Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hizi hapa njia za kupiga pesa kupitia hatifungani

Hatifungani ni mojawapo ya njia salama za uwekezaji zinazoweza kumhakikishia mwekezaji mapato ya uhakika. Licha ya kuwa njia ya kuhifadhi mtaji, hatifungani zinaweza pia kutumika kwa mbinu mbalimbali ili kuongeza kipato. Hapa kuna njia kuu nne za kufanikisha hilo:

1. Fursa za tofauti ya bei

Manufaa yatokanayo na tofauti ya bei (Arbitrage) ni mbinu ya kupata faida kutokana na tofauti za bei au riba kwenye masoko tofauti. Mwekezaji anaweza kupata faida bila kujihatarisha kwa kununua hatifungani kutoka Benki Kuu ya Tanzania na kuuza katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa bei yenye faida.

Njia nyingine ya kupata kipato ni kwa kuchukua mkopo wenye riba ya chini na kutumia fedha hizo kununua hatifungani zinazotoa riba ya juu. Kwa mfano, Vanessa anaweza kukopa kutoka SACCOS kwa riba ya asilimia 8 kwa mwaka kwa mfumo wa ‘Reducing Balance’, kisha kutumia mkopo huo kununua hatifungani za serikali za muda mrefu zinazotoa riba ya asilimia 15 kwa mwaka.

Kwa kuzingatia kuwa riba ya asilimia 8 kwa mfumo wa Reducing Balance inalingana na takriban asilimia 4.27 kwa mfumo wa Flat Rate, Vanessa ataweza kupata faida ya nyongeza ya asilimia 10.98 kutoka kwenye uwekezaji wake baada ya kulipa mkopo. Kwa njia hii, mwekezaji anaweza kujenga chanzo cha kipato cha kudumu kwa maandalizi ya kustaafu.

2. Kutumia hatifungani kama dhamana ya mikopo

Hatifungani zinaweza kutumika kama dhamana ya mikopo kwenye benki na taasisi za kifedha. Wawekezaji wanaweza kutumia dhamana hii kukopa fedha za kuanzisha biashara, kununua mali kama magari na nyumba, au hata kugharimia mahitaji ya kifamilia kama ada za shule.

Kwa kuwa mapato ya hatifungani ni ya uhakika, mwekezaji anaweza kulipa mkopo kwa kutumia riba anayopata kutoka kwenye hatifungani. Baada ya kulipa mkopo, hatifungani husalia kama chanzo cha mapato kinachoendelea kuingiza fedha kwa mwekezaji bila kuhitaji juhudi zaidi.

3. Kipato cha uhakika (Passive Income)

Hatifungani za muda mrefu zinaweza kukuwezesha kupata kipato cha uhakika kwa muda mrefu. Riba ya hatifungani hulipwa mara mbili kwa mwaka, yaani kila baada ya miezi sita. Mwekezaji anaweza kununua hatifungani zenye tarehe tofauti za malipo ili kuhakikisha anapata mapato kila mwezi.

Kwa mfano, kama mtu atanunua hatifungani sita zenye miezi tofauti ya malipo, ataweza kupokea mapato ya kila mwezi, jambo ambalo linaweza kusaidia kugharimia mahitaji ya kila siku kama vile kodi ya nyumba, ada za shule, au gharama za matibabu.

4. Kutumia mapato ya hatifungani kufunika gharama za kudumu

Kwa kuwa hatifungani hutoa mapato ya mara kwa mara, zinaweza kutumika kama chanzo cha fedha cha kufidia gharama za muda mrefu. Kwa mfano, mapato ya kila baada ya miezi sita yanaweza kutumika kulipia kodi ya nyumba, ada za shule, au hata bima ya afya.

Njia hii inampa mwekezaji uhakika wa kifedha kwa muda mrefu, kwani anajua kuwa sehemu ya gharama zake za msingi zitalipwa kupitia mapato ya hatifungani. Pia, inampunguzia utegemezi wa vyanzo vingine vya mapato ambavyo vinaweza kuwa na mabadiliko ya ghafla.

Kwa kutumia mbinu hizi, wawekezaji wanaweza kuhakikisha kuwa uwekezaji wao katika hatifungani hauwapi tu faida ya mtaji, lakini pia unazalisha kipato endelevu kwa maisha yao ya baadaye.