Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Daraja la JPM litakavyofungua uchumi wa Kanda ya Ziwa

Mradi wa ujenzi wa Daraja la JPM maarufu kama Kigongo-Busisi unaotarajiwa kukamilika Februari 2025, unatoa matumaini mapya kwa wakazi na wafanyabiashara wa Kanda ya Ziwa, kama inavyoelezwa na wakazi hao.

“Nikitoka kuchukua mizigo Mwanza nikapita Kigongo – Busisi wakati mwingine nakaa hadi saa tatu kabla sijavuka maana watu wa malori hatupewi kipaumbele na ikitokea ukaja msafara hali inakuwa mbaya zaidi, hata saa tano zinakatika,” anasema Geofrey Joel ambaye ni dereva wa lori.

Anasema kujenga daraja katika eneo hilo kutaongeza urahisi katika shughuli tofauti hususani za uchukuzi kati ya Mwanza na maeneo mengine ambayo yameunganishwa na jiji hilo la pili kwa ukubwa nchini.

Ukiachia mbali Joel, kwa wakazi na wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, kukamilika daraja la JPM maarufu kama Kigongo-Busisi linalokatiza kwenye Ziwa Victoria, si tu litapunguza muda wa kuvuka kwa dakika 40, bali ni mwanzo mpya wa kuimarika kwa uchumi wa eneo hilo la pili kiuchumi nchini.

Wengi wanasubiri kwa hamu urahisi wa kuvuka kutoka eneo la Kigongo, Wilaya ya Misungwi kwenda Busisi Wilaya ya Sengerema ambako watavuka kwa dakika tano kutoka dakika 45 hadi saa moja walizokuwa wanatumia kuvuka awali kwa kutumia vivuko vya Mv Mwanza na Mv Misungwi. Waenda kwa miguu watatumia dakika 15.

Mradi huo unaotekelezwa na mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Bureau Group Corporation kwa gharama ya Sh716.33 bilioni ulianza Februari 25, 2020 na unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika Desemba, 2024.

Zaidi ya Sh699.3 bilioni za mradi huo ni gharama za mkandarasi wakati mwandisi mshauri analipwa Sh11.1 bilioni, Sh3.14 bilioni zimetumika kuwalipa fidia wananchi kupisha eneo la mradi huku Sh2.8 bilioni zilitumika kufanya usanifu wa mradi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyekuwa anatoa taarifa fupi ya ulipofikia ujenzi huo kwa Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 13, mwaka huu, ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 93 na litaanza kutumika Februari 2025.

 "Kilomita zote tatu zimekamilika ... kazi iliyobaki kwa sasa ni kuliweka daraja katika ubora na viwango vya kimataifa kwa maana ya kusafisha mavyuma yaliyopo na kuanza kuweka demarcations (kingo) za upande wa kwenda na kurudi ... kwa hiyo tukuhakikishie itakapofika mwakani mwezi wa pili daraja lote litakuwa limekamilika na tayari kwa matumizi ya wananchi," alisema Bashungwa.


Sifa za daraja la JPM

Daraja hilo litakapokamilika, litakuwa refu kuliko yote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, litakuwa na njia mbili za magari zenye upana wa mita saba kila upande, njia ya waenda kwa miguu yenye upana wa mita 2.5 kila upande, maegesho ya dharura yenye upana wa mita 2.5 kila upande na njia ya waenda kwa miguu yenye upana wa mita 2.5.

Daraja la JPM litakuwa la sita kwa urefu katika Bara la Afrika likiwa na urefu wa kilomita 3, upana wa mita 28.45 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66.

Kwenye daraja hilo lililopewa jina la JPM kama sehemu ya kutambua, kuenzi na kumbukumbu Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli aliyeasisi wazo na kuanza utekelezaji wa mradi huo aliouacha kwa asilimia 25 ya ujenzi, kuna nguzo za msingi 804, vitako vya nguzo za madaraja 65, nguzo 64 na nguzo za mlalo 806.

Usanifu wa daraja hilo uliotumia teknolojia ya madaraja marefu (Long Span Bridges), inayoitwa ‘Extra Dosed Bridge’ ambapo kutakuwa na nguzo Kuu (Pylons) tatu zenye kimo cha mita 40 na umbali mita 160 kutoka nguzo moja hadi nyingine.

Kwenye hizo nguzo 64, mbili kati ya hizo zitakuwa umbali wa mita 100 kutoka nguzo moja hadi nguzo kuu wakati zilizobaki zitakuwa umbali wa mita 40 kutoka nguzo moja hadi nyingine na kwenye kila nguzo ya daraja kuna nguzo za msingi (pile foundations) zilizochimbiwa ardhini kwa urefu wa kati ya mita 11.5 na mita 66.

Kwa lugha nyingine, daraja hilo lina upenyo mita 120 kati ya nguzo zake kuu kuruhusu meli na vyombo vingine vya usafirishaji majini kupita na hivyo kuwa daraja lenye upenyo mkubwa zaidi nchini kulinganisha na daraja la Tanzanite na Kigamboni ya jijini Dar es Salaam.


Manufaa ya kiuchumi

Kijiografia, daraja la JPM limejengwa katika eneo la ushoroba wa Ziwa Victoria kuanzia mpaka wa Sirari Wilaya ya Tarime mpakani na nchi ya Kenya hadi mpaka wa Mtukula Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera inayopakana na nchi ya Uganda; na mpaka wa Rusumo na Kabanga Wilaya ya Ngara inayopakana na nchi jirani za Rwanda na Burundi.

Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassani, ujenzi wa daraja hilo siyo tu umewapatia Watanzania ajira bali hata baada ya kukamilika litaendelea kutoa ajira kwa kuwa pale linapojengwa ndipo kilipo kituo kikubwa cha magari yanayokwenda nje ya nchi na yanayokwenda pande mbalimbali za Tanzania.

"Nimetoka kuliangalia daraja, lipo asilimia 93 bado kidogo mwezi wa pili mwakani nakuja kulifungua ... magari yanapita, mnafanya kazi zenu, biashara zinaenda ... hakuna kilichosimama," alisema Rais Samia Oktoba 13, 2024 wakati akiwasalimia wakazi wa Kigongo mara baada ya kulikagua daraja hilo.

Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Paschal Ambrose alisema kukamilika kwa ujenzi wa daraja la JPM kuna faida ikiwemo ongezeko la shughuli za kiuchumi ndani na nje ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, Tanzania kwa ujumla na nchi jirani za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Tunajenga daraja hilo kwa lengo la kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla kwanza litapunguza muda wa kusafiri ambapo muda utakuwa anavuka ndani ya dakika tano yuko upande wa pili … Kama mtu atafika mapema mahali alikokuwa anataka kufika ina maana itachochea uchumi kwa sababu atafanya biashara mapema,” anasema Ambrose

Anaongeza kuwa, “Pia itachochea kukua na ongezeko la biashara nchini, watu kutoka nje ya nchi watakuja kununua vitu hapa kwa sababu reli ya SGR ikikamilika kutakuwa na bandari katika eneo lile ambapo mizigo itakuwa inatoka Dar es Salaam mpaka hapo kwenye bandari hivyo watu kutoka Burundi, Kenya, Uganda watakuwa wanachukulia hapo mizigo badala ya kwenda Dar es Salaam,”

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara kutoka jijini Mwanza, Donai Jersey anasema litakapokamilika daraja hilo litafanya urahisi wa usafirishaji wa bidhaa kwa wafanyabiashara, kukua kwa soko la biashara ya samaki na dagaa Kwa mikoa ya kanda ya ziwa na sekta ya madini kutangazika zaidi kwa nchi jirani kama Rwanda.

“Biashara kwa ujumla zitakua kwa sababu ya uhakika wa bidhaa kutoka Mwanza kwenye maduka ya jumla na kufika kwa uharaka sehemu kama Sengerema, Geita, Katoro, Nyarugusu na pia kuongezeka kwa uwekezaji katika eneo la majengo na makazi (real estate) mfano nyumba za kupangisha (apartment), hoteli na nyumba za kulala wageni (guest houses),” anasema Jersey

Mtaalamu wa Masuala ya Uchumi na Biashara, Dk Zakaria Jackson anasema litakapokamilika daraja hilo hata bei za bidhaa zitashuka bei kwa kuwa bidhaa zinazotoka ng’ambo kwenda kwa walaji wa mwisho zinakuwa na bei kubwa kutokana na gharama ya usafirishaji.

“Bidhaa nyingi zitakazokuwa zinaenda au kutoka sokoni kwenda kwa mlaji wa mwisho zimekuwa na bei kubwa kwa sababu ya usafirishaji hivyo tunatarajia kwamba hata bei za bidhaa zitapungua kutokana na gharama za usafiri kupungua,” anasema.

“Kukamilika kwake kutafungua wigo mpana wa watu kufanya biashara mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa sababu ni moja ya njia ambayo imekuwa ikitegemewa sana na wafanyabiashara ambao wanatoka mikoa jirani kama Kagera na Geita … Kwa hiyo faida ambazo tunazitarajia kama matokeo ya kukamilika Kigongo Busisi ni kutanua mawanda ya kibiashara kwa maana ya biashara zile ambazo zinaingia au kutoka Mwanza zitakua sana lakini pia tutegemee kuboreshwa kwa mnyororo wa thamani kwa sababu moja ya kigezo chake ni usafirishaji,”

Dk Jackson anasema faida za kiuchumi zitokanazo na daraja hilo pia ni mwingiliano wa watu kuja kufanya biashara ndani ya Kanda ya Ziwa na hasa Mwanza utakuwa mkubwa na kiuchumi kuna faida nyingi sana ambazo daraja hilo linaenda kuleta ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu kuongezeka.


Ujuzi kwa wakandarasi wa ndani

Kwa mujibu wa Ambrose, pamoja na manufaa kiuchumi, litakapokamilika daraja hilo pia wahandisi na mafundi wazawa wanaoshiriki kutekeleza mradi huo watapata ujuzi, maarifa na teknolojia mpya na kufanya Taifa kuwa na wataalamu kwenye sekta ya ujenzi wa madaraja.

Ujenzi huo unaotumika pia kama darasa kwa wataalamu wa ndani, umetoa zaidi ya ajira 29,211 tangu kuanza kwake ambapo asilimia 93.33 sawa na ajira 27,262 ni wazawa na ajira 1,949 sawa na asilimia 6.67 ni wageni.

Pia, wahandisi wahitimu 11 walioko chini ya mpango unaoratibiwa na Bodi ya Usajili Wahandisi nchini (ERB) nao wanashiriki utekelezaji wa mradi huo kwa lengo la kuwapa ujuzi na maarifa ya teknolojia mpya na ya kisasa utakaotumika katika miradi mbalimbali itakayotekelezwa nchini huku, wahandisi wanne kutoka Tanroads wakifanya kazi hapo muda wote kwa ajili ya kujifunza.


Mchango katika pato la Taifa

Kwa mwaka 2022 Kanda ya Ziwa ilichangia zaidi ya robo ya pato lote la nchini asilimia 25.9 kwenye patop la Taifa ikifuatiwa na kanda ya Kaskazini asilimia 17.2.

Kanda ya nyanda za juu kusini ilichangia asilimia 15.8 ya pato lote la Taifa, Kanda ya Kati asilimia 13.5 huku Kanda ya Kusini mashariki ikiwa na mchango mdogo zaidi wa asilimia 10.5.