Bajeti kiduchu kwa vijana, deni la Taifa likipewa kipaumbele

Dar es Salaam. Wakati vijana wakiwa ndiyo nguvu kazi inayotegemewa katika kujenga uchumi shindani, lakini ndilo kundi lililotengewa fedha kiduchu katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2025/26, huku robo ya bajeti hiyo ikielekezwa kulipa deni la Taifa.
Katika bajeti hiyo ya Sh56.49 trilioni, kundi la vijana limetengewa Sh38.4 bilioni, ikiwa ni kiwango kidogo zaidi cha fedha kilichotengwa kwa mujibu wa mgawanyo wa bajeti katika sekta.
Hata hivyo, kiwango hicho kilichotengwa ni ongezeko la asilimia 12.9 kutoka Sh34 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya vijana mwaka uliopita.
Hiyo ni kwa mujibu wa mgawanyo wa bajeti kwa sekta ulioainishwa kupitia hotuba ya mapato na matumizi ya Serikali, iliyosomwa leo na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, bungeni jijini Dodoma.
Katika mgawanyo huo, sekta iliyoongoza kwa kutengewa fedha nyingi ni huduma za utawala, ikibeba Sh24.5 trilioni, kati ya hizo deni la taifa litabeba Sh14.2 trilioni, huku mihimili ya utawala, usimamizi wa mapato ya matumizi, mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, ukitarajiwa kutumia Sh10.3 trilioni.
Kiwango kilichotengwa kwa ajili ya deni la Taifa ni takriban asilimia 25 ya bajeti yote.
Bajeti hiyo inaeleza, sekta ya elimu ndiyo itakayokuwa katika nafasi ya pili kwa kutumia fedha nyingi, ikitengewa Sh7.39 trilioni, ikifuatiwa na ulinzi, utawala wa sheria na usalama iliyopewa Sh6.3 trilioni.
Inayofuata ni sekta ya ujenzi, usafirishaji na mawasiliano, ikipewa Sh5.52 trilioni, kisha hifadhi ya jamii Sh3.1 trilioni na afya Sh3 trilioni.
Sekta nyingine ni nishati iliyotengewa Sh1.96 trilioni, ikifuatiwa na kilimo Sh1.92 trilioni.
Zinazofuata ni sekta ya maji Sh897.1 bilioni, habari, michezo na utamaduni Sh519.6 bilioni, maliasili, utalii na mazingira Sh317.4 bilioni, viwanda na biashara Sh239.5 bilioni, madini Sh225 bilioni na maendeleo ya jamii Sh196.5 bilioni.
Pia, imo sekta ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, iliyotengewa Sh166.9 bilioni.