Bei ya petroli yashuka, dizeli ikiongezeka

Muktasari:

  • Bei ya petroli inayoingia katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara imepungua Julai ikilinganishwa na Juni

Dar es Salaam. Bei ya petroli ya rejareja kwa Julai imeshuka katika mikoa inayochukua mafuta hayo bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ikilinganishwa na Juni, huku dizeli ikiongezeka kidogo.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha bei za mafuta kuanzia leo Jumatano Julai 3, 2024 kwa yanayochukuliwa Bandari ya Dar es Salaam, petroli imeshuka kwa Sh51 kwa lita na kuwa Sh3,210, huku dizeli ikiongezeka kidogo kwa Sh3 kutoka Sh3,112 hadi Sh3,115 katika mkoa huo.

Kwa petroli inayochukuliwan katika Bandari ya Tanga, bidhaa hiyo imeshuka kutoka Sh3,263 Juni hadi Sh3,210 Julai na kwa Bandari ya Mtwara imepata ahueni kutoka Sh3,267 hadi Sh3,212 katika kipindi sawa na hicho.

Hata hivyo, dizeli inayopokewa katika Bandari ya Tanga imeongezeka kutoka Sh3,121 Juni hadi Sh3,124 Julai, pia kwa Bandari ya Mtwara imeongezeka kutoka Sh3,122 hadi Sh3,124 katika kipindi kama hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule kupitia taarifa kwa umma amesema miongoni mwa sababu za kupungua bei ya bidhaa hiyo ni kupungua kwa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB).

“Mabadiliko ya bei za mafuta kwa Julai 2024 yamechangiwa na kupungua bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 5.92 kwa mafuta ya petroli na asilimia 0.65 kwa mafuta ya dizeli,” amesema.

Sababu nyingine amesema ni kuongezeka kwa wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa asilimia 0.6, kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa mafuta (premiums) kwa wastani wa asilimia 1.6 kwa petroli na asilimia 3.35 kwa dizeli katika Bandari ya Dar es Salaam.

Dk Mwainyekule amesema sababu nyingine ni kupungua kwa gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 11.75 kwa petroli na asilimia 11.75 kwa dizeli katika Bandari ya Tanga, na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 11.25 kwa mafuta ya petroli na asilimia 11.22 kwa dizeli katika Bandari ya Mtwara.

Kwa upande mwingine, katika mwezi huu petroli itanunuliwa kwa bei ya juu eneo la Kyerwa mkoani Kagera kwa Sh3,448.