Sauti nzuri ya Mungu katika ndoto ya Celine Dion

Muktasari:
- Kutokana na kuvutiwa na wimbo wa mwanamuziki wa Ufaransa, Hugues Aufray, Celine (1966) wakaona sio vibaya kumpa jina hilo mtoto wao huyo aliyezaliwa Machi 30, 1968.
Dar es Salaam. Miaka 56 iliyopita huko Charlemagne, Quebec nchini Canada, Adhemar Dion na mkewe Therese Nee walijaliwa mtoto wa kike na kuamua kumpa jina la Celine akiwa ni mtoto wa 14 na mwisho katika familia yao.
Kutokana na kuvutiwa na wimbo wa mwanamuziki wa Ufaransa, Hugues Aufray, Celine (1966) wakaona sio vibaya kumpa jina hilo mtoto wao huyo aliyezaliwa Machi 30, 1968.

Uamuzi huo ni uthibitisho kuwa familia hiyo yenye asili ya Ufaransa iliisikia na kuitii sauti nzuri ya Mungu na hivyo kumuhusisha mtoto wao na muziki mapema kwani fungu lake kubwa alilopangiwa hapa duniani lipo kwenye tasnia hiyo.
Mtoto huyo kwa sasa ndiye Celine Dion, 56, mwanamuziki maarufu ulimwenguni katika miondoko ya Pop, Rock na R&B, huku akishikilia rekodi kama msanii wa Kifaransa aliyeuza zaidi kwa wakati wote, kwa ujumla ameuza rekodi zaidi ya milioni 200.
Staa huyo wa kibao maarufu, I'm Alive (2002) kutoka katika albamu yake ya saba, A New Day Has Come (2002), tayari ameshinda tuzo tano za Grammy na kutunukiwa shahada mbili za udaktari wa heshima kutoka vyuo vya Berklee na Laval.
Celine aliyelelewa katika misingi ya Kikatoliki ndani ya familia yenye maisha duni, sauti nzuri ya Mungu ina maana gani katika maisha yake binafsi na kazi yake ya muziki kwa ujumla?.

Tangu alipokuwa mdogo, Celine alipenda muziki, mama yake Therese alimsaidia kurekodi wimbo wa kwanza wa Kifaransa, 'Ce n'était qu'un rêve' au Kiingireza ukiitwa 'Nothing But a Dream' au 'It Was Only a Dream' - 'Ilikuwa ni Ndoto Tu' kwa Kiswahili.
Kaka yake Celine alipopata anuani ya Rene Angelil kutoka nyuma ya albamu ya mwanamuziki wa Canada, Ginette Reno, aliisikia sauti nzuri ya Mungu akimwambia amtumie Angelil wimbo huo aliorekodi mdogo wake Celine na punde tu akafanya hivyo.
Angelil, mtayarishaji muziki aliyekuwa na umri wa miaka 38 wakati huo, aliposikia sauti ya Celine, binti wa miaka 12, akakoshwa vilivyo na talanta yake, naye sauti ikamjia na kumueleza hii ni mali, fanya haraka uichukue itakufaa zaidi hata nje ya muziki.

"Nilipokuwa nikiimba Angelil alianza kulia machozi, nilijua basi nimefanya kazi nzuri," alisema Celine alipokuwa akizungunzia kutano lake la kwanza na Angelil mwaka 1980 na kuamua kuwa meneja wake.
Basi Angelil akaweka rehani nyumba na utajiri wake ili kufadhili albamu ya kwanza ya Celine aliyoimba kwa Kifaransa, La voix du bon Dieu (1981), jina la albamu hii kwa lugha ya Kiswahili ni "Sauti Nzuri ya Mungu", au "Good God's Voice" kwa Kiingereza.

Kwanini Celine aliipa albamu hiyo jina hilo?, pengine aliona jinsi ambavyo ndoto zake na familia yake vinavyoenda kutimia, albamu hiyo iliyouza nakala zaidi ya 100,000 ilifanya vizuri na kutawala chati za Canada huku baadhi ya nyimbo zikifanya vizuri Ufaransa.
Baada ya kujifunza Kiingereza, Celine alijiunga na Epic Records nchini Marekani na kutoa albamu yake ya kwanza ya Kiingereza, Unison (1990) iliyompa mafanikio makubwa ikiwemo kushinda tuzo ya Grammy.
Albamu zake mbili, Falling into You (1996) na Let's Talk About Love (1997) ziliuza nakala zaidi ya milioni 30 Marekani, huku akipata umaarufu na nyimbo zake kama 'The Power of Love', 'Think Twice', 'It's All Coming Back to Me Now', 'My Heart Will Go On' n.k.
Mwaka 2009, Celine alitajwa na Los Angeles Times kama msanii aliyeingiza fedha nyingi kwa muongo huo ambazo ni Dola748 milioni. Kutoka familia duni hadi kushika fedha hizo, kweli ilikuwa ni sauti nzuri ya Mungu katika ndoto yake ya muziki.
Hata hivyo, ni vigumu kutenganisha mafanikio hayo na uhusiano wake na Angelil, unajua Celine alipofikisha miaka 19 walichumbiana, na mwaka 1994 wakati Celine ana miaka 25 wakafunga ndoa.
Ndoa hii yenye tofauti kubwa ya umri wakiwa wamepishana miaka 26, yaani Angelil kazaliwa Januari 1942 na Celine Machi 1968, iliwaleta duniani watoto watatu, Charles (2001) na pacha Nelson na Eddy (2010).
Celine alimfaa zaidi Angelil pale alipongundulika ana saratani ya koo mwaka 1999, alisimamisha maonyesho yake kwa miaka miwili ili kumuuguza mumewe. Ila kwa bahati mbaya alfajiri ya Januari 14, 2016 Angelil alifariki zikiwa ni siku mbili kabla ya siku yake ya kuzaliwa.

"Ninahisi kama Angelil amenipa mengi kwa miaka mingi na hadi leo anafanya hivyo, nikiwaona watoto wangu ni kama bado tunaishi naye, yeye ni sehemu ya maisha yetu kila siku," alisema Celine mwaka 2021.
Oktoba 2016 Celine katika onyesho lake huko Las Vegas alifichua katika maisha yake hajawahi kumbusu mwanaume mwingine zaidi ya marehemu mumewe na vigumu kusema kama atakuja kupenda tena.
"Sijawahi kumbusu mwanaume mwingine maishani mwangu zaidi yake, kwa hiyo alikuwa mwanaume wa maisha yangu, alikuwa mwenzangu na tulikuwa kitu kimoja. Kwa hiyo alipoacha kuteseka (kufariki) nilijiambia yuko sawa na hastahili kuteseka," alisema Celine Dion.