Konde Boy amuomba msamaha Diamond

Muktasari:
- Kupitia Insta Story yake, Harmonize ameandika kuwa anatumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kuomba msamaha kwa yeyote aliyemkosea, akisisitiza kuwa hana tena nafasi ya kutoelewana na mtu yeyote
Dar es Salaam. Nyota wa Bongo Fleva, Harmonize a.k.a Konde Boy amemuomba msamaha Diamond Platnumz kwa tofauti zilizowahi kutokea kati yao, ikiwamo cha siku ya karibuni wakiwa visiwani Zanzibar.
Kupitia Insta Story yake, Harmonize ameandika kuwa anatumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kuomba msamaha kwa yeyote aliyemkosea, akisisitiza kuwa hana tena nafasi ya kutoelewana na mtu yeyote.
"Naungana na waislam wenzangu kumuomba Mungu msamaha wa makosa yetu tuliyoyafanya kwa kukusudia na kutokusudia bila shaka Mungu ni Mwingi wa kusamehe atatusamehe In Shaa Allah.
Kipekee kabisa nimuombe msamaha yeyote niliyemkosea, kwani bado nina sifa za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kukosea!!!"
"Kutoka ndani ya moyo wangu kwa dhati kabisa!! Nimemsamehe yeyote tuliyekwazana kwa lolote!! Kupitia mwezi huu mtukufu, nitahakikisha kila changamoto na tofauti zozote nazitatua!! Namuomba Mungu kupitia neema ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ulete mapatano, maridhiano na kazi ziendelee.

kila anaye soma maandiko haya anamchango wa aina yake katika maisha yangu!!!! "
Tarehe 15 mwezi huu wa tatu In Shaa Allah natimiza miaka 31, Alhamdulillah namuomba Mungu uhai, afya pamoja na riziki ninayostahili. kipekee kabisa sitaki kuhusishwa au kutajwa katika tofauti zozote zile kwani hazimpendezi mungu, binafsi nimezichoka."
"Safari yangu ya Zanzibar imenivutia, bila shaka imekuwa kama ukumbusho kwangu, kwamba maisha ya upendo ni bora zaidi kwa namna yoyote ile. Sikutakiwa kurushiana maneno na my brother Naseeb, so sorry my brother, i apologize, nilichelewa kutambua hakuna mkamilifu. tuliyofanya pamoja ni mazuri na ni mengi kuliko shetani aliyekati yetu. sioni haja na faida yake!!!!"
"Mwezi mtukufu wa ramadhani huleta amani na upendo kwa watu wote"
Tujikumbushe
Ilikuwa mwishoni mwa mwaka 2019, Harmonize aliamua kuondoka katika Lebo ya WCB ya Diamond Platnumz akiwa ni msanii wa pili kufanya hivyo baada ya Rich Mavoko aliyedumu hapo toka Machi 2016 hadi Julai 2018.
Hata hivyo, kuondoka WCB haikuwa kazi rahisi, kwa mujibu wa Harmonize mwenyewe alidai kuwa ili kuvunja mkataba wake wa miaka 10 na lebo hiyo, ilimlazimu kulipa Sh 600 milioni
Mwaka mmoja baadaye, Harmonize akaondoka katika lebo hiyo, mgogoro wa kimaslahi na kile alichokiita kunyanyapaliwa, ndivyo vilipelekea kuchukua maamuzi hayo.
Mkataba wao ilikuwa ni kwamba kila ambacho Harmonize ataingiza kupitia muziki, basi Diamond (WCB Wasafi) atachukua asilimia 60 na Harmonize asilimia 40. Ukiwa mkataba huo wa miaka 10 ulisaniwa rasmi mwaka 2015, basi ungemalizika mwaka 2025, hivyo Harmonize alitumikia takribani miaka minne tu ya mkataba huo
Oktoba 24, 2019 Harmonize alihojiwa na kipindi cha XXL cha Clouds FM, alidai kuwa ili kuvunja mkataba wake na WCB ilimlazimu kulipa Sh 500 milioni ila baadaye zikaongezeka Sh100 milioni, kutokana hakuwa na fedha hizo ilimlazimu kuuza hizo nyumba zake tatu.
“Kiukweli sikuwa na fedha, nikauza baadhi ya mali zangu, kuna sehemu nilikuwa na nyumba kama tatu ilinibidi niuze, tukalipa," alisema Harmonize.

Novemba 19, 2021 Harmonize akizungumza na Wanahabari Uwanja wa Ndege Dar es Salaam (JKIA), alidai licha ya kulipa fedha hizo, WCB hawakumpatia hati ya kuvunja mkataba, baada kuzungushwa sana aliamua kumtumia Hayati Rais John Magufuli.
“Nikaamua kumpigia simu Rais Magufuli nikamuelezea kile kinachoendelea na namshukuru sana, kwani aliagiza nipewe hati ya kuvunja mkataba. Nakumbuka siku hiyo Diamond alikuwa anasafiri kwenda ziarani Marekani, wakatakiwa wasiondoke bila kunipa hati,” alisema Harmonize.