Bosi CRDB Bank Foundation ang’ara tuzo Nigeria

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa
Muktasari:
- Aidha, Katika hafla hiyohiyo, Rais Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa tuzo ya Heshima ya Kipekee kwa Uongozi wa Kiwango cha Juu Barani Afrika (Imperial Honour for African Iconic Global Leadership of the Year).
Lagos. Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa, ametajwa kuwa Kiongozi anayeongoza kwa uwezeshaji Barani Afrika katika hafla ya tuzo za kutambua wanawake mashuhuri Afrika (African Iconic Women Recognition Awards).
Katika tukio hilo ambalo la kihistoria kwa Tanzania ambapo mbali ya Tully pia Rais Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa tuzo ya Heshima ya Kipekee kwa Uongozi wa Kiwango cha Juu Barani Afrika (Imperial Honour for African Iconic Global Leadership of the Year).
Heshima hiyo inakuja kwa Tanzania kwa kuwa wanawake viongozi wawili wametambuliwa kwa heshima za juu katika bara la Afrika siku moja. Huu ni ushahidi wa nguvu, ushawishi, na msukumo mkubwa wa wanawake wa Kitanzania katika jukwaa la kimataifa.
Tuzo ya Tully ni matokeo ya juhudi zake kubwa katika kuwawezesha wanawake na vijana kupitia programu jumuishi na bunifu za kifedha.
Uongozi wake ndani ya CRDB Bank Foundation umebadili maisha ya maelfu ya Watanzania, hususan wajasiriamali vijana na wanawake kupitia programu ya iMbeju, ambapo ndani ya mwaka mmoja tokea kuanzishwa kwake imefikia zaidi ya wanawake na vijana 800,000.
Programu ya iMbeju inatoa mafunzo ya ujasiriamali, ushauri, elimu ya fedha, na mitaji wezeshi.
Tully ana uzoefu wa zaidi ya miongo mitatu katika sekta ya benki, ambapo amehusika katika kubuni bidhaa na huduma bunifu zilizochangia kupanua wigo wa ujumuishi wa kifedha nchini. Kupitia CRDB Bank Foundation, anaendelea kuwa chachu ya matumaini na mabadiliko chanya katika jamii.
Tuzo hii imekuja katika kipindi cha kipekee ikiwa ni miaka 30 tangu Azimio la Beijing, mpango muhimu wa kihistoria wa kuendeleza haki na usawa wa wanawake duniani.
Pia, tuzo hii imekuja wakati Benki ya CRDB ikisherehekea miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ni taasisi ya kifedha inayozidi kuonesha dhamira ya dhati katika kuwawezesha wanawake.
Wakati dunia inatafakari mafanikio ya miaka 30 ya harakati za usawa wa kijinsia tangu Beijing, na wakati Benki ya CRDB ikisherehekea miongo mitatu ya huduma kwa Watanzania, tuzo ya Tully inakuwa alama hai ya mafanikio haya. Kazi yake inaakisi malengo ya Azimio la Beijing katika kuondoa vikwazo, kutoa fursa kwa wanawake, na kuinua jamii.
Tuzo hii pia inaipa Benki ya CRDB nafasi ya pekee ya kuwa miongoni mwa taasisi za kifedha barani Afrika ambazo haziegemei tu upande wa ujumuishwaji wa kifedha, bali pia zinakuwa mstari wa mbele katika kufanikisha usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.
Katika tuzo hii Tully ameibuka mshindi dhidi ya viongozi wengine wanawake mashuhuri barani Afrika ikiwamo Odunayo Sanya, Mkurugenzi Mkuu wa MTN Foundation, Balo Atta, ofisa Mtendaji Mkuu wa UBA Foundation), Osayi Alile Ofisa Mtendaji Mkuu wa Aspire Coronation Trust Foundation).
Somachi Chris-Asoluka, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tony Elumelu Foundation, na Claire Akamanzi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo Rwanda.
Ushindi wa Tully ni uthibitisho muhimu kuwa wanawake wana nafasi muhimu ya kubadili maisha na kuchochea maendeleo katika jamii na Taifa.