Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Biteko ainadi sekta ya nishati Russia

Muktasari:

  • Katika mkutano huo amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Urusi kuongeza uwekezaji nchini hususan katika nishati safi ya kupikia, ambapo ameelezea uwepo wa fursa za uwekezaji wa sekta binafsi za uzalishaji umeme wa kujitegemea na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dk Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati wa Russia,  Sergey Tsivilev kuhusu kuimarisha ushirikiano katika sekta ya nishati na maeneo mengine muhimu ikiwemo teknolojia na uwekezaji.

Mazungumzo hayo kati ya Dk Biteko na Tsivilev yamefanyika kando ya Jukwaa la Kimataifa la Uchumi St. Petersburg nchini Russia.

Kupitia mkutano huo, Dk Biteko amesema kiwango cha uwekezaji nchini kutoka Russia kinafikia dola za Marekani milioni 424 kupitia miradi 44 iliyoajiri watu zaidi ya 3,000, huku akielezea fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya nishati.

"Tanzania ina asilimia 61.7 ya nishati kutoka vyanzo vinavyoweza kurejeshwa na fursa za uwekezaji zenye thamani ya dola bilioni 4 katika sekta ya nishati," amesema Dk Biteko.

Ametaja jitihada za Serikali katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya nishati sambamba na kushirikisha sekta binafsi kwenye utekelezaji wa miradi ya pamoja.

Jitihada nyingine ni  kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia akitolea mfano Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika Dar es Salaam Januari, 2025 uliolenga kutoa umeme kwa Waafrika milioni 600 ambao hawana nishati hiyo muhimu.

Pia, Dk Biteko amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Russia kuongeza uwekezaji nchini, hususan katika nishati safi ya kupikia ambapo ameelezea uwepo wa fursa za uwekezaji wa sekta binafsi za uzalishaji umeme wa kujitegemea na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Katika mazungumzo hayo amesema  uhusiano wa kidiplomasia wa takriban miaka 64 kati ya Tanzania na Russia unalenga kunufaisha wananchi wa nchi hizo.

Kwa upande wake, Waziri Tsivilev amesema kuwa Russia ipo tayari kusaidia teknolojia na kujengea uwezo wataalamu wa Afrika Tanzania ikiwamo,  ili kuhakikisha uhuru wa teknolojia unakuwepo.

 Waziri huyo amezungumzia umuhimu wa nishati katika maendeleo ya kiuchumi hususan katika masuala ya usalama wa nishati, upatikanaji, bei nafuu na ufanisi.

"Russia ina mkakati wa haki katika ushirikiano na malengo ya kuendeleza mifumo ya nchi kwa washirika wa muda mrefu. Tuko tayari kusaidia maeneo mbalimbali ikiwemo afya, usalama wa mtandao na ulinzi wa miundombinu muhimu, " amesema Tsivilev.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INTER RAO Export, ambayo ni moja ya kampuni kubwa zaidi ya nishati duniani, Maxim Sergeev licha ya kuonesha nia ya kuwekeza nchini amesema kuwa ina uwezo wa kutengeneza vifaa mbalimbali ikiwemo mashine umba na jenereta, pia ina mikataba ya kila mwaka inayofikia dola bilioni nane.

Aidha, mazungumzo hayo kati ya Dk Biteko na Tsivilev yamehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania Moscow, Frederick Kibuta, Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Petroli, Mhandisi Marwa Petro.

Kando ya mazungumzo hayo naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania Tanesco, Lazaro Twange amefanya mazungumzo na Kampuni ya Rosatom na Unigreen kuhusu ushirikiano wa uzalishaji wa umeme unaotokana na urani pamoja na jua, ambapo Unigreen inaendelea na taratibu za uwekezaji nchini.