Filamu zinavyotumika kutunza, kulea watoto

Muktasari:
- Katika kuonesha umuhimu wa filamu Taasisi inayojihusisha na uandaaji wa tamasha la kimataifa la filamu Zanzibar, (ZIFF), katika miaka yake 27 tangu lianzishwe limeendelea kuonesha filamu zenye mlengo wa kitamaduni na maadili mema kwa watoto na jamii nzima.
Zanzibar, Katika dunia ya sasa ambayo teknolojia imeendelea kukua kwa kasi, filamu zimekua chombo muhimu cha kuburudisha, kuelimisha, kurithisha utamaduni na kulea watoto, endapo tu maudhui yake yakizingatia maadili.
Katika kuonesha umuhimu wa filamu Taasisi inayojihusisha na uandaaji wa tamasha la kimataifa la filamu Zanzibar, (ZIFF), katika miaka yake 27 tangu lianzishwe limeendelea kuonesha filamu zenye mlengo wa kitamaduni na maadili mema kwa watoto na jamii nzima.

Kwa mwaka 2024, ambapo ni tamasha la 27, wanafunzi wa shule ya Tamani iliyopo kijiji cha Matemwe kisiwani Zanzibar wamepata fursa ya kuoneshwa filamu iitwayo ‘Baada ya Masika’ yenye kuwajenga na kuwahimiza watoto kusimamia ndoto zao.
Akizungumza na Mwananchi mwezeshaji ZIFF katika kitengo cha Children Panorama, Mkubwa Hamad Hassan amesema kitengo hicho huwa na dhamira ya kuonesha filamu kwa watoto na kisha kuwauliza maswali kwa lengo la kuwafundisha.
“Kuna umuhimu wa watoto kuoneshwa filamu kwa sababu wanapenda sana kwa hiyo sasa hivi tumeamua kuweka jukwaa la watoto la filamu tunawafundisha wanapoangalia waziangalie kwa njia ya kuibua waliyojifunza.
“Siyo waige kwa sababu wakiiga wanachoona kwenye filamu watapotea kwa hiyo wajifunze mazuri wayafanyie kazi na mabaya wayaache, waangalie utamaduni wao na mambo mengine yanayohusu utamaduni hasa Wazanzibar,” amesema.
Hata hivyo, ameeleza kuwa filamu kabla ya kuoneshwa kwa watoto hupitiwa na kisha kuchaguliwa.
“Kwanza kunakuwa na bodi ya ZIFF inakaa ikishirikiana na bodi ya sensa wanazipitia na kuzikagua filamu kwa hiyo wanachagua za watoto,”amesema.
Aidha Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Tamani Foundation, Abdallah Mohammed amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa wanafunzi kuoneshwa filamu na siyo kusoma tu kwenye vitabu
“Kuna umuhimu mkubwa hasa wa kitamaduni wa watoto kuoneshwa filamu kwa sababu zina mafunzo, wanajifunza kupitia tamthilia siyo tu wanasoma kwenye vitabu lakini wanajifunza kwa kuona na kusikia sauti,”amesema.
Naye mwalimu Mariam Ally Said kutoka katika shule hiyo, amesema umuhimu wa kutazama filamu kwa watoto ni mkubwa sana hivyo liwe jambo endelevu.
“Umuhimu wa kutazama filamu watoto ni mkubwa sana kama hii tuliyoangalia ina mafunzo kwa watoto, tumeona ndoto ya Aisha aliipambania hadi kufanikiwa kwa hiyo watoto wanapata faida kwamba hata kama wanahitaji kitu watapitia kwenye changamoto wasikate tamaa wapambane na mwisho watafikia malengo.”
Mbali na walimu hao mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo aitwaye Nurr Bin Nasur amesema kupitia filamu aliyoona amejifunza kuwa na subira ili kufikia malengo.
Pia Ilham Ally Juma mwanafunzi wa darasa la saba wa shule hiyo amesema ni muhimu wanafunzi walio na ndoto kuzifanyia kazi.
“Katika filamu tuliyooneshwa nimejifunza kuwa kazi haihusiani na jinsia na hatutakiwi kuiga vitu vibaya, nawaomba watoto walio na ndoto wazifanyie kazi na wazifikie,”amesema.
Pamoja na hayo mdau wa habari na filamu Egbert Mtui ametoa rai kwa ZIFF kuendelea kuonesha filamu ambazo zina uhalisia na mazingira husika.
“Kwa upande wa ZIFF kuonesha filamu kwa watoto ni wazo zuri kwa sababu ni muhimu kuangalia namna ya kutengeneza vizazi vyetu kwa ajili ya kutunza utamaduni wetu kwa wakati ujao, lakini wangeendelea kutengeneza zile ambazo zinatoka kwenye mazingira yetu, lazima waoneshe ambavyo vipo kwenye utamaduni wetu.
“Kwa hiyo hata watoto waoneshwe zamani tulikuwa tunaishije ili waweze kuishi kama ilivyokuwa tangu zamani,”amesema.