Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nahreel nyuma ya mafanikio ya Vanessa

Muktasari:

  • Staa wa Bongofleva, Vanessa Mdee a.k.a Vee Money bado anatambua mchango mkubwa wa mtayarishaji muziki, Nahreel kutoka studio ya The Industry kwa kumtengenezea muziki uliokuza chapa yake kitu anachojivunia hadi sasa.

Dar es Salaam. Staa wa Bongofleva, Vanessa Mdee a.k.a Vee Money bado anatambua mchango mkubwa wa mtayarishaji muziki, Nahreel kutoka studio ya The Industry kwa kumtengenezea muziki uliokuza chapa yake kitu anachojivunia hadi sasa.

Vanessa ambaye ameachana na muziki kwa miaka zaidi ya mitano sasa na kujikita katika familia, ameweka wazi hilo wiki hii ambapo wimbo wake, Nobody But Me (2015) uliotayarishwa na Nahreel ukitimiza miaka 10.

Utakumbuka baada ya kusainiwa na Bxtra Records, zamani B’Hits Music Group, ndipo Vanessa akatoka na wimbo wake, Closer (2013) ulioshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Wimbo Bora wa RnB 2014.

Na baadaye Vee alitoa albamu moja, Money Mondays (2018), alifanya kazi na Universal  Music Group (UMG), huku akianzisha Mdee Music, rekodi lebo iliyokuja kuwasaini wasanii wawili, Brian Simba na Mimi Mars ambaye ni mdogo wake.

“Miaka 10 iliyopita tulitoa wimbo ‘Nobody But Me’ nikishirikiana na K.O, na baada ya hapo ni historia kama wanavyosema. Ni wimbo wangu uliofanya vizuri sana na ulibadilisha kabisa mwelekeo wa kazi yangu ya muziki kuwa bora,” alisema na kuendelea.

“Kamwe sitasahau jinsi K.O alivyokuwa mkarimu hata kushiriki katika huu wimbo ukichana versi yake na kuimba sehemu ya utangulizi. Utukufu kwa Mungu. Heri ya kumbukizi ya miaka kwa Nobody But Me,” alisema Vanessa, mtangazaji wa zamani wa MTV Base.

Pia Vee alimshukuru Joh Makini kwa kumwandikia K.O kutokea Afrika Kusini mistari ya Kiswahili aliyochana mwanzoni mwa wimbo huo ambao video yake imetazamwa zaidi ya mara milioni 5.1 YouTube ikiwa ni video yake ya pili kupata namba kubwa.  

Kwa mara ya kwanza video yake ilitambulishwa kupitia MTV Base hapo Machi 26 ikiwa ni video ya pili kwa Vanessa kutambulishwa katika kituo hicho cha kimataifa baada ya ile wimbo, Hawajui (2015) uliotengenezwa pia na Nahreel.

Kufanya vizuri kwa wimbo huo kulimpa Vanessa show za kimataifa, alitumbuiza tamasha la AMC 2015 Afrika Kusini pamoja na mastaa wengine kama Davido, AKA, Wizkid n.k, pia tamasha la Gidi Culture huko Nigeria.

Pia ulipelekea kuteuliwa kuwania tuzo za MTV MAMAs 2015 kama Msanii Bora wakike Afrika, na mwaka uliofuatia akatajwa na jarida la Essence Marekani kuwa ni miongoni mwa wanawake 15 wenye ushawishi mtandao Afrika akiwa Mtanzania pekee aliyechomoza.

“Mungu akubariki Nahreel kwa utayarishaji huu bila kumsahau Justin Campos kwa video hii,” alisema Vanessa ambaye alitangaza kuachana na muziki hapo Julai 2020 kwa madai ya kutomlipa kulingana na juhudi zake.

Nahreel anayetajwa hapa ni yule anayeunda kundi la Navy Kenzo na mwenzake Aika, mwamba amefanikiwa kama mwimbaji na kama mtayarishaji akifanya kazi na wasanii kama Joh Makini, Diamond Platnumz, Weusi, Mwana FA, AY, Izzo Bizness, G Nako, Roma n.k.

Ukiachana na Nobody But Me (2015) na Hawajui (2015), Nahreel ametengeneza nyimbo nyingi za Vanessa kama Come Over (2014), Never Ever (2015), Niroge (2016), Wet (2018), n.k. Na zote hizi video zake zimeongozwa na Justin Campos kutokea Gorilla Films ya Afrika Kusini.

Hata hivyo, Vanessa naye ana mchango katika mafaniko ya Nahreel, ipo hivi Vee ndiye aliwashauri Navy Kenzo watoe wimbo wao, Chelewa (Bokodo) ambao uliwatambulisha vizuri zaidi na ukawa mwanzo wa mafanikio yao.

Navy Kenzo walikuwa na mpango wa kwenda kujiendeleza kimasomo nje ya nchi na kuachana kabisa na muziki baada ya kutoona matunda yake ila walivyofuata ushauri huo wa Vanessa milango kwao ikafunguka na mengine sasa ni historia.

Baadaye Navy Kenzo walikuja kumshirikisha Vanessa katika wimbo wao, Game (2015) ambao video yake ilishika namba moja kwenye chati za muziki za MTV Base, pia ilifika namba chati za Trace Urban ya Ufaransa na Soundcity TV ya Nigeria.

Ikumbukwe kabla ya Nahreel kufungua studio yake ya The Industry, alifanya kazi katika studio mbalimbali ikiwemo Kama Kawa Records, Home Time Records na Switch Studio yake Quick Rocka.

Na baada ya Nahreel kuondoka Switch, nafasi yake ikachukuliwa na Luffa, naye alipohamia Wanene Studio, nafasi yake ikachukuliwa na S2kizzy.