Show za Chaka to Chaka zilivyompa maisha Mr. Blue

Muktasari:
- Akizungumza na Mwananchi, Byser amesema show hizo zinapaswa kuheshimiwa na kutambulika kwani zimempatia mafanikio makubwa.
Dar es Salaam. Hivi karibuni baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva walionekana wakifanya Shows za Chaka to Chaka(Vijijini) ambazo licha ya kubezwa na mashabiki zimekuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya wasanii nchini. Ikiwemo kwa msanii Mr. Blue ambaye amefanya shoo hizo kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwananchi, Byser amesema show hizo zinapaswa kuheshimiwa na kutambulika kwani zimempatia mafanikio makubwa.
"Kwa mimi niseme shikamoo Chaka to Chaka, naomba niiamkie kwa sababu ndio imefanya nimefika hapa. Watu wanajua kuna ndugu zangu siwezi kuwataja lakini ni waheshimiwa wa shoo hizo kama unavyojua huwa ngumu kidogo kuzipost mitandao .

“Anaweza kuwa Chaka to Chaka lakini asiposti mpaka ukikutana naye. Lakini tunashukuru tumepata wafuasi wengi, zamani tulikuwa tunahesabika watu wa show hizo, sasa hivi naona vijana mmekuwa wengi kama mmejua hela yenu ilipo na mnatakiwa muifate, ni jambo zuri sana," amesema Blue.
Ameongezea kwa kusema shoo hizo haziui brand ya msanii bali humpa nafasi ya kukutana na mashabiki wake ambao wapo maeneo ya mbali.
"Hakuui brand ya msanii, kama ipo ipo tu Mungu amekubariki hata ufanye nini huwezi kuipandisha. Kama umepewa brand itabaki.
"Mpaka nafikia hapa ni shoo hizo zimenipa nyumba zaidi ya moja, hata ambayo naishi leo kuna hela mule mpaka za watu wangu, kwahiyo shikamoo Chaka to Chaka na niwaambie vijana pale upo katika kutafuta maisha yako. Usiogope kudharaulika wala chochote, tafuta mpaka maisha yatakapokuwa vizuri utaacha," amesema Blue.
Amesema katika historia yake ya kufanya Chaka to Chaka hawezi kusahau tukio la kupigwa vibao kama mtoto.
"Siwezi kusahau tukio la kupigwa vibao kama mtoto, tulipigwa vibao na mshikaji wangu mmoja hivi, mtoto wa kizenji tulienda kwenye shoo baada ya kupafomu tukadakwa juu kwa juu na jamaa akatuambia twende sehemu. Kufika huko tukaimbishwa sana mwisho wa siku tukahitaji kutoka jamaa hataki akatupiga vibao mimi na mshikaji wangu kama watoto na jamaa alikuwa na bunduki, kwa hiyo mambo ni mengi tunayokutana nayo," amesema Blue.
Hata hivyo, hakuacha kugusia sababu ya nyimbo zake kudumu kwenye masikio ya mashabiki wake.

"Natumia muda kutengeneza muziki na ndiyo maana unachukua muda mrefu pia kuishi kwa sababu mimi ni mgumu sana kwenye kutoa nyimbo hovyo hovyo. Baadhi ya watayarishaji wananiuliza kwanini mimi ni mgumu kuamini nyimbo itoke kwa hiyo ni tabia ambayo ninayo toka zamani na imenisaidia kupata nyimbo nzuri," amesema Byser.