Bei ya mchele Mbeya yapaa, Serikali yafafanua

Muktasari:
- Bei ya mchele mkoani Mbeya imeonekana kupanda huku ukame ukitajwa kuathiri zao hilo na kuhofiwa uzalishaji wake kupungua.
Mbeya. Wakati bei ya mchele ikipanda mkoani Mbeya, wakulima wa zao hilo wamesema huenda bidhaa hiyo ikazidi kupanda kutokana na ukame wa mvua msimu huu.
Kwa sasa bei ya zao hilo ipo juu ambapo ndoo ya kilo 20 imefikia kati ya Sh60,000 hadi Sh65,000 kutokana na ubora sokoni, hali inayotia hofu kwa wananchi haswa wenye kipato cha chini ikilinganishwa na awali ilipouzwa kati ya Sh30,000 hadi Sh 45,000.
Mchele ni moja ya chakula na zao kubwa jijini Mbeya, licha ya uwapo wa uzalishaji wa vyakula vingine ikiwamo ndizi aina zote, mihogo, viazi aina zote na mahindi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi leo Aprili 9,2025 baadhi ya wakulima wilaya za Mbarali na Kyela wamesema kuwa hali ya uzalishaji wa zao hilo kwa sasa imepungua kutokana na kukosa mvua za kutosha na kwa wakati.
Modestus Kilufi mkulima wa zao hilo Wilaya ya Mbarali mkoani humo, amesema mvua ndogo na ukame wa baadhi ya maeneo umefanya uzalishaji kupungua.
Amesema kilimo katika baadhi ya maeneo wilayani humo hutogemea maji yanayotoka kwenye milima ya Makete tofauti na matarajio yao na kwamba huenda bei ya mchele ikazidi kupanda.
"Mvua imekuwa ndogo sana imepunguza uzalishaji, sioni bei ikishuka, inaweza kupaa zaidi, kilimo chetu tunahitaji mvua ya kutosha na kwa wakati" amesema Kilufi.
Naye Christian Lwoga amesema msimu huu mashamba yamekumbwa na ukame kutokana na mvua kupungua na kwamba si zao la mpunga pekee bali hata mahindi yameharibika.
Amesema wakulima wengi walitarajia mavuno mengi, lakini kwa sasa wanasubiri litakalokuwa na liwe akieleza kuwa wanajipanga na msimu ujao wa kilimo kujua hali itakavyokuwa.
"Mavuno ya msimu huu yatakuwa kidogo mno, kuna sehemu nyingine huko Rukwa mvua ni kubwa imeharibu mpunga, huku kwetu ni ukame hadi kwenye mahindi, uhalisia lazima bei izidi kupaa" amesema Lwoga.
Kwa upande wake Rose Mpande amesema mabadiliko ya bei yanasababishwa na mambo mengi ikiwamo kuadimika kwa bidhaa yenyewe akieleza kuwa mchele umepanda bei.
"Mchele wa kawaida mashineni Sh45,000 hadi Sh50,000, ule kiwango cha juu zaidi ya Sh55,000 ila inategemea na maeneo ya mzigo ulipo, hata hivyo kwa sasa tunaona imepungua bei " amesema Rose.
Mkulima Erasto Mwonga wa wilayani Kyela amesema pamoja na bei hiyo kudaiwa kupanda, wananchi wasiangalie zaidi upande wao badala yake waangalie pia gharama za kilimo kwa mkulima kuanzia maandalizi ya shamba hadi mavuno.
"Tunatumia gharama kubwa pia sisi wakulima kuanzia kupata shamba, maandalizi, mbegu, mbolea, vibarua hadi kuvuna, hivyo bei kupanda isishangaze sana bali tuangalie na nguvu ya uzalishaji " amesema Mwonga.
Naye Willy Martin mkulima amesema mvua za msimu huu zimekuwa ndogo, “bei ya mchele lazima iongezeke kwa kuwa kinachopandwa na kinachovunwa ni tofauti akieleza kuwa wananchi wasiweke hofu kwa kuwa ni mambo ambayo hutokea kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
"Kilo inaweza kufika hadi Sh2,700 kutokana na ubora wake, mvua zimekuwa chache sana huku Kyela kipindi cha nyuma, kwa sasa inaweza kunyesha nyakati za usiku utakuta zimeharibu sana kwa kuwa hakuna usimamizi" amesema Martin.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Florah Luhala amesema kwa sasa mvua zipo na mazao yanastawi vyema japokuwa bei ya mchele kupanda ni suala la kawaida kutokana na msimu wa mavuno kuwa bado.
Amesema si Kyela pekee bali hata maeneo mengine bei ya zao hilo ipo juu kwa kuwa kwa sasa mzigo uliopo sokoni ni wa zamani, hivyo huenda ikashuka msimu wa mavuno ukianza.
"Mvua imepotea nyuma ikaathiri baadhi ya wakulima, lakini kwa sasa hali ni shwari na hii bei ni kwa mchele wa zamani, ila mavuno yakianza inaweza kupungua na suala hili lipo maeneo mengi kwa kuwa mvua ilipungua nyuma" amesema Frolah.