Yemi Alade adai kulogwa kisa Beyonce

Muktasari:
- Katika mahojiano na CNN African Voices, Yemi Alade amefichua kwamba alipoteza sauti katika hali ya kushangaza sana baada ya kuwasili Los Angeles, Marekani ili kushirikiana na Beyonce katika albamu yake.
Nigeria. Mwimbaji wa Afrobeats kutokea Nigeria, Yemi Alade, (35), alipoteza sauti yake muda mfupi kabla ya kurekodi na staa wa Pop duniani, Beyonce Knowles, 43.
Katika mahojiano na CNN African Voices, Yemi Alade amefichua kwamba alipoteza sauti katika hali ya kushangaza sana baada ya kuwasili Los Angeles, Marekani ili kushirikiana na Beyonce katika albamu yake.
Utakumbuka Yemi Alade ni miongoni mwa wasanii wa Afrika walioshirikishwa na Beyonce katika albamu yake, The Lion King: The Gift (2019) ambayo ilikuwa maalamu kwa ajili ya filamu ya The Lion King (2019) chini ya Disney’s.
Wengine ni Burna Boy, Mr. Eazi, Tiwa Savage, Tekno, Busiswa, Moonchild Sanelly, Salatiel na Wizkid ambaye wimbo alioshirikishwa na Beyonce, Brown Skin Girl (2019) ulishinda Grammy 2021 ikiwa ni tuzo ya kwanza kwa staa huyo wa Nigeria.
Yemi Alade ambaye kipaji chake kilionekana kupitia Peak Talent Show 2009 na kuchukuliwa na Effyzzie kisha kuvuma zaidi na kibao chake, Johnny (2014), katika albamu hiyo ya Beyonce amesikika kwenye nyimbo mbili, Don’t Jealous Me na My Power.
Akiongea na Larry Madowo wa CNN, Yemi Alade aliyetoka na albamu yake, King of Queens (2014), amesema siku moja kabla ya kurekodi na kukutana na timu ya Beyonce alitembelea studio ambayo wangeitumia na kila kitu kilikuwa sawa.
Hata hivyo, alipoamka asubuhi iliyofuata, aligundua kwamba hakuwa na uwezo wa kuzungumza, licha ya kusikia vizuri hakuweza kutamka maneno hivyo alilazimika kuwasiliana na watu kupitia maandishi.
Mara moja alifanya mpango wa kurejesha sauti yake, alitumia mchanganyiko wa maji moto, vitamini C, tangawizi na chai, baada ya mafundo kadhaa sauti yake ilirejea kama kawaida na kuweza kurekodi nyimbo mbili na Beyonce, mshindi wa Grammy 32.
Yemi Alade anahusisha tukio lake la kupoteza sauti ghafla na imani za kishirikina akidai ni hujuma kutoka kwa watu wa kijiji chake huko Nigeria lakini anashukuru kwamba juhudi zao mbaya hazikuweza kuzaa matunda.
Ikumbukwe hadi mwanzoni mwa mwaka 2019 Yemi Alade alikuwa ndiye mwimbaji pekee wa kike Afrika aliyatazamwa (views) zaidi ya mara milioni 100 YouTube, huku akiwa ni msanii wa pili Nigeria baada ya Davido.
Yemi Alade sio mwanamuziki wa kwanza Nigeria kupata changamoto ya kupoteza sauti, Julai 2022 Tems alitangaza kupata tatizo la sauti linajulikana kama Reflux Laryngitis, hivyo kusogeza mbele show zake zilipopangwa kufanyika Birmngham na London, Uingereza.
Tems ambaye ni msanii wa kwanza wa kike Nigeria kushinda Grammy na aliyechaguliwa mara nyingi zaidi kuwania tuzo hizo, alipata tatizo hilo kufuatia mfululizo wa matamasha barani Ulaya na Amerika Kusini, hivyo akalazimika kupumzika kwa muda.