Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mastaa hawa mizani iko sawa kwa Alikiba, Diamond

Muktasari:

  • Hata hivyo, kutokana na ushindani wao kimuziki ulizaliwa uhasama wa kikazi wenye timu mbili ndani yake zinazohusisha mashabiki, wasanii wenzao, watayarishaji muziki, wadau n.k.

Dar es Salaam. Ni wazi kuwa Alikiba na Diamond Platnumz wamekuwa na nguvu kubwa ya ushawishi sio kwa mashabiki tu bali hata kwa wasanii wenzao ambao wamekuwa wakipigana vikumbo kutaka kufanya kazi na wakali hao ili nao kusogea mbele.

                     

Hata hivyo, kutokana na ushindani wao kimuziki ulizaliwa uhasama wa kikazi wenye timu mbili ndani yake zinazohusisha mashabiki, wasanii wenzao, watayarishaji muziki, wadau n.k.
Jambo hilo limepelekea baadhi kuchagua upande na hivyo kushindwa kufanya kazi na upande mwingine lakini wapo wasanii ambao wameweza kuwashirikisha na kushirikishwa katika nyimbo za Alikiba na Diamond.

                      

1. Waliowashirikisha Alikiba na Diamond

Katika Bongo Fleva kuna wasanii wengi waliofanikiwa kuwashirikisha Alikiba na Diamond katika nyimbo zao ila rekodi zinaonyesha huchukua muda kidogo hata zaidi ya miaka mitatu hadi hilo kukamika, hawa ni baadhi.


A. Nay wa Mitego

Rapa huyo kutokea Free Nation amemshirikisha Diamond katika nyimbo zake mbili, Muziki Gani (2013) na Mapenzi au Pesa (2016) ambazo zilifanya vizuri na kumuongezea mashabiki huku huo wa kwanza ukishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA).

Baada ya miaka minane akakutana na Alikiba studio na kumpa shavu katika wimbo wake ‘Nikikuona’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Rais wa Kitaa (2022), iliyotoka na nyimbo 14 na kuwashirikisha wakali wengine kama AY, Jux,  Maua Sama, Marioo n.k.


B. Chege

Miezi miwili iliyopita Chege kutoka TMK Wanaume Family aliachia wimbo wake, Kipofu (2024) akimshirikisha Alikiba, Mkurugenzi Mtendaji wa Kings Music ikiwa ni miaka minane tangu alipotamba na kolabo yake na Diamond, Waache Waoane (2016).

Ikumbukwe video ya wimbo ‘Waache Waoane’ iliyofanyika Afrika Kusini na Director Justin Campos ndio ilikuwa ya kwanza kwa Chege kutazamwa (views) zaidi ya mara milioni 1 katika mtandao wa YouTube na sasa ikiwa imefikisha milioni 29.


C. Navy Kenzo

Kundi la Navy Kenzo linaloundwa na Nahreel na Aika tangu mwaka 2013, katika albamu yao ya kwanza, AIM (Above Inna Minute) (2016), walimshirikisha Alikiba katika wimbo ‘Lini’ ingawa walishindwa kutoa video yake licha ya kupendwa na wengi.

                      

Na kipindi wanasimamiwa na Sallam SK, Meneja wa Diamond, ndipo Navy Kenzo wakapata fursa ya kumshirikisha na staa huyo wa WCB Wasafi kwenye wimbo wao, Katika (2018) ambao nao video yake ilifanyika Afrika Kusini kwa Justin Campos.


2. Waoshirikishwa na Alikiba, Diamond

Kwa upande huu ni wasanii wachache Bongo wanaopata nafasi za kushirikishwa na Alikiba na Diamond kutokana wakali hawa wenyewe wanaogopa kupoteza ule ushindani wao, hivyo hutazama zaidi wale wa karibu yao au wasio na upande.


A. Chid Benzi

Mshindi huyu wa TMA 2006 kama Msanii Bora wa Hip Hop kupitia kolabo yake na K-Lynn, Miss Tanzania 2000, miaka ya nyuma alikuwa akishirikishwa sana na wasanii wenzake kutokana kila wimbo uliotoka ukiwa na sauti yake ulifanya vizuri.

Basi Alikiba akamuita Chid Benzi pale G Records na kutoa wimbo ‘Far Away’ uliojumuishwa katika albamu yake ya pili, Ali K4Real (2009), huku Diamond akimshirikisha Chid katika wimbo ‘Nalia na Mengi’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Kamwambie (2010).  

                       

B. Jay Melody

Katika Extended Play (EP) mpya na ya kwanza kutoka kwa Alikiba, Starter (2024) yenye nyimbo saba, amemshirikisha Jay Melody katika wimbo ‘Hatari’ unaofanya vizuri sasa ikiwa ni wiki tatu kuachiwa kwake.

Kolabo hiyo inakuja miezi nane tangu Jay Melody kupewa shavu na Diamond katika wimbo wake, Mapoz (2024) wakiwa pia na Mr. Blue ambaye awali alikutana na Diamond katika kolabo mbili, Nakupa Moyo Wangu (2010), na BBM (2011) wake Ngwea.

                     

C. Rude Boy (P-Square)

Kundi la P Square kutoka Nigeria linaloundwa na Mr. P na Rudeboy lilishirikishwa katika wimbo wa Diamond, Kidogo (2016) ambao uliandaliwa na maprodyuza watatu, Shirko, Laizer na V-Teck huku video ikisimamiwa na Director Godfather wa Afrika Kusini.

Baada ya kundi la P-Square kusambaratika, ndipo Alikiba akafanya kazi na Rudeboy pekee aliyesikika katika wimbo wake ‘Salute’ kutoka katika albamu yake ya pili, Only One King (2021) ambayo ilishinda tuzo ya TMA 2021 kama Albamu Bora ya Mwaka.


Wenyewe Wafunguka

Wakizungumza na gazeti hili, Mocco Genius, Queen Darleen na Director Ivan ambao wamewahi kufanya kazi na Alikiba na Diamond. Wameeleza jinsi ambavyo walifanikiwa kufanya kazi na wakali hao na upi mtazamo wao kuhusu kuchukua upande.

Mocco Genius ambaye sasa anaimba na alitajwa kuwania TMA 2023 ikiwa ni baada ya kuwatengenezea nyimbo Alikiba na Diamond akiwa kama Prodyuza, amesema hofu ndio inafanya baadhi ya wasanii kushindwa kufanya kazi waimbaji hao.

“Mtu anaona akifanya kazi huko na huku inaweza kumletea shida lakini sidhani kama kiuhalisia inakuwa na shida, kwa sababu suala la Prodyuza kufanya kazi na wasanii tofauti tofauti ndio jukumu lake la msingi, vinginevyo awe amekuajiri,” amesema Mocco.

Hadi sasa Mocco Genius kutoka Imagination Sound, ametengeneza nyimbo za Alikiba kama ‘Mshumaa’, ‘Mwambie Sina’ na ‘Toto’ za Kings Music, pia katengeneza nyimbo za WCB Wasafi kama ‘Cheche’ ya Zuchu na Diamond, ‘Maajab’ ya Mbosso n.k.

Kwa upande wake Queen Darleen ambaye ameshirikiana na Diamond na Alikiba katika nyimbo nyingi, amesema suala la msanii kufanya kazi na wakali hao kwa wakati mmoja halina shida hasa ikiwa lengo kuu ni biashara.

“Kibiashara haina shida yoyote kwa sababu wasanii wote wanatafuta riziki, kwa hiyo kama mtu akiamua kufanya biashara yake iwe sehemu moja basi ndio riziki yake alipoamua iwe hapo huwezi kumlazimisha,” amesema Queen Darleen.

Ikumbukwe Queen Darleen alivuma na kibao chake ‘Najua Nakupenda’ akimshirikisha Alikiba, huku akikutana na Diamond katika kolabo mbili za WCB Wasafi, Zilipendwa (2017) na Quarantine (2020).

Director Ivan ambaye ameongoza video ya wimbo wa Alikiba, Utu (2022) na ile ya Diamond, Mapoz (2024), amesema kutanguliza ueledi mbele kuliko utimu ndio siri ya kuendelea kuaminiwa na wasanii hao na wengine wengi.

“Mpaka anakuamini anakupa kazi anajua wewe ni msiri huwezi kutoa kitu cha huko ukapeleka kule, hata kama video nimeshuti na huyu siwezi kumuonyesha yule. Hivyo mimi sipo kwenye timu yoyote, naongea vizuri na Alikiba pamoja na Diamond,” amesema Ivan.

Ukiachana na hizo za Diamond na Alikiba, Director Ivan ameongoza video kama ‘I Made It’ ya Harmonize, ‘Dangerous’ ya Joh Makini, ‘Nitachelewa’ ya Ibrah, ‘Penzi la Bando’ ya Weusi, ‘Mapenzi’ ya Rich Mavoko, ‘Sitaki’ ya Mbosso, ‘I love My Self’ ya Lady Jaydee n.k.