Rais Samia kukagua daraja la JPM, Meli mpya ya Mv Mwanza

Muonekano wa daraja la JPM maarufu kama daraja la Kigongo-Busisi.
Muktasari:
Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa Kilometa 3.2 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66 ulianza Februari 25, 2020 na unatarajiwa kukamilika Februari 24, 2024 ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 75.
Mwanza. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anaendelea na ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Mwanza ambapo leo Juni 14, 2023 anatarajiwa kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja la JPM maarufu kama daraja la Kigongo-Busisi inayopita juu ya maji ya Ziwa Victoria.
Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa Kilometa 3.2 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66 ulianza Februari 25, 2020 na unatarajiwa kukamilika Februari 24, 2024 ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 75.
Kukamilika kwa daraja la Kigongo-Busisi kutapunguza muda wa kuvuka hadi dakika 5 kwa kutumia gari na dakika 15 kwa watembea kwa miguu kulinganisha na muda wa sasa wastani wa dakika 25 hadi 45 kwa kutumia kivuko.
Mradi mwingine unaotarajiwa kutembelewa na kukaguliwa na Mkuu huyo wa nchi leo ni ujenzi wa meli mpya ya Mv Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh109 bilioni.
Utekelezaji wa mradi ujenzi wa meli ya Mv Mwanza katika eneo la Bandari ya Mwanza Kusini ulioanza Januari, 2019 unatarajiwa kukamilika mwaka huu.
Meli hiyo ambayo ndio itakuwa kubwa kuliko zote Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ina kimo cha ghorofa nne ikiwa na urefu wa mita 92.6, upana wa mita 17 na uzito wa tani 3, 500 huku ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1, 200, magari 20 na tani 400 ya mizigo.
Rais Samia pia anatarajiwa kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa hotel ya kisasa jijini Mwanza unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Katika ziara yake iliyoanza Juni 12, 2023, Amiri Jeshi Mkuu huyo tayari amefanya kazi ya kuzindua tamasha la ngoma za asili za Jamii ya Kisukuma maaruu kama Bulabo linaloendelea katika makumbusho ya Bujora Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.
Uzinduzi huo uliofanyika jana Juni 13, 2023, ulimwezesha Rais Samia kurejea katika viwanja vya Red Cross eneo la Kisesa ambako ndiko Rais Samia alikosimikwa kuwa Chifu Mkuu wa Machifu Tanzania na kupewa jina la Chifu Hangaya katika hafla iliyofanyika Septemba 8, 2021.
Jina la Chifu Hangaya alilopewa Mkuu huyo wa nchi wakati wa hafla ya kusimikwa kushika wadhifa huo ina maana ya ‘’nyota angavu ya asubuhi yenye matumaini’’