Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanasha alivyoacha maswali kwa mashabiki wake

Muktasari:

  • Tanasha, mwanamuziki na mwanamitindo kutoka Kenya, jina lake lilitakata Afrika Mashariki kufuatia kushirikiana na Diamond katika wimbo ‘Gere’ kutoka katika EP yake, DonnaTella (2020) ambao ulivuma kwa sababu ya uhusiano wao.

Dar es Salaam, Baada ya kuachana na Diamond Platnumz tu polepole, Tanasha Donna alianza kushuka kimuziki na sasa hasikiki kabisa, na hilo linaacha swali iwapo staa huyo wa WCB Wasafi aliondoka na nyota yake katika sanaa.

Tanasha, mwanamuziki na mwanamitindo kutoka Kenya, jina lake lilitakata Afrika Mashariki kufuatia kushirikiana na Diamond katika wimbo ‘Gere’ kutoka katika EP yake, DonnaTella (2020) ambao ulivuma kwa sababu ya uhusiano wao.

Hata hivyo, kabla ya Tanasha kutoa wimbo huo uliotayarishwa na Laizer Classic tayari alishaachia kazi yake, Radio (2019) wakati akiwa mtangazaji wa NRG Radio Kenya na wengi walitarajia angefika mbali. 

Uhusiano wake na Diamond ulioanza mwishoni mwa 2018 ulikuwa kama neema katika ndoto ya kufika mbali kimuziki na kweli mambo yalianza vizuri ila walipoachana Machi 2020, muziki kwa Tanasha ikawa ni kazi ngumu.

Utakumbuka Tanasha alipata umaarufu Afrika Mashariki pindi alipotokea kwenye video ya wimbo wa Alikiba na Christian Bella, Nagharamia (2015), na kabla ya hapo alikuwa akifanya mitindo chini ya Dominique Model’s Agency huko Brussels, Ubelgiji.

Kwa sasa ni miezi minane bila Tanasha kutoa kazi mpya wimbo wake wa mwisho kuachia ‘Okay’ ulitoka Julai 26, 2024 na video yake haijatoka hadi leo licha ya kutoa ahadi nzuri kwa mashabiki wake kufuatia ukimya wa muda mrefu. Ikumbukwe kabla ya kurejea hiyo Julai 26, 2024, Tanasha alikuwa amekaa kimya kimuziki kwa zaidi ya mwaka mmoja wimbo wake mwisho kuachia ‘Karma’ akimshirikisha Barak Jacuzzi ulitoka Agosti 2022 na baada ya hapo akatoweka katika muziki.

Kwa nje inaonekana kuna mambo mengi hayaendi sawa kwa Tanasha upande wa muziki, video za nyimbo zake nyingi ikiwemo ‘Radio’ uliomtambulisha mwaka 2019 zimeondolewa katika mtandao wa YouTube.

Tanasha ambaye alitabiriwa na wengi kufika mbali kutokana na ukali wa EP yake iliyowashikirisha Diamond, Mbosso na Khaligraph Jones, nyimbo zake nyingine zilizoshushwa YouTube ni Nah Easy, Ride, Te Amo na kadhalika. Mnamo Januari 2023 Tanasha aliijia juu kampuni moja ya usambazaji muziki na kutishia kuishtaki kwa madai ya kutoa video ya wimbo wa Tommy Flavour ‘Numero Uno’ ambao kashirikishwa bila ridhaa.

Kufuatia malalamiko hayo, video hiyo ilifutwa YouTube na hadi sasa haijarudishwa na haijawahi kuelezwa sababu ya kuchukuliwa uamuzi huo mgumu uliowaacha mashabiki njia panda. 

Mbali na kazi yake ya muziki, Tanasha pia amekuwa kimya sana katika mitandao ya kijamii hasa Instagram, sio mtu wa kuposti kila mara kama wanavyofanya wanamitindo wengi, ukurasa wake una machapisho 35 kwa sasa. Pengine hana maudhui ya kutosha na kama hana ni wazi hajishughulishi ipasavyo na muziki na mitindo, mara ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa Desemba 10, 2023 alipohudhuria shoo ya Zari All White Party jijini Kampala, Uganda.

Yupo kimya na hakuna anayemfuatilia kama wakati yupo na Diamond ambaye walikuwa pamoja kati ya 2018 hadi 2020 na kujaliwa kupata mtoto mmoja, Naseeb Jr (2019) ambaye ni wa nne kwa Diamond.

Mnamo Agosti 2023 Tanasha alikuwa Bongo kwa ajili ya besidei ya mtoto wake ambaye husheherekea siku hiyo na baba yake, licha ya kuwa studio wakati Diamond na Naseeb Jr wakipiga picha, Tanasha hakuonekana katika picha yoyote.

Kwa kifupi amekuwa mtu wa kujificha sana, ilishangaza kuonekana akimpongeza msanii wa WCB Wasafi, D Voice kwa uzinduzi mzuri wa albamu yake, Swahili Kid (2023) siku moja baada ya tukio hilo lakini katika shughuli yenyewe hakuonekana kabisa.

Ikumbukwe kwa mujibu wa Tanasha, sababu ya kuachana kwake na Diamond ni kutokuwa na maelewano mazuri na Mama mzazi wa Diamond, Bi. Sandra maarufu kama Mama Dangote ambaye anadai alikuwa anaingilia sana uhusiano wao.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna mwanamke ambaye amewahi kufanyiwa birthday party kubwa na Diamond kama Tanasha, birthday yake ya mwaka 2019 pale Mlimani City, Dar es Salaam, Diamond alimzawadia Tanasha gari jipya aina ya Toyota Land Cruiser V8.

Zari, Hamisa, Wema Sepetu na Penny hawakuwahi kufanyiwa kitu kama hicho, ni Tanasha pekee ila sasa mambo yamebadilika licha kuonekana wameshibana kwa sababu Tanasha amezaliwa siku moja na Mama Dangote ambaye naye alizawadiwa gari siku hiyo. 

Utakumbuka kabla ya Tanasha, tayari Diamond aliwahi kuwa na uhusiano wanawake wengine maarufu Afrika Mashiriki, miongoni mwao ni Zari The Bosslady (Uganda) aliyejaliwa naye watoto wawili na Hamisa Mobetto (Tanzania) mwenye mtoto mmoja naye.