Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Benki ya Taifa ya Ushirika kuzinduliwa, kuanza na matawi manne

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Kilimo wakiwa katika mkutano wa kuelezea kuhusu uzinduzi wa Benki ya Taifa ya Ushirika.

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan atazindua rasmi Benki ya Taifa ya Ushirika ambayo inalenga kuondoa changamoto ya mifumo ya fedha kutoelewa soko na tabia za kilimo nchini.

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan atazindua rasmi Benki ya Taifa ya Ushirika ambayo inalenga kuondoa changamoto ya mifumo ya fedha kutoelewa soko na tabia za kilimo nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe leo Alhamisi Aprili 10, 2025 alipokuwa akizungumzia uzinduzi huo.

Bashe amesema changamoto kubwa inayokabili sekta ya kilimo ni mitaji na kuwa moja ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ilikuwa kuhakikisha inapatikana.

Amesema awali kuliwahi kuwapo Benki ya Ushirika ambayo sasa inajukana kama CRDB, lakini kutokana na mambo mengi ikiwemo ushirika kufilisika ilitetereka.

Bashe amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita benki nyingi zilifilisika zikiwemo za ushirika na baada ya maelekezo ya Rais Samia mchakato wa kuianzisha ulianza.

“Jambo hilo limefanikiwa Aprili 28,2025 Rais Samia atakuwa anaizindua na  itaanza na matawi manne, lakini vyama vikuu vya ushirika vyote vitakuwa ni mawakala wa benki,” amesema Waziri Bashe.

Amefafanua kuwa vyama vikuu vya ushirika vyote vitakuwa na kazi za kufungua akaunti, kuweka na kutoa fedha na hayo yote yatafanyika kwa mujibu wa sheria za benki kuu.


Amesema wakulima wamekuwa wakiingiza mapato mengi nchini, lakini likija suala la uwezeshaji, mifumo ya fedha haielewi soko wala tabia za kilimo.

Hivyo Waziri Bashe amesema ni muhimu kuwa na chombo cha fedha kinachowaelewa wakulima.

Amesema vyama vikuu vya ushirika pamoja na vya Kuweka na Kukopa (Saccos) na vile vya Msingi (Amcos) vinamiliki asilimia 51 ya benki hiyo na asilimia 49 zinamilikiwa na wadau wengine.

Waziri Bashe amesema makao makuu jengo la ushirika huo yatakuwa Dodoma huku ikianza na matawi manne ya Mtwara, Kilimanjaro, Tabora na Dodoma huku awamu ya pili ikiwa ni Kagera, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Katavi.

“Hii ilikuwa ndoto ya  Rais Samia kuona uwezeshaji unakuwa, haianzishwi kwa nia ya kuuwa benki ya biashara. Itazinduliwa ikiwa na mtaji wa Sh55 bilioni,”amesema.

Bashe amesema wanunuzi wote wa mazao makubwa ikiwemo ya kahawa, tumbaku na korosho hatapewa leseni kama hawana akaunti katika benki hiyo.

Mkulima kutoka Kongwa, Arodia Aizack amesema benki hiyo ni muhimu kwa wakulima wadogo ambao walikuwa wakikosa mikopo kutoka taasisi za fedha kutokana na kukosa dhamana.

“Labda sasa tutakomboka, maana benki nyingi zilikuwa zinatukimbia, huenda sasa tutapata na sisi mikopo kama wengine,” amesema Aizack.