Prime
Hamisa ana nyota au anatazama fursa?

Mwanamitindo Hamisa Mobetto kwa sasa uhusiano wake na mchezaji wa Yanga SC, Aziz Ki ndio habari ya mjini, picha na video za bata lao huku Dubai zimegeuka gumzo huku wakiahidi mambo mazuri mbeleni.
Lakini uhusiano huu unaacha swali moja iwapo Hamisa ana nyota ya kupendwa kweli au anatazama fursa?, hii ni kwa sababu kulingana na historia yake amekuwa akihusishwa kutoka na watu wenye nguvu ya ushawishi na kifedha.
Hamisa ambaye ni mwanamke wa pili Afrika Mashariki kuwa na wafuasi wengi Instagram akiwa nao milioni 11.9, amekuwa maarufu hasa kutokana na mitindo kitu kinachofanya kutazamwa na wengi.

Ila linapokuja suala la mahusiano Hamisa anaonekana kutopenda kukaa kinyonge, watu wake ni wale ambao wanaweza kwenda nchi yoyote kwa ajili ya kutalii tu maana kwao fedha sio tatizo, miongoni mwao ni hawa wafuatao.
1. Majizzo - 2014
Septemba 2014 katika birthday ya Mkurugenzi Mtendaji wa E FM Radio na TV E, Francis Ciza maarufu kama Majizzo, ndipo Hamisa alimtambulisha kama mpenzi wake wakati akimtakia heri ya kuzaliwa kupitia Instagram.

Kipindi hicho ndipo E FM Radio ilikua imeanza, licha ya majukumu ya kiofisi Majizzo alikuwa anapata muda wa kumposti Hamisa Instagram na muda mwingine kumuita mke wake.
Kufika Desemba 2014 katika birthday ya Hamisa, Majizzo akatangaza kuwa yeye na mwenzake wanatarajia mtoto wao wa kwanza, na kweli Mungu akajalia mnamo Aprili 2015 wakapata mtoto wa kike na kumpa jina la Fantasy.
Hata hivyo, uhusiano huu hakudumu sana kwani kuanzia Machi 2016, Majizzo alianza kuhusishwa na muigizaji Elizabeth 'Lulu' Michael na miazi kadhaa wakaja kudhibitisha uhusiano wao na kuja kufunga ndoa hapo Februari 2021 na tayari wamejaliwa watoto wawili.
2. Diamond Platnumz - 2016
Tangu Februari 2014 Hamisa alihushishwa kutoka na Diamond Platnumz, Mkurugenzi wa WCB na Wasafi Media ingawa alikanusha jambo hilo na kusema haitowezekana kwa sababu anafahamu msanii huyo yupo na Wema Sepetu, Miss Tanzania 2006.
Hamisa alipokuja kutokea katika video ya wimbo wa Diamond, Salome (2016), tetesi za kuwa pamoja zikaibuka tena na wote wakakana ila Hamisa alipojifungua mtoto wake wa pili hapo Agosti 2017, ndipo Diamond akakiri walikuwa na uhusiano.

Suala hilo lilita mgogoro kati ya Diamond na aliyekuwa mpenzi wake, Zari The Bosslady kutokea Uganda ambaye Februari 2018 alitangaza rasmi kupitia Instagram kuachana na msanii huyo kwa madai ya kutoheshimu uhusiano wao.
Septemba 2018 Hamisa akiongea na Citizen Radio Kenya alidai alijuana na Diamond kitambo sana akiwa bado mwanafunzi, na hata kipindi wanaanzisha uhusiano alimuuliza kuhusu Zari na akamjibu anaweza kuoa hata wake wawili kitu ambacho alikuwa tayari.
3. Rick Ross - 2021
Rapa wa Marekani, Rick Ross ambaye ni Mkurugenzi wa Maybach Music Group, kila mara alikuwa anaacha ujumbe wa kuonyesha ni kiasi gani anampenda Hamisa katika picha na video alizokuwa anaposti mrembo huyo.
Kufikia Novemba 2021 Hamisa na Rick Ross akaonekana pamoja Dubai huku wakitajwa kuwa na uhusiano lakini baadaye walikuja kuonekana wote katika tangazo la moja ya kampuni za mawasiliano ya simu nchini.

Hata hivyo, pia ilikuja kubainika baada ya kazi hiyo kupita ukaribu wao uliishi hadi Rick Ross kuacha kumfuata (unfollow) Hamisa katika mtandao wa Instagram kitu kilichowakasirisha sana mashabiki wake.
Ikumbukwe Rick Ross alivuma kimuziki duniani baada ya kutoa wimbo wake, Hustlin (2006) na mwaka huo Jay Z akamsaini Def Jam Recording na kuachia albamu yake ya kwanza 'Port of Miami' iliyoshika nafasi ya kwanza chati za Billboard 200.
4. Kevin Sowax - 2023
Mnamo Septemba 2023 Hamisa alimtambulisha mpenzi wake mpya, Kevin Sowax kutokea Togo ambaye alikuja nchini na wote kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kutoa msaada kwa watoto wadogo wanaopambana na ugonjwa wa saratani.
"Tangu wakati nilipokuona nilijua wewe ndio mwenyewe, kadiri navyoendelea kukujua, hisia zangu zinaendelea kukua, nashukuru kuwa na wewe maishani mwangu, nafurahi juu ya nyakati zetu zijazo," alisema Kevin kuhusu Hamisa.

Kauli ya Kevin ilikuja mara baada ya kumzawadia Hamisa gari jipya aina Range Rover na kuteka mazungumzo mtandaoni, muda mfupi baadaye walionekana wakiwa pamoja huko Guangzhou nchini China lakini haikuchua muda wakaachana.
"Katika mahusiano yangu, naamini yale nilifurahia sana, hakuna chochote ninachoweza kujutia katika maamuzi niliyofanya ambayo naamini yalikuwa sahihi, ni mahusiano ambayo hayakunipa shida," alisema Hamisa hapo Juni 2024 baada ya kuachana na Kevin.
5. Aziz Ki - 2024
Mei 2024 ndipo tetesi za Hamisa kuwa na uhusiano na Aziz Ki zilianza baada ya kuonekana wakitoka wote Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) lakini Hamisa alikanusha hilo akisema wao ni marafiki tu.

Katika hafla ya tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyofanyika Agosti 2024 ndipo wakaweka wazi kuwa wao ni wapenzi na kuahidi kwenda pamoja Dubai kutalii baada ya Aziz Ki kushinda tuzo ya MVP.

Kufikia Februari 2025 mama mzazi wa Hamisa akadai kuwa mwanae na Aziz Ki walishafunga ndoa muda mrefu takribani miezi minne iliyopita na waliodhuria ni watu wachache, hivyo shughuli inayofuata ni kama kuweka jambo hilo rasmi kwa umma.
Aziz Ki aliyetua Yanga hapo Julai 2022 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ndiye alimfanya Hamisa kuhamia Yanga kama shabiki akitokea Simba, hilo linaendelea kuachwa ikiwa Hamisa anapenda na kupendwa kweli au ni mjuzi wa kutazama wapi penye fursa?