Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mchele fursa mpya kimataifa, hapa nchini bei ikizidi kupaa

Muktasari:

Huenda kwa sasa mchele ukawa ni chanzo kingine cha mapato kwa nchi, ikiwa nguvu kubwa zitaelekezwa katika uzalishaji wake badala ya mazao ya asili yaliyozoeleka.

Dar es Salaam. Huenda kwa sasa mchele ukawa ni chanzo kingine cha mapato kwa nchi, ikiwa nguvu kubwa zitaelekezwa katika uzalishaji wake badala ya mazao ya asili yaliyozoeleka.

Hali hiyo ni baada ya mchele pekee kuliingizia Taifa karibu nusu ya mapato yaliyopatikana katika mazao aina saba ambayo Taifa limezoea kuuza kwa miaka mingi.

Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya Uchumi ya Taifa ya mwaka 2021 iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, mchele uliingiza Dola 301.9 milioni (zaidi ya Sh692.3 bilioni) katika mwaka 2021, huku mazao saba asilia yaliyozeleka yakiingiza dola 627.9 milioni za Marekani (zaidi ya Sh1.442 trilioni).

Mazao ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakitumika kama chanzo cha fedha za kigeni kwa nchi ni kahawa, pamba, katani, chai, tumbaku, korosho na karafuu.

Lakini kati ya mwaka 2019, 2020 hadi mwaka 2021 mapato yanayopatikana katika bidhaa hizo asilia yamekuwa yakishuka mfululizo kutoka dola 817.7 milioni za Marekani, Dola 808.1 milioni za Marekani hadi Dola 627.9 milioni za Marekani katika mtiririko wa awali.

Mwaka mmoja pekee ulitosha kuufanya mchele kung’ara na kuleta mapato mengi kwa nchini kutoka dola 143.7 milioni za Marekani (zaidi ya Sh328.9 bilioni) mwaka 2020 na kufikia zaidi ya Sh692.3 bilioni mwaka 2021.

Wakati mauzo yakipanda, uzalishaji wa mchele kati ya mwaka 2020 hadi mwaka 2021 ulishuka kwa asilimia 11.5 kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Takwimu zinaonyesha, tani 3.038 milioni za mchele zilizalishwa mwaka 2020 kiwango ambacho kilipungua hadi tani 2.688 milioni mwaka 2021.

Jambo hilo huenda likawa limechangia ongezeko la bei ya mchele nchini kwani zimekuwa zikitofautiana kati ya eneo na eneo. Tofauti na zamani ambapo mtu aliweza kupata mchele mzuri kwa Sh2000 sasa hali ni tofauti kwani bei hiyo ni kwa mchele ambao wakati mwingine uliuzwa hadi Sh1400 ndani ya jiji la Dar es Salaam.

“Mchele haushikiki, bei yake imepanda sana, kuna wakati tulikuwa tukiuza mchele mzuri kwa Sh2000 na bei kubwa Sh2,300 hivi sasa mchele mzuri ambao mtu huweza kuridhika ni kuanzia Sh3,000,” alisema Juma Khamis muuzaji wa mchele katika soko la Kisutu Dar es Salaam.

Mikoa ambayo inaonesha kuwa na uzalishaji mkubwa ni Morogoro, Mbeya, Tabora, Arusha, Tabora, Mwanza, Katavi, Simiyu na Ruvuma ambako wakulima na wafanyabiashara wamekuwa wakiwekeza huko.


Kauli ya Serikali

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema lengo la Serikali ni kulisha Afrika na dunia.

Bashe alisema katika mwaka 2021, mchele ulishika namba moja kati ya bidhaa zilizouzwa nje hivyo kufanya mwelekeo wa Serikali kuwa ni kuongoza katika uuzaji wa chakula nje hasa nafaka.

Ili kufanikisha hilo, uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji umefanyika na malengo ni kufikisha hekta milioni nane za umwagiliaji mwaka 2030.

Katika bajeti hii, asilimia 50 itaelekezwa kwenye umwagiliaji na asilimia 20 ya bajeti ya kilimo itawekezwa kwenye utafiti na uzalishaji wa mbegu.

“Pia tunarekebisha skimu zote za zamani ambazo ziliharibika. Tunaajiri wahandisi 320 wa umwagiliaji na kuweka skimu meneja kwenye kila skimu na kuweka maghala yote ambayo yapo kwenye skimu kuwa na usimamizi, huku tukiweka uzio mashamba yote ya umwagiliaji na kuweka mhandisi wa umwagiliaji kwenye kila wilaya,” alisema Bashe.

Alisema kuweka fedha kwenye utafiti na uzalishaji wa mbegu bora za mpunga, ni jambo ambalo limefikiriwa, huku likienda sambamba na ujenzi wa ekari 15,000 za umwagiliaji kwenye mashamba yote ya mbegu na utafiti.

“Pia Serikali sasa inafanya upembuzi yakinifu kwenye mabonde yote makubwa kwa ajili ya kujenga skimu za umwagiliaji,’’ alieleza.

Kuhusu soko la mchele alisema Afrika pekee inahitaji tani milioni 45 huku uzalishaji ukiwa tani 25 milioni jambo ambalo linafanya kuendelea kuwapo kwa fursa hiyo.


Wachumi

Dk Donath Olomi ambaye ni mtaalamu wa uchumi na biashara alisema ili kupata tija zaidi katika eneo hilo la mchele, ni lazima kuwapo kwa sera wezeshi na zinazotabirika.

“Kwa sasa sera zilizopo zinabadilika na si wezeshi, kukiwa na shida ya chakula kidogo Serikali inakataza kuuza nje ya nchi, hili linarudisha nyuma kilimo chochote, watu wanatakiwa kuwekeza kwa wingi ila mwekezaji akijua hapatabiriki, hawekezi,” alisema Dk Olomi.

Pia alisema upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo za gharama nafuu, ni suala linalopaswa kuendelea kuwekewa mkazo, huku akitaka uwekezaji katika upatikanaji wa maji.

“Uwepo wa maji utafanya watu wasibahatishe, watu wamwagilie, kuna baadhi ya sehemu miradi ya mabwawa haitunzwi vizuri kutokana na kukosa usimamizi, tukifanya haya tunaweza kukuza uzalishaji wetu,” alisema Dk Olomi.

Profesa Haji Semboja ambaye ni mchumi mbobevu alisema kinachotakiwa kufanyika ili kukuza biashara hiyo ni kuhuisha sera nzuri za kilimo cha biashara na sera za uwekezaji.

Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa kama nchi bado ina uwezo wa kuzalisha zaidi mazao hayo na kuuza nje, huku akieleza kuwa si mchele tu bali pia nguvu inaweza kuwekwa katika sehemu nyingine ikiwemo ngano.

“Hiyo ni kwa sababu tunayo ardhi yenye rutuba, tuna maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kuliko nchi nyingine ndani ya Afrika,” alisema Profesa Semboja.

Ili kuweza kufanya hilo alisema umefika wakati wa watu kuanza kuwekeza katika kilimo kikubwa kinachoweza kubadili mazao ya chakula kuwa mazao ya kilimo kwa kutumia umwagiliaji. Alipendekeza hayo yafanywe na wazawa na ikiwa itashindikana basi ubia uruhusiwe.


Mahindi nayo yamo

Aidha, mahindi nayo yameonekana kufanya vizuri kwani mapato yaliyotokana na mauzo yake yamepanda kwa asilimia 234 katika kipindi cha miezi nane ya kwanza ya huu.

Takwimu rasmi za Wizara ya Kilimo zinaonyesha Tanzania ilipata kiasi cha Sh325 bilioni, kutokana na mauzo ya mahindi nje ya nchi kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu.

Katika kipindi kama hicho mwaka jana, nchi ilipata Sh97.55 bilioni pekee. Ongezeko hilo linachangiwa na kuimarika kwa mauzo ya nje kwa asilimia 96, pamoja na ongezeko la asilimia 70.6 la bei ya bidhaa. Hii inaashiria mwaka jana, ambapo kilo moja ya mahindi iliuzwa kwa wastani wa Sh481.878.