Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hekaya za Mlevi: Angalia usiue brandi yangu

Muktasari:

  • Wanasema uungwana ni kutomfanyia mwenzako kitu ambacho usingelipenda mtu mwingine akufanyie. Lakini ngurumbili hawaishiwi vituko, wao wanaiga hulka za watoto wadogo wasiojitambua. Nyakati zingine wanafanana na “kasongo” anayemtingisha chui aliyelala kwa kutegemea mbio zake. Huu ni usumbufu uliopitiliza je, akikamatwa? Akiliwa atamlaumu chui?

Dar es Salaam. Wanasema uungwana ni kutomfanyia mwenzako kitu ambacho usingelipenda mtu mwingine akufanyie. Lakini ngurumbili hawaishiwi vituko, wao wanaiga hulka za watoto wadogo wasiojitambua. Nyakati zingine wanafanana na “kasongo” anayemtingisha chui aliyelala kwa kutegemea mbio zake. Huu ni usumbufu uliopitiliza je, akikamatwa? Akiliwa atamlaumu chui?

Juma lililopita nilikuwa safarini kuelekea Korogwe Mashewa. Nilienda kufuata nini, nitawaambia wakati utakaporuhusu. Kwa kuwa sina uzoefu na safari za huko, nilikata tiketi siku moja kabla ili kuepuka usumbufu. Hapa utaona ni jinsi gani sipendi usumbufu. Nilichagua basi kwa kigezo cha kampuni iliyodumu kwa muda mrefu kwenye ruti, maana wakongwe hujiongeza kadiri ushindani unavyoongezeka.

Isivyo bahati, nikachagua kampuni ya Wandewa ambao hawatofautiani na wazee wa kimila huko vijijini mwao. Miaka mingi iliyopita nilitembelea kijiji kimoja mitaa ya huko, nikajifunza baadhi ya mila na desturi zao. Kamusi yao haikuwa na maneno ya “haraka”, “bize” wala “fasta”. Mambo yalikwenda taratibu kiasi kwamba ingelikuwa ni Kariakoo basi pasingepitika. Kinamama walitua ndoo za maji na mizigo ya kuni kusalimia watu njiani.

Maeneo yote yalikuwa ni ya wenyeji waliorithi kutoka kwa wazee wao. Hawa warithi waligeuka kuwa wazee hata kama walikuwa na umri mdogo. Pindi ulipokutana na mzee wa eneo unalopita ilikupasa “kutoghoa”, yaani kumsalimu kwa kumsifu, kumshukuru na pengine kumwachia zawadi kama umebeba mizigo. Halafu ungemhadithia safari yako nzima tangu ulikotoka hadi pale ulipofika. Kama ulikutana na kenge au mjusi ungesema. Mzee angelipokea salamu zako, kisha kukubariki uendelee na safari yako.
 
Mambo haya niliyaona zaidi ya miaka 20 iliyopita. Kumbe bado yapo kwani basi nililosafiri nalo halikuwa na haraka hata kidogo. Katika kila kituo ambacho basi lilisimama, kuliteremshwa mifuko midogo ya karatasi na kupatiwa vijana waliokuwa wakicheza bao pale. Maagizo yalikuwa: “Huo wa Mzee Shemboza, lakini pitisha kwanza huu kwa  Shemzughi”. Nilihisi zilikuwa ni zawadi za wazee.

Hilo silo lililonikera, kwani ni sehemu ya mila na desturi. Wanasema ukikuta Wagagagigikoko wanasalimiana kwa kupigana makwenzi, basi nawe huna budi kujitayarisha kwa salamu hizo. Kilichonikera ni baada ya mwendo mfupi kutoka Dar, aliingia mtu mwenye mavazi ya kimasai. Siwezi kujua alikuwa kabila gani kwani hata Wamakonde huvaa kimasai wakati wa kuomba kazi ya ulinzi. Wahuni wengine hutumia mavazi hayohayo kuuzia dawa na ugoro.

Mtu huyo aliketi kwenye siti ya kando yangu. Kitu cha kwanza nilichokihisi ni mabadiliko ya hali ya hewa tuliyotoka nayo. Ghafla nikahisi harufu ya jasho miksa tumbaku na ugoro. Nikajifanya kuwa bize kutazama ramani kwenye simu yangu, lakini jamaa akanigusa kiwikoni: “Rafiki!” Nikamtazama usoni naye akanionesha chupa ndogo ya plastiki ya pombe kali iliyo maarufu sana kule mtaani. 

Nikakataa kwa kichwa, akanielekeza “hii inatoa uchofu”. Nikamjibu “itanisumbua”. Akatikisa kichwa kwa namna ya kunisikitikia, kisha akainywa. Kutokea hapo sikuwa na amani tena. Mimi ni mlevi, lakini najua jinsi pombe inavyotaka adabu. Kama unataka kunielewa vizuri, kunywa pombe asubuhi kabla hujagusa kitu kingine. Ghafla utabanwa na haja ndogo ambayo itakuwa na ubishi wa kushindwa kuvumilika. Kadiri ya utakavyoendelea kuibana, ndivyo mawazo ya maliwato yanavyozidi kuongezeka. Mwisho wa siku breki zitafeli, na unajua kitakachotokea.

Huyu jamaa yetu yalimkuta hayo. Alimwomba utingo asimamishe basi ili ajisaidie. Utingo akapuuza na kumwuliza kwa nini alisahau pampasi. Mimi nilimtazama kwa macho ya “si nilikwambia inasumbua hiyo?” Na yeye kwa kutokubali matokeo, akakunja nne kwenye siti yake na kuendelea kuubana. Lakini kwa mbali nilimwona akiwa anakata viuno kwa siri, nikajua ngoma imemfika mlangoni!

Amani ilinitoweka kabisa. Nilijua mwisho wa mawingu mvua, huyu jamaa ni lazima atalimwaga kojo kabla ya kufika stendi. Nilijuta kwa nini niliamua kusafiri siku hiyo. Pengine ningekuja kulipia nauli pale kituoni nisingepata siti inayoambatana na ya huyu msumbufu. Nikajikuta nikimwita utingo na kumwomba amsaidie huyu chizi, vinginevyo tungeathirika sote. 

Utingo alikataa katakata: “Huyu ni msumbufu sana. Mwanzoni alitudanganya na umasai, lakini wamasai wanamkataa. Hivi atanisumbua nauli mpaka nitamshusha porini...” Wakati utingo anamkanyagia, jamaa alifunua shuka lake na kumimina kojo kwenye kichupa kitupu alichonywea pombe. Mimi nilinyanyuka haraka kutoka kwenye siti, kumbuka nilipata siti ya dirishani. Nikajua ni lazima mashambulizi yatahamia kwangu.

Nikamruka na kusimama upande wa nyuma ya basi. Kumbe sikuwa mimi pekee niliyejihami na dhoruba ile, utingo na abiria wote walioshuhudia sakata hilo walicharuka. Wengine walimtaka dereva asitishe msafara watafute usafiri mwingine.

Ilibidi busara itumike na mlugaluga yule akateremshwa na wengine tukaendelea na safari. Nilishangazwa sana mambo ya zama za mawe kuonekana nyakati hizi za sayansi na teknolojia. Mimi nilidhani ni vibaka tu ndio wanaoficha uhalisia wao kwa utanashati. Kumbe kuna watu wanajifanya washamba kuficha ununda wao.