SMZ kumkabidhi Idriss Elba hekta 80 kwa ajili ya studio

Msanii Idriss Elba
Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa hekta 80 katika Kijiji cha Fumba kwa ajili ya nguli wa filamu duniani, Idriss Elba kufungua Studio ya Filamu ya Kimataifa.
Hayo ameyasema leo Alhamisi Agosti Mosi 2024 Waziri wa Uwekezaji Zanzibar Shariff Ali Shariff, wakati akifungua tamasha la 27 la ZIFF.
Elba aliyezaliwa Septemba 6, 1972 London, Uingereza kwa sasa ni mmoja wa waigizaji maarufu na wenye mafanikio makubwa, ambaye ameonyesha ujuzi wake katika filamu, na muziki.
Elba alianza safari yake ya uigizaji akiwa kama muhusika anayecheza sehemu chache katika vipindi vya televisheni, mwaka 2002, alijulikana zaidi baada ya kuigiza kama Stringer Bell katika mfululizo wa kipindi cha "The Wire".
Baada ya mafanikio hayo, Elba aliendelea kujitokeza katika filamu mbalimbali uhusika kama vile Luther katika "Luther", ambapo alikubalika sana kwa uigizaji wake.
Aidha, alicheza katika filamu ya "Pacific Rim", "Mandela: Long Walk to Freedom", na "Thor".
Mbali na uigizaji, Elba ni mtunzi na mtayarishaji wa muziki. Idris Elba pia katika masuala ya kijamii. Amekuwa balozi wa haki za binadamu na amekuwa akishiriki katika miradi mbalimbali inayopigania haki na usawa wa kijinsia.
Mwaka 2023 aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Zuhura Yunus, wakati akiwapa waandishi wa habari taarifa kuhusu matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan huko Davos, Uswisi, alisema Idris Elba, ana mipango ya kuwekeza studio kubwa ya filamu nchini Tanzania.