Dk Mwigulu atangaza kiama wakwepa kodi

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, akizungumza bungeni jijini Dodoma leo.
Muktasari:
- Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji, ameliomba Bunge kuidhinisha Sh110.8 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025.Kati ya fedha hizo, Sh81.1 bilioni ni matumizi ya kawaida na Sh29.9 bilioni ni matumizi ya maendeleo. Bunge limepitisha fedha hizo.
Dodoma. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ametoa msimamo mkali kwenye ukusanyaji wa kodi unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwamba wanaokkwepa kodi ni wezi kama wezi wengine.
Mwigulu amesema hayo leo Jumatano, Mei 22, 2024 wakati akijibu hoja za wabunge zilizojitokeza wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara yaliyowasilishwa bungeni na Dk Ashatu Kijaji, aliyeliomba Bunge kuidhinisha Sh110.8 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kati ya fedha hizo, Sh81.1 bilioni ni matumizi ya kawaida na Sh29.9 bilioni ni matumizi ya maendeleo. Bunge limepitisha fedha hizo.
Hoja ya malalamiko ya kodi ilitolewa na wabunge kadhaa akiwamo mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei ambaye alidai TRA imekiuka agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la ukomo wa miaka mitatu wa kufanya tathmini wa hesabu zinazodaiwa kampuni za kibiashara.
Amesema bado wapo wawekezaji wazawa wanapata changamoto ya kutakiwa kukaguliwa na TRA hesabu za miaka ya nyuma licha ya kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aliweka ukomo.
“Wanalalamika kwa mfano Rais Samia aliweka ukomo wa TRA kukagua au kutathmini mahesabu ya kampuni ili kuona kama zililipa kodi zao sawa sawa, lakini bado wanakwenda wanataka hesabu za miaka mitatu kwa kisingizio cha tathmini… ule ukomo haufanyi kazi halafu ule ukomo haujawekwa katika walaka ambao ungeweza kutekelezeka na TRA,” amesema.
Hata hivyo, Dk Mwigulu ametoa ufafanuzi kuhusu makundi ya walipa kodi wakiwamo wafanyakazi ambao wanakatwa kwenye mishahara yao, na ulipaji wao hauna malalamiko tofauti na wafanyabiashara wakubwa na kundi la wanaokusanya kodi kwa niaba ya Serikali waliosajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
“Kundi la walipa kodi wakubwa na kundi wanaokusanya kodi kwa niaba ya Serikali waliosajiliwa VAT, kodi si ya kwake, si yeye anayelipa, yeye anatumika kama mkusanyaji wa kodi ya Serikali.
“Sasa inatokea mtu ambaye amekusanya kodi ya Serikali anatakiwa aiwasilishe siyo yeye aliyelipa, amekusanya kodi za walipa kodi wengine.
“Yeye amekusanya kama wakala wa kukusanya anatakiwa aiwasilishe serikalini…Inatokea mwaka wa tatu hajawasilisha, ametumia kodi ya walipa kodi wengine.
“Kaichukua anatembea anaonekana tajiri kumbe kachukua kodi ambayo walipa kodi wamelipa, watu wa aina hii hata ipite miaka mingapi huyu ni mwizi kama mwizi mwingine.
“Na mimi nikiwa Waziri wa Fedha hawa lazima walipe kodi ili watoto wa masikini waweze kusoma hatuwaacha kwa sababu imepita miaka.
“Mtu ambaye amekusanya kodi kwa niaba ya Serikali anatakiwa aiwasilishe kodi hiyo serikalini hii haina mwezi, haina mwaka anatakiwa aiwasilishe kodi serikalini. Na hata Rais aliposema akiwa Kagera alikuwa anongelea hawa walipa kodi wadogo wadogo ambao hawajui hata kutunza takwimu,” amesema Mwigulu.
Mwigulu amesema sheria inasema mtu yeyote akikusanya kodi ya Serikali anatakiwa aifikishe serikalini.
Naye Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema wizara yake imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kuzalisha viwanda vidogo vya wajasiliamali.
Pia, amesema hoja viwanda vya chai kufungwa nchini, ni changamoto ya dunia, na kwamba Serikali inachukua hatua ambapo kati ya viwanda 24 vilivyopo nchini viwanda saba vimefungwa.
“Viwanda saba kati ya hivyo, vitatu ni vya Mohammed Enterprises (Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL), viwili ni vya DL Group na kimoja tunakifungua,” amesema.
Pia, alisema siyo sahihi kuamini kwamba wakulima wadogo hawawezi kuendesha viwanda na kwamba kuna mkulima ambaye anamiliki kiwanda cha chai na Serikali imeendelea kumsaindia awe na kiwanda kikubwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema wizara yake imeendelea kushirikiana na wafanyabishara na kwamba kuhusu TRA wanapokwenda kudai kodi huwa wanampigia simu, hata ikiwa ni kwenye soko la Kariakoo.
Amesema wizara yake kwenye mwaka ujao wa fedha, imedhamiria kuwa na mtaa wa viwanda kila wilaya kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali wadogo.