Humu tu, miaka miwili ya ndoa ya Billnass na Nandy

Muktasari:
- Wawili hao waliofunga ndoa Julai 16, 2022 katika Kanisa la KKKT Mbezi Beach, Dar es Salaam, wiki hii wamesherehekea miaka miwili ya ndoa yao ambayo imejaliwa mtoto mmoja, Naya aliyezaliwa Agosti 2022.
Dar es Salaam, Miaka miwili ndani ya ndoa, Billnass, 31, na Nandy, 32, wamefanikiwa kupingana na kuishinda ile dhana kuwa wanamuziki wanapooa au kuolewa ushawishi wa sanaa yao hushuka kutokana na kupoteza mvuto kwa mashabiki wengi.
Wawili hao waliofunga ndoa Julai 16, 2022 katika Kanisa la KKKT Mbezi Beach, Dar es Salaam, wiki hii wamesherehekea miaka miwili ya ndoa yao ambayo imejaliwa mtoto mmoja, Naya aliyezaliwa Agosti 2022.
Kama wanavyosema Weusi katika wimbo wao mpya, Humu Tu (2024), yaani ushindi tu, ndivyo ilivyo katika ndoa ya Billnass na Nandy ambao kwa mara ya kwanza walikutana mwaka 2016 wakiwa wanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) Dar es Salaam.
Hakuna kipindi Billnass amefanya vizuri kimuziki kama baada ya kuingia kwenye ndoa, ameshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) kwa mara ya kwanza na kutoa nyimbo zilizopata namba kubwa katika majukwaa ya kidijitali kuliko zote za mwanzo akiwa bachela.
Akiwa na miaka minane katika muziki tangu alipotoka na wimbo wake, Raha (2014) chini ya Rada Entertainment, hapo Mei 2023 Billnass alishinda tuzo ya TMA kwa mara ya kwanza kupitia kipengele cha Msanii Bora wa Kiume wa Hip Hop 2022.
Kinyang’anyiro cha TMA 2015 na 2021, Billnass hakushinda ila baada ya kuingia tu katika ndoa, basi ikawa baraka kwa kushinda mbele ya wakali wa Hip Hop kama Fid Q, Joh Makini, Country Wizzy na Kala Jeremiah.
Ushindi huo ulikuja baada ya Billnass kufanya vizuri na wimbo wake, Puuh (2022) ambao uliweka rekodi kama wimbo wa Bongofleva uliosikilizwa zaidi katika Jukwaa la Boomplay Music kwa mwaka uliopita ambapo uliongoza chati kwa wiki sita mfululizo.
Hadi sasa wimbo huo ambao amemshirikisha Jay Melody ndiyo wimbo pekee wa Billnass uliosikilizwa zaidi Boomplay ukiwa na ‘streams’ zaidi ya milioni 53.3, pia ndiyo wimbo wake ambao video yake imetazamwa zaidi YouTube kwa muda ikiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 13.
Kwa upande wake Nandy, licha ya kuanzisha lebo yake, The African Princess miaka mingi nyuma, hakuweza kumsaini msanii yeyote ni hadi pale alipoingia kwenye ndoa ndipo akamsaini Yammi, 22, hapo Januari 2023 akiwa ni msanii wa kwanza.
Ikumbukwe wazo la kufungua lebo lilianza tangu Nandy alipoachia albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) chini ya Epic Records inayomilikiwa na Sony Music Entertainment, kampuni tanzu ya Sony Corporation of America.
Katika lebo Nandy amefanikiwa kwa sababu Yammi anafanya vizuri kimuziki, Yammi ni msanii wa tatu wa kike Bongo aliyesikilizwa zaidi Boomplay kwa mwaka uliopita akiwa ametanguliwa na Zuchu na Nandy ambao ni wakubwa kwake kimuziki na hata kiumri.
Yammi ambaye amejiunga na kampuni kubwa ya usambazaji muziki Afrika na India, Ziiki Media yenye ushirikiano na Warner Music Group, nyimbo zake kali kama Tiririka (2023) zimejizolea mamilioni ya wasikilizaji YouTube zikiwa na jumla ya ‘views’ milioni 18.2.
Akiwa ndani ya ndoa, Nandy anatolewa kimasomaso na wimbo wake, Dah Remix (2024) akimshirikisha Alikiba ambao umekuwa wa kwanza kwake kwa video yake yake kufikisha ‘views’ zaidi ya milioni 14 pale YouTube ndani ya miezi mitano tu!
Kabla hajaolewa hakuna wimbo wake ulioweka rekodi hiyo, hata ule wa kwanza kumshirikisha Alikiba, Nibakishie (2020) uliotoka miaka mitatu iliyopita hadi leo haujafikia hata nusu ya namba ulizopata ‘Dah!’ iliyoachiwa baaada ndoa yake na Billnass.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kuanzia uhusiano hadi ndoa yenye mafanikio, mathalani Aprili 2018 walikumbwa na tukio la aibu baada ya video yao ya faragha kusambaa mtandaoni kitu ambacho kilitazamiwa kuharibu kabisa kazi yao ila kwa bahati nzuri haijawa hivyo.
Billnass na Nandy ambao wameyaimba mapenzi yao katika nyimbo nne walizoshirikiana ambazo ni Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021) na Bye (2022), kwa sasa mashabiki wanasubiria kwa hamu kubwa wimbo wao wa kwanza pamoja baada ya kufunga ndoa.
“Mume wangu miaka miwili ya ndoa yetu imekuwa fundisho kubwa kwangu kujua upendo ni kitu muhimu sana, uwepo wako umerahisisha maisha yangu na ya kipenzi chako Naya, jua tu tunakupenda sana.” Ni ujumbe wa Nandy kwa Billnass.
Baada ya mtoto wao Naya kutimiza mwaka mmoja ndipo sura yake ilionekana mtandaoni na kufunguliwa ukurasa wake wa Instagram ambao sasa una wafuasi zaidi ya 439,000, huku akiwa balozi wa bidhaa mbalimbali za watoto.
“Mwenyezi Mungu pamoja na wazazi wako naamini walikuandaa kwa ajili yangu, na nakuahidi utafurahi mpaka siku yangu ya mwisho kwenye hii dunia, nakupenda Nandy.” alisema Billnass.
Katika ndoa yao kila mmoja ana biashara zake moja au mbili anazojishughulisha nazo, Nandy ana lebo yake, The African Princess, anauza bidhaa za urembo na ana kampuni inayohudumia maharusi, huku Billnass akiuza bidhaa za kieletroniki hasa simu.