Kinachofanya Weusi wajiite Ronaldo

Muktasari:
- Miaka zaidi ya 10 wakitoa burudani kwa mashabiki wao, Weusi wameshinda tuzo, wametoa albamu, wameshiriki matamasha yote makubwa ya ndani huku wakilamba dili nyingi za ubalozi. Hawa ndio Weusi.
Dar es Salaam. Hadi kufikia sasa Weusi ni miongoni mwa makundi machache katika Bongofleva yaliyofanikiwa kudumu kwa kipindi kirefu na kuwa na mwendelezo mzuri wa kutoa kazi ambazo zimekuwa zikipata mapokezi mazuri.
Miaka zaidi ya 10 wakitoa burudani kwa mashabiki wao, Weusi wameshinda tuzo, wametoa albamu, wameshiriki matamasha yote makubwa ya ndani huku wakilamba dili nyingi za ubalozi. Hawa ndio Weusi.

Kundi la Weusi ilizaliwa kufuatia kuvunjika kundi la Nako 2 Nako, hivyo G Nako na Lord Eyes wakajiunga na Nikki wa Pili, Joh Makini na Bonta ambao nao walitokea kundi la River Camp, kisha wakanzisha Weusi.
Weusi katika Hip Hop wanajifananisha na Cristiano Ronaldo, mshambuliaji wa Ureno ambaye bado anacheza soka la kulipwa huko huku Saudi Pro League katika klabu ya Al Nassr FC licha ya kufikisha umri wa miaka 40.
Sasa idadi ya wasanii wa kundi la Weusi ni sawa na tuzo za Ballon d'Or alizoshinda Ronaldo, pia ni sawa na mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) aliyobeba, ndipo Weusi wakatoa wimbo wao, Ronaldo (2022) uliyotayarishwa na S2kizzy kutokea Pluto Republic.

Hata hivyo, awali Lord Eyes alikuwa na kundi la Hood Squard Hardcore Unit, akiwa na wenzake, JCB na Spark Dogg, baadaye akaungana na G Nako na Bou Nako kutokea Chronic Mob ndipo wakaunda Nako 2 Nako.
Kwa ujumla kundi la Weusi linaundwa na wasanii watano ambao ni G Nako, Nikki wa Pili, Joh Makini, Lord Eyes na Bonta ambaye amekuwa hasikiki sana kwenye kazi zao kwa kile kinachotajwa ni kujikitia kwenye kazi yake ya udaktari.
Ikiwa ni miaka 13 tangu kuanzishwa kwake, hadi sasa Weusi wamefanikiwa kutoa wimbo mmoja pekee ambao umekutanisha wasanii wote watano wa kundi hilo. Wimbo huo, Watoto wa Mungu (2013) ilitoka chini ya Bongo Records kwa P-Funk Majani.
Wimbo wa kwanza kuwapatia mafanikio ni Gere (2013) uliojumuisha wasanii watatu, G Nako, Nikki wa Pili na Joh Makini, ni wimbo uliowafanya kushinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) 2014 kama Wimbo Bora wa Hip Hop na Kundi Bora la Mwaka.
Mtayarishaji wa wimbo huo kutoka studio ya The Industry, Nahreel hakuamini iwapo G Nako anaweza kufanya vizuri kwenye Gere wakati wakirekodi kutokana na aina yake ya muziki ila ulipotoka tu, ukawa gumzo la jiji.
Kwa miaka yote ya kufanya kazi pamoja, ni wasanii wawili tu ambao hawajawahi kukosekana kwenye wimbo wowote wa kundi la Weusi, nao ni G Nako na Joh Makini, rapa aliyetoka kimuziki na kibao chake, Chochote Popote (2006).
Lord Eyes alikosekana katika wimbo wao, Mdundiko (2018), Bonta akikosekana katika albamu yao yote ya kwanza na ya pekee, Air Weusi (2021) huku Nikki wa Pili akikosekana kwenye nyimbo kama Waoshe (2021), Hujabalehe (2022), Booty Hammer (2024) n.k.
Na tangu Nikki wa Pili kuteuliwa hapo Juni 2021 kuwa Mkuu wa Wilaya Kisarawe kisha Kibaha, hajatokea katika video yoyote ya Weusi licha ya kusikika katika nyimbo kama Ronaldo (2022) na Hii Hapa (2024).
Akiwa bado hajafanikiwa kimuziki, Whozu alionekana katika video ya kundi laWeusi, Nicome (2017), hiyo ni sawa na Mimi Mars
alipotokea katika video ya kundi la Navy Kenzo, Game (2015) kipindi bado hajatoa wimbo wowote.

G Nako hakuwepo wakati wenzake wanashuti video ya wimbo wao, Wapoloo (2019), hivyo vipande vyake vyote unavyoviona katika video hiyo alishuti peke yake kisha akatuma kwa director wa video hiyo.