila mwaka, lakini ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) zimekuwa zikionyesha kila mwaka kuwa fedha hizo zimekuwa zikitafunwa au kutumika kwa shughuli nyingine ambazo hazikukusudiwa na hata hazikuwamo kwenye bajeti.
Sisi tunadhani tatizo la madeni limesababishwa na Serikali kuibuka na mipango mipya kila kukicha ambayo haimo katika bajeti wala mpango wa maendeleo wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa bajeti ya mwaka 2014/15, deni la Taifa lilipanda kwa haraka kutoka Sh23.67 trilioni mwaka 2013 hadi Sh30.56 trilioni mwaka jana. Deni la Taifa linajumuisha Deni la Nje na Deni la Ndani. Hili ni ongezeko la kutisha na linamaanisha kuwa matumizi yanakuwa ni makubwa kuliko mapato.
Pamoja na ukubwa wa deni hilo, katika bajeti ya mwaka 2013/14, Serikali ililipa Deni la Ndani kwa Sh1.6 trilioni tu, huku riba ikichukua karibu theluthi moja ya fedha hizo. Pia, katika kipindi hicho, Serikali ililipa Deni la Nje kwa Sh340 bilioni tu.
Malimbikizo ya madeni hayo ni kusababisha Serikali kupoteza fedha nyingi zinazotokana na riba, lakini kibaya zaidi kunaumiza wananchi. Serikali haina budi kuchukua hatua za dhati kurekebisha hali hiyo.