Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Harmonize anavyosuka mwelekeo wa muziki wake

Muktasari:

  • Uzinduzi wa albamu hiyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, ulihudhuriwa na watu kutoka sekta mbalimbali huku mgeni rasmi akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Wikiendi iliyopita Jumamosi, Mei 25, 2024 mwanamuziki Rajabu Abdul ‘Harmonize’ alifanya uzinduzi wa albamu yake aliyoipa jina la ‘Muziki wa Samia’.

Uzinduzi wa albamu hiyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, ulihudhuriwa na watu kutoka sekta mbalimbali huku mgeni rasmi akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Albamu hiyo yenye jumla ya nyimbo kumi ambazo ni ‘Tunatamba Naye’, ‘Anatekeleza’, ‘Samia Tena’ ,‘Tanzania’, ‘Mama Anajenga’ , ‘Mama Teacher’, ‘Tuvushe’ na nyinginezo,  inaenda kuwa albamu yake ya tano tangu alipoanza rasmi kukitumikia kiwanda cha Muziki wa Bongo Fleva mwaka 2015.

Albamu hiyo ya Harmonize, ‘Muziki wa Samia’ imezua mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya wadau wa muziki wakidai kuwa huenda isifanye vizuri kutokana na asilimia kubwa ya mashairi yake kutaja majina ya baadhi ya watu.

Huku wengine wakipinga na kudai majina hayo yanaweza kuwa chanzo cha albamu hiyo kufanya vizuri kuliko albamu za nyuma.  

Hata hivyo, ikumbukwe kuwa Harmonize siyo msanii wa kwanza kutoa ngoma zenye kutaja majina ya watu, kwani wapo wengine waliowahi kuachia ngoma za namna hiyo kwa kutaja majina ya viongozi wa serikali, wanamichezo na wafanyabiashara maarufu.

Kama alivyowahi kufanya Diamond kwenye ngoma yake iitwayo ‘Simba’ iliyotoka miaka mitatu iliyopita alisikika akitaja majina ya baadhi ya watu kama vile Haji Manara wakati akiwa Simba.

Huku wa Harmonize ametaja majina kama Mariam Mwinyi, Anna Makinda, Sophia Kawawa na wengine. 

Marioo, mwaka mmoja uliopita alitoa wimbo uitwao ‘Yanga Anthem’ ndani ya ngoma hiyo alitaja majina ya baadhi ya wachezaji wa Yanga akiwemo Fiston Mayele, Feisal Salum na Yannick  Bangala, lakini kwa sasa wachezaji hao wote hawapo ndani ya klabu hiyo.

‘Ate’ ngoma ya Mbosso iliyotoka mwaka 2020 ina mistari ambayo mwanamuziki huyo ametaja jina la Diamond na aliyekuwa mpenzi wake Tanasha, akiyatumia majina hayo kama mfano wa watu wanaopendana. Lakini kwa sasa wawili hao hawapo tena pamoja.

Aidha Sir Jay mwaka mmoja uliopita, aliachia ngoma iitwayo ‘Ndo huyohuyo’, pia kwenye ngoma hii mwanamuziki huyu ametaja majina ya wachezaji mbalimbali kama vile Feisal Salum, ambaye kwa sasa hayupo tena Yanga.

Yaliyotokea kwenye nyimbo hizi na nyingine zenye majina ya watu ndiyo yanasababisha mijadala hiyo na mashaka kwa mashabiki, wakidhani kuwa kuna wakati nyimbo hizo zinaweza kupoteza maana na kukosa uhalisia  kutokana na mabadiliko mbalimbali ambayo hutokea kwa watu.

Ni afya msanii kuimba mistari inayotaja majina ya watu?

Marco Chali

Akizungumza na gazeti hili mzalishaji mkongwe wa muziki nchini Marco Chali amesema utumiaji wa majina kwenye muziki siyo afya sana lakini pia hauna athari mbaya kwani kila msanii huwa na malengo yake.

“Nadhani kutumia majina ya watu fulani kwenye kutengeneza muziki wako kunaweza kukuletea nafasi nzuri kwenye mauzo endapo jina ambalo umetumia linahusisha watu mbalimbali ambao wanatumia jina hilo lakini kwa mimi ninavyoona siyo mbaya sana na wala si nzuri kwa sababu tunatofautiana malengo na mawazo na namna tunavyotaka kazi zetu ziwafikie watumiaji,” alisema Marco Chali.

Mkubwa Fella

Kutokana na ukongwe wake kwenye tasnia ya muziki akiwa kama msimamizi wa wasanii mbalimbali Said Fella  ‘Mkubwa Fella’ amebariki kitendo cha wasanii kutumia majina ya watu kwenye kazi zao.

“Ni swala jema kwa wasanii kufanya hayo, mfano nchi yetu ina utaratibu, inafika wakati mnaacha biashara mnatetea nchi maana nchi ikiwa salama nyinyi mnaweza kufanya lolote, mfano mataifa mengine Afrika hawachezi wala hawana burudani ya aina yoyote, kwa hiyo kuna muda tunafanya hivyo kwa sababu ya usalama maana pakiwa na shari mambo yanakuwa hayaendi vizuri,” alisema.

Jabir Saleh

Kwa upande wa mtangazaji mkongwe wa vipindi vya burudani  Jabir Saleh, amesema hakuna shida kwa msanii kufanya hivyo huku akitolea mfano wimbo wa Joyner Lucas kutoka Marekani ambaye mwanzo hadi mwisho wa mashairi yake alikuwa akimtaja na kumsifia mwigizaji Will Smith.

Wadau wa muziki

Hata hivyo, kwa upande wa mdau wa muziki Abdul Juma wa Tabata Kimanga amesema kikubwa kazi ifike kwa wasikilizaji.

“Sidhani kama ni sawa sana lakini pia sioni kama kuna ubaya kwa wasanii kutumia majina fulani ya watu kuhusisha sanaa yake cha msingi kazi inafika kwa watu na wanasikiliza ni jambo zuri,”alisema

Mwanahawa Issa mkazi wa Zanzibar ambaye pia ni mdau wa muziki amesema suala hilo halina afya kwa kazi za sanaa endapo likizidi.

“Mimi jamani naona siyo sawa kwa sababu msanii akiimba nyimbo zote anataja tu majina inachosha lakini kama ikitokea kwa mara moja moja inakuwa sawa shida ni kwamba mashabiki tunataka kusikiliza muziki mzuri na siyo majina mwanzo mwisho,”alisema.

Naye Peter Mkumbo, mkazi wa Arusha amesema kufanya hivyo kunaweza kupoteza maana halisi ya wimbo kwani watu hubadilika.

“Unajua mambo yanabadilika sana na sisi binadamu tunabadilika sasa leo hii unaimba unamtaja mtu fulani  na mahusiano yake lakini baada ya muda hao watu wameachana mnabaki kusikiliza wimbo lakini tena unakuwa hauna uhalisia,” alisema.