Zaidi ya watu 190,000 wapona corona, wamo watu maarufu

Dar es Salaam. Iddi Mbita amekuwa mgonjwa wa kwanza wa virusi vya corona, Covid-19 kufariki dunia, tangu Tanzania ilipotangaza kuwa na mtu wa kwanza kuugua ugonjwa huo mpya.
Habari za Iddi, aliyeugua kwa takriban wiki moja, zimefunika habari njema za kupona kwa Isabela Mwampamba ambaye alikuwa mtu wa kwanza kugundulika kuwa na maambukizi hayo na amekuwa wa kwanza kupona ugonjwa huo ulioua zaidi ya watu 44,000 kote duniani hadi jana jioni.
Kwa mujibu wa taarifa ya Machi 26 iliyotolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu mgonjwa huyo mwenye miaka 46 aliyegundulika Arusha akiwa wa kwanza nchini, ameonyesha kupona ugonjwa huo baada ya kupitia vipimo vyote.
Isabela ni kati ya wagonjwa wengi waliougua ugonjwa huo wakatibiwa na kupona. Jana, Waziri Ummy pia alitangaza mgonjwa wa pili kupona hapa nchini, bila kufafanua ni nani.
Tovuti ya worldometer.com inaonyesha kuwa kati ya wagonjwa 871,985 waliokuwa wameripotiwa kupata maambukizi hayo kote duniani, 190,000 wamepona ugonjwa huo hadi jana jioni licha ya kwamba bado haujapata tiba.
Hata hivyo, habari hiyo njema haimaanishi kuwa ugonjwa huo umeshapatiwa tiba au umedhibitiwa na katika ujumbe wa watu maarufu waliopona, wamesisitiza kufuata maelekezo ya madaktari.
Pia madaktari wa ndani na nje waliohojiwa wanasisitiza kuwa jambo muhimu ni watu kufuata masharti kujikinga kushikwa na ugonjwa kutokana na ukweli kuwa tiba ya ugonjwa huu haijapatikana.
“Baadhi ya wanaopona ni wagonjwa ambao wanapewa tiba kwa ugonjwa ambao madaktari wameona dalili zake, huku kinga yao ya mwili ikipambana kuvishinda virusi vya corona,” anasema Profesa Jonathan Ball wa Chuo Kikuu cha Nottingham alipoongea na BBC.
“Kama mgonjwa ana dalili za tatizo la kupumua, madaktari humsaidia kupumua. Kama ni shinikizo katika viungo, watajaribu kuusaidia mwili kuondoa hilo shinikizo,” anasema Profesa Ball.
Naye Dk Tumaini Haonga wa kitengo cha elimu cha Wizara ya Afya anathibitisha kuwa mtu aliyeambukizwa virusi hivyo anaweza kupona.
Kulingana na mtaalamu huyo virusi vinapoingia mwilini, kinga ya mwili inaanza kupambana kuvitokomeza.
Kasi ya mapambano hayo inategemea na uimara wa kinga ya mwili ya mgonjwa husika na matokeo yanaweza kuwa chanya au hasi kwa mwili.
“Kinga ya mwili inapopambana inaweza kufanikiwa kwa asilimia 80. Kiwango hiki ni kwa mtu ambaye kinga yake ipo juu kinyume na hapo mgonjwa anaweza kudhoofika au hata kupoteza maisha.
“Ikitokea kinga ya mwili ikashinda kwenye mapambano hayo kile kirusi kinakufa na kitamezwa na seli za mwili. Hapo mtu akipima atakutwa negative na ndiyo inakuwa amepona,” alisema Dk Haonga.
Mtaalamu huyo anaeleza kuwa kwa mtu mwenye kinga imara zoezi la kupambana na kirusi huchukua kati ya siku 7 hadi 10.
Alisema licha ya kuwa hakuna dawa iliyothibitika kutibu corona, mgonjwa hutibiwa dalili zote zinazojitokeza ili kuhakikisha kinga yake ya mwili haishuki.
Alivitaja vinavyochochea kushuka kwa kinga ya mwili kuwa ni magonjwa, lishe duni na msongo wa mawazo.
Isabela ndiye mgonjwa aliyetangazwa na Serikali ya Tanzania kuwa amepata ahueni, lakini yumo mwanamuziki nyota wa miondoko ya rap, Mwana FA na Sallam, meneja wa nyota wa muziki nchini, Diamond Platnamuz, waliojitangaza wamepona.
Kama ilivyo kwa nyota wengine duniani, Mwana FA, ambaye jina lake halisi ni Hamisi Mwinjuma, alithibitisha kuwa amekutwa hana tena virusi hivyo, Machi 19 alipoweka video katika akaunti yake ya Instagram akiwahakikishia mashabiki wake kuwa amepona na kutaka “kila mmoja amjali mwenzake”.
Sallam naye alitangaza Jumanne kuwa amepona ugonjwa huo wa virusi vya corona
“Nimshukuru Allah na pia niwashukuru wote mlionitumia msg, comments, DM na dua zenu. Bila kuwasahau Temeke Isolation Centre kwa kuwa bega kwa bega pamoja na mie bila kunichoka pale nilipokuwa nimezidiwa,” anasema Sallam akikaririwa na pulselive.co.ke.
“Shukurani zangu zingine kwa madaktari bingwa kujua maendeleo yangu mara kwa mara na pia Serikali yangu na viongozi wake husika. Wizara na mkoa walikuwa hawana ubaguzi kutujulia hali na kutupa moyo na kutupa mahitaji tutakayo. Naomba niwape taarifa ndugu yenu, kijana wenu nimechukuliwa vipimo mara mbili na nimekutwa NEGATIVE na kwa sasa nipo huru. Ila naomba tuendelee kujikinga na kufuata ushauri wa viongozi wetu na kuacha maelekezo ya utashi yasiyokuwa na uhakika. ALLAH IS GREAT.”
Hadi jana Tanzania ilikuwa imetangaza wagonjwa 20 walioripotiwa kuwa na ugonjwa huo, wawili wakiwa wamepona na mwingine mmoja kufariki.
Orodha ya watu waliopona ugonjwa huo duniani inahusisha watu wa kada tofauti; viongozi wa nchi, wanasiasa, wanamichezo, wasanii na wengine maarufu.
Mtoto wa Malkia Elzabert, Charles na familia yake ni kati ya waliogundulika kuwa na maambukizi. Msemaji wake alisema Prince alitumia siku saba kujitenga katika jumba la kifalme la Birkhall akifuata maelekezo ya Serikali baada ya kupata mafua ya kawaida.
Taarifa nyingine za kupona Covid-19 zilitoka kwa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta ambaye aligundulika kuwa na maambukizi Machi 12, lakini wiki iliyopita alitangazwa kuwa amepona na kuanza shughuli zake.
Arteta aliugua sambambana mchezaji wa Chelsea, Collum Hudson-Odoi ambaye pia amepona.
Wengine waliougua na wamepona ni nyota wa filamu wa Hollywood, Tom Hanks na mkewe Rita Wilson, nyota wa Uingereza Idris Elba, na Sophie Gregoire Trudeau, mke wa Waziri Mkuu wa Canada.