Wanamuziki wanavyotumia soka kubaki kwenye gemu

Muktasari:
- Kutokana na hilo naweza sema soka bila muziki ni kama chai bila sukari, hii inajionyesha kwenye baadhi ya matukio ya soka nchini, ambayo husindikizwa na pafomansi za wasanii mbalimbali na wakati mwingine ukikosekana muziki hata idadi ya mashabiki inapungua.
Sihami, Ndo huyo huyo, Simba, Kwa Mkapa hatoki mtu, Yanga Anthem, na Yanga Tamu, haya ni majina ya baadhi ya ngoma ambazo hupigwa kwenye mechi mbalimbali za soka nchini, kupigwa kwake huamsha vaibu la mashabiki hata kama wakiwa na mawazo ya mchezo ujao.
Kutokana na hilo naweza sema soka bila muziki ni kama chai bila sukari, hii inajionyesha kwenye baadhi ya matukio ya soka nchini, ambayo husindikizwa na pafomansi za wasanii mbalimbali na wakati mwingine ukikosekana muziki hata idadi ya mashabiki inapungua.
Achana na ile iliyozoeleka kwenye fainali za Kombe la Dunia, wasanii hutunga nyimbo na kutumbuiza kama ilivyokuwa Afrika Kusini (2010), Shakira alikuwa na wimbo unaoitwa ‘Waka Waka’ , akaimba tena (2014) Brazil, akishirikiana na Carlinhos Brown wimbo ‘La La La’. Au Urusi (2018) ‘Live It Up’ ulioimbwa na Will Smith, Nicky Jam, na Era Istrefi, pia kwenye fainali (2022) Qatar, alitumbuiza Davido, Aisha na Triniadad Cardona wimbo ‘Hayya Hayya’.

Kama ilivyo kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia,
Bongo pia mwamko umekuwa mkubwa, muziki na soka vimeingiliana, jambo linalosababisha vitu hivi viwili kukua pamoja.
Utakumbuka mwaka 2023 mwanamuziki Zuhura Othman ‘Zuchu’ alipafomu, Simba Day kwenye Uwanja wa Mkapa huku akiwa amepigilia nguo zenye rangi nyeupe na nyekundu kuwakilisha timu hiyo. Si yeye tu pia Juni 13, 2023 nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, alikiwasha kwenye paredi la Yanga, iliyofanyika makao makuu ya klabu hiyo Jangwani na kuwarusha mshabiki ipasavyo.

Mbali na wasanii kuhudhuria na kupafomu kwenye matamasha ya soka, pia huingia studio na kurekodi nyimbo kwa ajili ya mashabiki wa mchezo huo, kama alivyofanya Harmonize mwaka 2023, kuachia wimbo uitwao Yanga, ambao YouTube umetazamwa na watu 1.3 milioni hadi sasa.
AliKiba aliachia ‘Mnyama’ (2023) YouTube 3.4 milioni, Marioo ‘Yanga’ (2023) YouTube 1.3 milioni, Nandy ‘Yanga’ (2022 ) YouTube 1. 4 milioni, Tunda Man ‘Tambeni’ (2021 ), 1.5 milioni na nyinginezo.

Mbali na wasanii maarufu ambao wameimba nyimbo za soka, wapo pia wasanii wachanga ambao wamejulikana kwa ukubwa baada ya kuimba nyimbo zinazogusa matukio ya soka nchini.
Utakumbuka ujio wa aliyekuwa mchezaji wa klabu ya Simba mwaka 2022, raia wa Serbia Dejan Georgijevic ulipelekea mwanamuziki wa singeli Viwalo Viva, kuangusha kibao kilichokwenda kwa jina la ‘Mlete Mzungu’ na kumfanya msanii huyo kutambulika kwa wapenzi wa muziki. Hadi sasa ‘Mlete Mzungu’ umetembelewa na wasikilizaji 360k YouTube.
Si yeye tu hata Sir Jay ambaye alifahamika kupitia wimbo wa Yanga uitwao Ndo huyo huyo (2023), ambao hadi sasa YouTube una wasikilizaji 322k. Hajaishia hapo pia ana ngoma nyingine za soka kama vile ‘Watoto wa Jangwani’.
Hayo yote yanaonesha namna ambavyo vitu hivi viwili vinavyokwenda pamoja na kujijengea wigo mpana zaidi.

Kwani wapo baadhi ya wasanii akiwemo Tunda Man ambao hawafanyi gemu kama mwanzo lakini kupitia ngoma zinazohusu soka wanaendelea kusikika.
Uwepo wa wasanii kwenye soka husaidia kuvuta mashabiki wa muziki na kuwasogeza kwenye boli, pia wapenzi wa boli wengi hujikuta wakizama kwenye muziki kuwafuatilia wasanii ambao hufanya poa kwenye matamasha ya soka.

Kwa hiyo pande zote mbili hunufaika, lakini pia nyimbo mbalimbali za wasanii zimekuwa zikitaja majina na wanasoka na wakati mwingine timu.